Serikali yatoa mwongozo unyonyeshaji wanafunzi waliojifungua

Dodoma. Serikali imesema mwongozo wa wanafunzi wanaorejea shuleni baada ya kujifungua hawaruhusiwi kwenda shuleni na watoto wao na badala yake, unawataka wazazi kusaini makubaliano na uongozi wa shule ya kuwajibika kuwalea wanafunzi na watoto wanaorudi shuleni.

Novemba 24, 2021 aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alitangaza kuruhusiwa kwa wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni kwa mfumo rasmi baada ya kujifungua.

Uamuzi huo ulitokana na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, John Magufuli, kupiga marufuku wanaopata mimba shuleni kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari Juni, 2017.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ameyasema hayo leo Februari 7, 2025 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Najma Giga.

Katika swali la msingi, Najma amehoji  Serikali imejipangaje kuhakikisha watoto wachanga wa wasichana wanaoendelea na masomo wananyonya maziwa ya mama zao kwa wakati.

Akijibu swali hilo,  Kipanga amesema kulingana na mwongozo wa wanafunzi wanaorejea shuleni baada ya kujifungua hawaruhusiwi kwenda shuleni na watoto wao na badala yake, mwongozo unawataka wazazi kusaini makubaliano na uongozi wa shule ya kuwajibika kuwalea wanafunzi na watoto wanaorudi shuleni.

Hata hivyo, amesema kupitia elimu nje ya Mfumo Rasmi, wanafunzi wenye watoto wachanga wanaruhusiwa kunyonyesha kwenye kituo. 

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki katika vituo vya elimu nje ya mfumo rasmi,  kwa kujenga chumba maalumu cha watoto katika vituo vyote vipya vinavyojengwa kupitia mradi wa uboreshaji elimu ya sekondari kwa njia mbadala, ambapo katika vituo hivyo, kuna mlezi anayekaa na watoto.

Amesema mwanafunzi mwenye mtoto anapata nafasi ya kunyonyesha mtoto wake kwa wakati, pindi inapohitajika kufanya hivyo.

Katika swali la msingi, Najma amesema Haioni umuhimu wa kuwapa muda wa miaka miwili watoto hawa ambao wamejifungua wakiwa shuleni ili watoto hawa waweze kupata haki ya kimsingi ya kupata maziwa ya mama.

Haioni umuhimu wa kurasimisha rasmi vituo hivi kwa sababu hili jambo limeshakuwa rasmi nchini kwetu?,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Kipanga amesema wamepokea ushauri wake na watakwenda kufanyia tathimini, waone namna anavyoweza kutekeleza jambo hilo.

Serikali inaendelea kuangalia namna bora ya kuhuisha ama kuimarisha vituo vile vya kulelea watoto ndani ya shule ama karibu na shule ili kuhakikisha kuwa watoto hawa wanaozaliwa wanaweza kupata malezi bora na kuangalia afya zao pindi wanapopata maziwa ya mama,” amesema.

Related Posts