Dar es Salaam. Swali vichwani mwa wafuatiliaji masuala ya siasa, amani na usalama ni je, wakuu wa nchi wanaokutana kesho Jumamosi Februari 8, 2025 jijini Dar es Salaam watapata suluhisho la vita Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo?
Wakuu hao wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wanakutana kutafuta suluhisho la mgogoro huo, ambalo wadau wanatamani lipatikane la kudumu na amani itawale DRC.
Mkutano huo umetanguliwa na wa mawaziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi wa nchi za EAC SADC uliofanyika leo Februari 7, 2025.
Mkutano huo unafanyika huku vikundi vya waasi chini ya Alliance Fleuve Congo (AFC/M23) umekamata miji ya Goma, Kivu Kaskazini na Nyabibwe, Kivu Kusini, vikielekea Bukavu.
Hayo yanaendelea wakati Februari 6, M23 walipotangaza kusitisha mapigano dhidi ya vikosi vya Serikali ya DRC (FARDC) na jana waliutangaza uongozi mpya wa jimbo la Kivu Kaskazini, chini ya himaya ya makundi hayo.
Hali ikiwa hivyo nchini DRC, Rais Samia Suluhu Hassan atakuwa mwenyeji wa mkutano wa wakuu hao wan chi, utakaowakutanisha viongozi wa mataifa ya Afrika yanayoguswa na mgogoro wa DRC, wakiwamo Rais wa Rwanda, Paul Kagame, Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Felix Tsishekedi (DRC) na Yoweri Museveni wa Uganda.
Tangu kuanza kwa mgogoro kumekuwa na mvutano miongoni mwa viongozi hao, Tshisekedi akimlalamikia Kagame kuwa nchi yake inawaunga mkono M23, madai ambayo Rwanda imekuwa ikiyakanusha.
Rais Kagame pia amejikuta katika mzozo na Rais Ramaphosa, kila mmoja akimtupia lawama mwenzake kuhusu ushiriki wa vita katika eneo hilo.
Afrika Kusini ililalamikia kuuawa baadhi ya wanajeshi wake waliopelekwa DRC kulinda amani chini mpango wa Sadc, huku Rwanda ikijitenga na madai hayo ambayo yaliihusisha kupitia kinachodaiwa ni ushirika wake kwa M23.
Kukutana kwa viongozio hao ambao wako katkatio ya mzozo huo kunatamwa kama moja ya hatua ya kuitafuta amani ya kudumu.
Jumuiya ya asasi za kiraia Ukanda wa Maziwa Makuu zimeeleza matumaini yake kuwa SADC na EAC zina nafasi na ushawishi mkubwa katika kumaliza kinachoendelea DRC na hali ya kushutumiana baina ya Taifa hilo na Rwanda.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Joseph Butiku amesema wadau wa jumuiya hizo wamekutana kujadili kuhusu mgogoro huo na watawasilisha maazimio yao kwa wakuu wa nchi leo.
Butiku amesema wana matumaini kuwa mazungumzo yatajielekeza katika kurejesha amani, kwa sababu si nia ya kiongozi yeyote kutoka nchi wanachama wa SADC wala EAC kuona vita vinaendelea.
“Nilipigiwa simu na viongozi wa asasi hizi, kwa umoja wetu tukakubaliana tukutane kwanza kuunga mkono juhudi za wakuu wa nchi katika kutafuta suluhu ya mgogoro huu,” amesema.
Amesema uamuzi utakaotolewa na wakuu wa nchi wanaamini utalenga kumaliza vita.
“Sijawa na uhakika kama utaratibu utatuwezesha kuingia ndani ya mkutano, lakini hata tusipokwenda tunaruhusiwa kupeleka taarifa yetu,” amesema.
Butiku amesema SADC na EAC wanaamini zitamaliza mgogoro huo kwa sababu zina kanuni na muundo mzuri wa kusimamia amani kwa nchi zake wanachama.
Kiongozi wa Umoja wa Asasi za Kiraia nchini Kenya ambaye pia ameshiriki mkutano huo, Kennedy Walusala amesema kwa sababu DRC ni nchi mwanachama wa EAC na Taifa la Afrika, hawana budi kushinikiza amani ya watu wake.
Amesema watu wamepata shida nchini DRC hasa Mji wa Goma, hivyo wameona asasi kutoka ukanda wa maziwa makuu waungane na wakuu wa nchi kutafuta amani.
Amesema baada ya kikao cha wakuu wa nchi wanatarajia kukutana kwa tathmini ya hatua iliyofikiwa.
Akizungumzia mkutano huo, mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Dennis Konga ameieleza Mwananchi kuwa, ili kupata suluhisho la kudumu, viongozi wa EAC na SADC wanapaswa kugusa kiini cha mgogoro huo.
“Kwanza tujiulize, nani anafadhili majeshi ya nchi hizo yanayopigana DRC? Kwa kiasi kikubwa nchi hizi zinafadhiliwa na mataifa yanayoendelea na huenda hayatoi ufadhili wa kutosha kwenye majeshi yanayoisaidia DRC.
“Pili, sheria za Umoja wa Mataifa zinazuia majeshi yaliyo chini ya mpango wa kulinda raia na amani nchini DRC (Monusco) kutumia silaha za kivita, ndiyo maana majeshi hayo yanashindwa kirahisi na M23,” alisema.
Alisema ili viongozi hao wapate suluhisho, ni lazima watafute njia za kudhibiti majeshi ya waasi.
“Lazima watoke na njia za kuumaliza mgogoro huo hata kama ni za kijeshi, vinginevyo yatakuwa ni mazungumzo tu ya kujifurahisha,” alisema.
Mapema umefanyika mkutano wa mawaziri ulioongozwa na Katibu Mkuu wa EAC, Veronika Nduva na Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi.
Mawaziri wakuu walikuwa Musalia Mudavadi wa Kenya na Profesa Amon Murwira wa Zimbabwe.
Akihutubia mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda.
Amepongeza juhudi za viongozi wa EAC na SADC katika kushughulikia mgogoro wa DRC, akimshukuru Rais Samia kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kihistoria.
“Ni matumaini yangu kikao hiki kitaandaa njia bora kwa kikao cha marais kesho na hatimaye kupatikana amani ya kudumu nchini DRC,” amesema.
Nduva amesisitiza kuwa usalama wa DRC ni muhimu si kwa nchi hiyo pekee, bali kwa ustawi wa kikanda.
“Tunapaswa kusimama pamoja kuhakikisha hali hii ya mgogoro inashughulikiwa kwa umoja na mshikamano,” amesema.
Kwa upande wake, Magosi ameelezea kuhusu umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kumaliza mgogoro huo.
“Vita hii imegharimu maisha ya wengi na kuleta mateso makubwa kwa wanawake na watoto. Ni lazima wahusika wa mgogoro huu wakomeshe mapigano na kushiriki mazungumzo ya amani,” amesema.
Mkutano huo ulitarajiwa kutoa mapendekezo yatakayojadiliwa na wakuu wa nchi wa EAC na SADC kesho, lengo likiwa kuimarisha amani, usalama na mshikamano wa kikanda kwa manufaa ya wananchi wa DRC na ukanda mzima.
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limetangaza kuzifunga kwa muda barabara nne zinazoingia katikati ya jiji, ili kutoa nafasi kwa ugeni wa wakuu wa nchi watakaohudhuria mkutano huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, barabara zitakazofungwa ni Nyerere kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kwenda katikati ya Jiji.
Nyingine ni barabara ya Kivukoni na Luthuli, Sokoine kuanzia taa za Gerezani kwenda hoteli ya Johari Rotana, Hyatt Regency hadi Ikulu.
Pia, barabara ya Ohio kutokea Kivukoni kwenda Hoteli ya Serena na barabara ya Garden kutokea barabara ya uthuli kwenda Hoteli ya Southern Sun.
Jeshi hilo pia limezuia bodaboda na bajaji kuingia kwenye maeneo ya katikati ya Jiji, hasa barabara zilizotajwa kwa muda kwa sababu za kiusalama wakati wa ugeni.
Taarifa hiyo imeeleza katika kipindi chote cha mkutano, watumiaji wengine wa barabara wanashauriwa kutumia za Uhuru, Kawawa kupitia Magomeni, Kigogo kuelekea Temeke, barabara ya Morogoro na Msimbazi, Morogoro na Lumumba.
Kwa wanaotokea maeneo ya Chanika, imeshauriwa wanaweza kutumia njia mbadala ya mradi wa SGR ili kutokea barabara ya Mandela na Uhuru.
“Jeshi litajitahidi kupunguza usumbufu kwa kufanya kazi ya ziada kwenye barabara hizo kwa kuzifunga na kuzifungua haraka kadiri msafara utakavyokuwa unapita,” ilieleza taarifa hiyo.