Sababu mazoezi kuwa muhimu kwa mjamzito

Mmoja wa wakimbiaji wa Marathon aliuliza kama ni salama kushiriki Marathon akiwa katika ujauzito muhula wa kwanza.

Kwa kifupi, mazoezi mepesi hayana madhara kwa ujauzito katika hatua za awali yaani katika chini ya miezi mitatu au muhula wa kwanza.

Kuna ushahidi wa kitafiti kuwa mjamzito anayefanya mazoezi, ana uwezekano mdogo kupata matatizo ya uzazi wakati wa kujifungua kwa njia ya kawaida

Mazoezi mepesi ni muhimu kwa mjamzito ambaye hana tatizo lolote la kiafya, ikiwamo yale yanayotishia mimba kutoka au kuharibika.

Muhula wa kwanza, huambatana na mabadiliko mengi ya kimwili kipindi cha ujauzito na huwa ni kipindi cha mjamzito kutojisikia vizuri, ndiyo maana haishauriwi kufanya mazoezi magumu kipindi hiki zaidi mazoezi ya kunyoosha viungo vya mwili na kutembea.

Mazoezi haya yanashauriwa kufanyika katika muhula wa pili na wa tatu wa ujauzito na hayatakiwi kuwa magumu ya kuchosha bali mepesi na rahisi kufanyika.

Mazoezi mepesi ni kama vile kutembea, kuogelea, kuruka kamba, kucheza mziki, mazoezi ya viungo, kuendesha baiskeli na kufanya shughuli za ndani za kila siku kama vile usafi na kazi za bustani.

Mazoezi haya yana faida kubwa kwa afya ya moyo na mzunguko wa damu, mfumo wa hewa (mapafu), uondoaji taka mwili, misuli na viungo vya mwili.

Husaidia kuongeza kasi ya mapigo ya moyo na huku akivuta hewa kwa ufanisi zaidi, hivyo kuipa lishe ya kutosha misuli ya mwili.

Mazoezi humsaidia mjamzito kuepukana na matatizo makubwa ya kiafya, ikiwamo shinikizo la juu la damu na kisukari wakati wa ujauzito.

Humsaidia kudhibiti uzito wa mwili, kuepukana na matatizo kama vile maumivu ya mgongo na kiuno, kukosa choo, hamu ya kula na kunywa maji na kumsaidia uponaji wa haraka baada ya kujifungua.

Huifanya misuli na viungo kuwa na stamina na wepesi hivyo kumsaidia kujifungua kwa njia ya kawaida kirahisi, akipata nafuu katika uchungu huku akiwa na nguvu zaidi kumsukuma mtoto.

Kufanya mazoezi mara kwa mara huifanya misuli kuwa imara na myepesi hasa ile ya kitako cha kiuno na mgongoni ambayo ni muhimu wakati wa kujifungua.

Kupitia mazoezi viungo hivi huweza kuwa na wepesi wa kutanuka pasipo kupata majeraha, kuchochea kuzaa kwa njia ya kawaida na kumwondolea msongo wa mawazo, kwani mazoezi huleta hisia chanya.

Sababu ikielezwa kuwa ni kuimarika kwa mzunguko wa damu na huku mfumo wake wa hewa ukiingiza hewa yenye oksijeni nyingi, hivyo pia kumnufaisha mtoto anayepiga hatua za ukuaji.

Wakati wa kufanya mazoezi hayo avae mavazi rafiki kwa mazoezi na raba laini za mazoezi, anywe maji ya kutosha kiasi cha glasi nane hadi 10 kwa siku, afanye mazoezi maeneo salama kwake.

Vizuri afanye katika maeneo ya wazi au ndani ya ua wa nyumba kwenye hewa ya kutosha na nguo anazovaa ziwe zile zisizohifadhi joto zenye kunyonya jasho kirahisi.

Joto kali si rafiki kwa ujauzito hivyo vizuri kuwa mwangalifu kwa kufanya mazoezi jua likiwa limepungua, nyakati za jioni au asubuhi.

Related Posts