Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetangaza kuzifunga kwa muda barabara nne zinaoingia katikati ya Jiji, ili kutoa nafasi kwa ugeni wa wakuu wa nchi wanaotarajiwa kukutana kesho, Jumamosi ya Februari 8, 2025.
Ugeni huo ni wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambao Rais Samia Suluhu Hassan ndiye mwenyeji.
Mkutano huo, unatarajiwa kuzungumzia mgogoro unaoendelea Mashariki mwa DR Congo baina ya majeshi ya Serikali dhidi ya vikosi vya M23.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa leo Ijumaa, Februari 7, 2025, barabara zitakazofungwa ni Nyerere kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kwenda katikati ya Jiji.
Nyingine ni Barabara ya Sokoine, Kivukoni na Lithuli kuanzia taa za Gerezani kwenda Hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.
Pia, Barabara ya Ohio kutokea Kivukoni kwenda Hoteli ya Serena na Barabara ya Garden kutokea Barabara ya Lithuli kwenda Hoteli ya Southern Sun.
Pia, Jeshi hilo limezuia bodaboda na bajaji kuingia kwenye maeneo ya katikati ya jiji hasa barabara zilizotajwa kwa muda kwa sababu za kiusalama wakati wa ugeni.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, katika kipindi chote cha mkutano, watumiaji wengine wa barabara wanashauriwa kutumia barabara za Uhuru, Kawawa kupitia Magomeni, Kigogo kuelekea Temeke, Barabara ya Morogoro na Msimbazi, Morogoro na Lumumba.
Kwa wale wanaotokea maeneo ya Chanika, imeshauriwa kuwa wanaweza kutumia njia mbadala ya mradi ya SGR ili kutokea Barabara ya Mandela na Uhuru.
“Jeshi litajitahidi kupunguza usumbufu kwa kufanya kazi ya ziada kwenye barabara hizo kwa kuzifunga na kuzifungua haraka kadri msafara utakavyokuwa unapita,” imeeleza taarifa hiyo.