Mwanza. Mwandishi wa Habari Mwandamizi na mtangazaji wa Kenya, Leonard Mambo Mbotela, amefariki dunia kwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua, tovuti ya Kenyans.co.ke imeripoti.
Kifo cha Mbotela (85) kimethibitishwa na mke wa mwanaye anayetambulika kwa jina la Anne Mbotela kuwa mwanahabari huyo aliyehusika kuasisi programu mbalimbali za televisheni nchini Kenya amefariki leo Ijumaa Februari 7, 2025.
Mbotela ambaye alijizolea umaarufu kwa kipindi chake cha “Je, Huu ni Uungwana?” kilichokuwa kikirushwa na Shirika la Utangazaji la Kenya (KBC), alivuta hisia za watu wengi waliokuwa wakimfuatilia.
Kipindi hicho kilianza kuruka mwaka 1966, kikijikita kuhamasisha masuala mbalimbali ikiwemo maadili kimekuwa kikirushwa kupitia Televisheni ya KBC nchini humo.
Tangu akiwa shuleni, ndoto yake (Mbotela) katika uandishi wa habari haikupimika, kutokana na ustadi wake wa kusoma magazeti kwa sauti huku akifuatiliwa na wanafunzi wenzake.
Kutokana na bidii yake kwenye taaluma hiyo, alijikuta akitimkia katika Kampuni ya magazeti ya The Standard iliyopo Nakuru nchini humo.
Mwaka 1964, alihamia Voice of Kenya (VoK), ambayo sasa inafahamika kama Kenya Broadcasting Corporation (KBC) ambako alianza kazi ya utangazaji.
Mbotela alijizolea umaarufu zaidi akiwa VoK wakati wa jaribio la mapinduzi ya Kijeshi dhidi ya Serikali nchini humo ya mwaka 1982.
Agosti Mosi, 1982, wanajeshi walioasi walimtaka kupitia studio za VoK, atangaze kuwa Utawala wa Rais Daniel Arap Moi umepinduliwa.
Hata hivyo, baada ya jaribio hilo la mapinduzi kudhibitiwa, Mbotela alitakiwa kuuhabarisha umma juu ya mafanikio ya Serikali kukomesha mapinduzi hayo.
Aliaminika kila alichokisema kutokana na sauti yake ilivyokuwa ya kuvutia kwenye masikio ya msikilizaji.
Miongoni mwa mambo ya kuvutia kwa Mbotela, aliyezaliwa Freetown, jijini Mombasa, alishuhudia uongozi wa awamu zote tano za marais wa taifa hilo kuanzia kwa Jomo Kenyatta hadi Willian Ruto.
Pia, amewahi kufanya kazi na kitengo cha Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Enzi za uhai wake, Mbotela alitambuliwa na kutunukiwa tuzo mbalimbali kutokana na mchango wake kwenye Taaluma ya Uandishi wa Habari na Utangazaji.
Mwaka 1987 alitunukiwa kuwa mwandishi mwenye hadhi ya juu nchini humo (Head of State Commendation, HSC).
Pia, alitajwa kuwa mwandishi kinara wa Kenya mwaka 1992. Ilipofika mwaka 2009, Serikali ya Kenya ilimtangaza kuwa shujaa wa taifa hilo kutokana na mchango wake kwenye sekta ya habari nchini humo.
Mbotela alizindua Kitabu chenye jina, “Je, Huu ni Ungwana?” ambacho kinaelezea historia ya maisha yake na mchango wake kwenye vyombo vya habari mwaka 2024.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa Msaada wa Mashirika.