Mwanza. Mwili wa Mtukufu Aga Khan IV aliyekuwa Imamu wa 49 wa Madhehebu ya Shia Ismailia na mwanzilishi wa Mtandao wa
Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), utazikwa Mjini Aswan nchini Misri Jumapili Februari 9, 2025.
Mtukufu Aga Khan (88) alifariki dunia Jumanne Februari 4, 2025, jijiji Lisbon, Ureno akiwa amezungukwa na familia yake.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Imam wa Shia Ismailia, baada ya ibada maalumu ya mazishi itakayofanyika Jumamosi, jijini Lisbon Ureno, mwili wa kiongozi huyo utasafirishwa kwenda Misri kwa maziko.
Ibada ya mazishi ya Mtukufu Aga Khan IV, jijini Lisbon inatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya watu wakiwemo viongozi wa umma na Serikali nchini humo na wageni kutoka nje ya taifa hilo.
Baada ya kifo Mtukufu Aga Khan IV, mwanaye Rahim Al-Hussaini alitangazwa Jumatano Februari 5, 2025 kurithi mikoba na kuwa Imamu wa 50 wa madhehebu hayo, kwa mujibu wa wasia wa baba yake.
Enzi za uhai wake, Mtukufu Aga Khan IV alifahamika kutokana na mchango wake kwenye shughuli zinazochangia kuimarisha ustawi wa maisha ya binadamu katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.
Kiongozi huyo alizaliwa Desemba
13, 1936, Geneva, Switzerland katika familia ya Aly Khan na Joan Yarde-Buller, ambaye ni mzaliwa wa Uingereza. Aliishi maisha yake ya utoto jijini Nairobi, Kenya.
Kutokana na kuishi katika ukanda wa Afrika Mashariki, mchango wake ulionekana kwa kuanzisha kwa Taasisi za Aga Khan zilizoleta tija na manufaa mbalimbali kwa umma katika ukanda huo.
Kutokana na shughuli za kielimu, Aga Khan alijikuta nchini Switzerland, ambako alipata elimu ya dini katika Shule ya Le Rosey, kisha kujiunga na Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani.
Wakati baba yake anafariki dunia, yeye alikuwa masomoni akibobea katika Imani ya Kiislamu katika chuo hicho.
Huku akiwa mrithi wa 49 wa nafasi ya Imamu wa madhehebu ya Ismailia, Aga Khan IV katika umri mdogo alikatisha ndoto yake ya kuwa mchezaji wa soka na kuendelea na elimu katika ngazi ya Uzamivu (PhD), chuoni Harvard.
Alilazimika kukatisha ndoto hizo baada ya kuteuliwa kurithi mikoba ya uongozi huo wa kiroho wa mamilioni ya waumini wa madhehebu hayo, ambayo kwa wakati huo yalikuwa yamesambaa maeneo mengi uliwenguni, hususan India, Kenya, Pakistan, Bangladesh, Misri, Canada na Jumuiya ya Kisovieti (Urusi).
Akiwa kiongozi wa kiroho, alitwishwa jukumu la kuwa Imamu wa 49 wa madhehebu ya Shia Ismailia, wadhifa ambao aliutumikia kwa dhati.
Hata hivyo, wajibu wake haukuishia kuwa kiongozi wa kidini, bali alikuwa mwanzilishi wa shughuli mbalimbali zilizoleta mabadiliko ulimwenguni, hususan kwenye sekta ya afya, utamaduni, elimu, habari na maendeleo ya jamii katika kanda zote duniani.
Maeneo mengine aliyoyagusa moja kwa moja ni pamoja na sekta ya uwezeshaji kiuchumi ambako alibua mikakati ya kuongeza ustawi katika jamii.
Mtukufu Aga Khan ameacha nembo isiyofutika maeneo mbalimbali duniani hususan nchini Kenya na Tanzania ambako alianzisha taasisi mbalimbali zilizoleta mchango mkubwa katika maisha ya raia wa nchi hizo.
Miongoni mwa taasisi hizo ni pamoja na Shule za Aga Khan, Chuo Kikuu cha Aga Khan, vyote vilianzishwa ikiwa ni ishara ya kujitoa kwake kuikomboa jamii ya eneo husika.
Pia, alianzisha Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa Aga Khan (AKFED), mfuko huo ulichochea maendeleo endelevu huku ukitumia kauli yake: “AKFED hailengi kutengeneza faida ila ni mpango wa maendeleo ya kesho.”
Pia, ni mwanzilishi wa Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN)
ambao umeleta tija maeneo mbalimbali hususan katika sekta ya afya, elimu na utamaduni hususan uwezeshaji kiuchumi maeneo ya vijijini nchini Tanzania na Kenya.
Uwepo wa Aga Khan nchini Tanzania unaonekana kupitia uanzishwaji wa kampuni mbalimbali ikiwemo ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Hospitali za Aga Khan na miradi mbalimbali katika sekta ya afya na elimu.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa Msaada wa Mashirika.