Dar es Salaam. Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kwa kushirikiana na Crown Media imezindua jukwaa la tano la The Citizen Rising Woman Initiative 2025.
Jukwaa hilo linalenga kusherehekea mafanikio ya wanawake na mchango wao kwa jamii.
Uzinduzi wa jukwaa hilo umefanyika leo Ijumaa Februari 7, 2025 makao makuu ya Crown Media yaliyopo Mikocheni, Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Victor Mushi na mwanzilishi na mmiliki wa Crown Media, Ali Saleh maarufu Ali Kiba ni miongoni mwa waliohudhuria hafla ya uzinduzi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mushi alisema jukwaa hilo limenuia kukutanisha wadau wa mafanikio na maendeleo wanawake katika nyanja mbalimbali na kutoa nafasi ya kuleta watu binafsi na msahirila, taasisi, watunga sera na watekelezaji viongozi watendaji.
“Lengo ilikuwa kutambua, kusherehekea na kuwezesha wanawake wa Kitanzania katika nafasi za uongozi na katika kufanya maamuzi, hiyo ndiyo ahadi ya kuliwezesha Taifa,” amesema na kuongeza:
“Jukwaa la Rising Woman ni njia mojawapo tunayoitumia kuwezesha jamii inayotuzunguka, tukiangazia wanawake kama kundi mahususi.”
Amesema majukwaa mengine ndani ya MCL ni The Citizen, Mwananchi, Mwanaspoti, Mwananchi Scoop na Rising Woman ipo online.

“Pia kuna Mwanaclick ambayo ni mpya na ilitangaza nafasi kwa kuwekeza kwa wanawake kutoka katika nyanja ya kila kundi,” amesema.
Mushi amesema kinachowatofautisha Mwananchi ni kutumia mtindo wa simulizi katika habari.
“Hii ni upekee ambao unaangazia wanawake kwa kuangalia simulizi zao na kutumia simulizi hizo kuchechemua mijadala, fikra na kuwafanya watu wazungumze zaidi. Wadau watambue, washerehekee zaidi jitihada za kuwezesha wanawake,” amesema.

Mushi amesema Jukwaa la Rising Woman linatimiza miaka mitano mwaka huu, akieleza kazi zilizofanywa hadi sasa ni takribani simulizi 250.
Amesema kuna tuzo 45 zinazotambua mashirika na taasisi zinazowezesha wanawake kufanikiwa na kuwapa fursa za uongozi kwa ngazi za juu.
Mushi alieleza kutambua mchango wa KPMG kama mshirika wa data, akieleza umewezesha The Citizen Rising Woman kuwa jukwaa lenye hadhi na uaminifu mkubwa.
Mkurugenzi Mtendaji Crown Media, Apollo Temu amesema ushirikiano na MCL utawapeleka mbele kutokana na ukubwa wa kampuni hiyo.
“Ni heshima kubwa kwetu katika safari hii ambayo imelenga kuwawezesha wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha. Katika ulimwengu wa leo ushirikiano ni msingi wa maendeleo,” amesema na kuongeza:
“Ushirikiano wetu na Mwananchi ni ishara ya dhamira moja ya kuleta mabadiliko chanya, hususani kwa wanawake wanaotafuta nafasi za kujiendeleza, kung’ara katika jamii na sekta mbalimbali.”
Amesema kupitia Rising Woman wamelenga kutoa jukwaa la kuwawezesha wanawake kwa maarifa, fursa za mitandao na msaada wa kuendeleza ujasiriamali wao.
Temu amesema wanatambua mwanamke kwenye elimu, maarifa na mtandao mzuri wa kushirikiana ana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko si kwa maisha yake binafsi, bali kwa jamii nzima na hiyo ndiyo sababu ya kujivunia kuwa kwenye mpango huo na kufungua milango kwa wanawake wengi.

Awali, Kaimu Mhariri Mtendaji wa MCL, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa The Citizen, Mpoki Thomson alisema jukwaa la tano la Rising Woman 2025 litakuwa na utofauti mkubwa kwa kuzindua jarida la wiki linaloangazia wanawake kutoka sekta mbalimbali nchini.
“Jambo la kipekee kwa mwaka huu ni kwamba, tutakuwa na jarida la wiki la wanawake kutoka sekta tofauti ikilinganishwa na miaka ya nyuma tulikuwa na makala za kila siku kutoka kwa wanawake tofauti,” amesema.
Amesema ushiriki wa Crown Media mwaka huu utaongeza nafasi zaidi kwa wanawake kusikika na kushiriki mijadala yenye tija.
Mwakilishi wa KPMG Afrika Mashariki, Fabiola Ssebuyoya amesema kampuni hiyo inatambua mchango wa wanawake katika uchumi na nafasi zao katika sekta mbalimbali za jamii.
Amesema uwezeshaji na maendeleo ya wanawake ni msingi wa thamani wa kampuni hiyo, akieleza wanawake wanawakilisha takribani asilimia 52 ya wafanyakazi wa kampuni hiyo.
“Kampuni yetu inaendesha mipango mbalimbali, ikiwa ni pamoja na programu za uongozi na ushauri. Tumetengeneza pia mazingira wezeshi kwa wanawake wenye watoto wachanga na wajawazito, kuhakikisha wana mazingira rafiki wakati wa mpito wa kuwa wazazi,” amesema.