Mahakama ya kijeshi yatoa hati kiongozi wa M23 akamatwe

M23 wanatajwa kufadhiliwa na Serikali ya Rwanda hata hivyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame   akizungumza na CNN alikanusha kuhusika kuwafadhili waasi hao.

Goma. Mahakama ya Kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imetoa hati ya kukamatwa kwa kiongozi wa umoja wa makundi ya waasi nchini humo ya Alliance Fleuve Congo (AFC/M23), Corneille Nangaa.

Shirika la Habari la AP limeripoti leo Februari 7, 2025, kuwa mahakama ya kijeshi nchini humo imetoa hati Nangaa akamatwe akituhumiwa kuhusika katika kile ilichotaja kuwa ni uasi na uhalifu wa kivita dhidi ya raia nchini humo.

Televisheni ya Taifa ya DRC nayo iliripoti kuwa hati ya kukamatwa kwa Nangaa imetolewa Jumanne Februari 4, 2025, baada ya kuhusika katika mauaji ya maelfu ya raia katika mapigano yaliyoibuliwa na wapiganaji wake katika Jimbo la Kivu Kaskazini nchini humo.

Mahakama hiyo katika hati yake imesema kutekeleza mauaji ya raia katika mapigano hayo ni kinyume cha sheria za nchi na sheria za kimataifa.

Imeamuru Nangaa akamatwe akiwa mahali popote atakapokutwa duniani na kufikishwa katika Mahakama ya kijeshi nchini DRC.

Mapigano ya wapiganaji wa M23, dhidi ya Jeshi la Serikali ya DRC la FARDC, yaliibuka Mashariki mwa nchi hiyo katika Mji wa Goma wenye wakazi wanaokadiriwa kufikia milioni 2. Waasi hao wameuteka mji huo na kuuweka chini yahimaya yao.

M23 wanatajwa kufadhiliwa na Serikali ya Rwanda hata hivyo, Rais Kagame katika mahojiano yake CNN alikanusha kuhusika na ufadhili wa kundi la M23, huku akisema hana taarifa kuwa kuna wanajeshi wa Jeshi la Rwanda wako nchini DRC.

Ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa jana (Alhamisi) ilisema idadi ya watu ambao wameuawa katika mapigano kati ya vikosi vya FARDC dhidi ya M23 imefikia zaidi ya 3,000.

Maelfu ya raia wameyakimbia makazi yao katika Mji wa Goma, wengi wao wakikimbilia nchini Rwanda, wakiwemo watumishi wa taasisi za kimataifa ikiwemo Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia.

Shirika la Kusaidia Binadamu la Swiss Church Aid, lilisema jana Alhamisi kuwa wafanyakazi wake watatu ni miongoni mwa waliouawa katika mapigano kati ya FARDC dhidi ya M23 yaliyoyokea eneo la Rutshuru nchini humo.

Hata hivyo, Shirika hilo halikuweka wazi ni wapiganaji wa upande gani katika pande za mgogoro huo waliowaua watumishi hao.

Awali, M23, itangaza kusitisha mapigano Jumatatu dhidi ya vikosi vya Serikali kwa kile ilichodai ni kuwepo kwa Janga la Kibindamu baada ya kuukamata Mji wa Goma.

Hata hivyo, walikiuka tangazo hilo Jumatano, baada ya kutangaza kuuteka Mji wa Nyabibwe, Mji ambao una utajiri wa madini unaopatikana Jimbo la Kivu Kusini.

Vyanzo nane wakiwemo raia wa eneo la Nyabibwe, Mashirika ya Umma, waasi na jumuiya za kimataifa zinazofanya shughuli zake katika eneo hilo, zilithibitisha Nyabibwe kuanguka mikononi mwa waasi hao.

Waziri wa Mawasiliano wa Serikali ya DRC, Patrick Muyaya amesema kuwa M23 ilikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano hayo kwa kuuteka Mji wa Nyabibwe huku akidokeza kuwa vikosi ya FARDC vinaendeleza mapambano ya kuukomboa kutoka mikononi mwa waasi hao.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts