Taasisi zitakazokidhi vigezo kupewa uhuru wa kujiendesha

Na Mwandishi wa OMH

Dar es Salaam. Kama sehemu ya mageuzi yanayolenga kuongeza ufanisi wa taasisi za umma zenye mrengo wa kibiashara na za kimkakati, Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina mpango wa kuzipa taasisi, lakini zenye sifa, uhuru wa kujiendesha.

Jukumu hili la kuangalia namna bora ya kutoa uhuru huo limekabidhiwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, chini ya Bw. Nehemiah Mchechu, ambaye ni Msajili wa Hazina.

Mpango huu unafuatiwa kuwepo kwa changamoto ya taasisi hizo kushindwa kujiendesha kwa ufanisi.

Tatizo hilo linachagizwa na taasisi zote kuwa na mfumo unaofanana katika usimamizi wa masuala ya rasilimaliwatu, ununuzi na mamlaka za Bodi za Wakurugenzi katika kusimamia taasisi zao.

Hali hiyo inasababisha baadhi ya taasisi kutofikia malengo ya uanzishwaji wake kutokana na kuwajibika kwa mamlaka zaidi ya moja, na uwepo wa taratibu za kisheria ambazo haziendani na malengo na mazingira halisi ya baadhi ya taasisi.

Ni katika muktadha huo, serikali imeona ni vema kutatua changamoto hii kwa kutoa uhuru wa kujiendesha kwenye baadhi ya maeneo kwa taasisi za kimkakati na zile zinazojiendesha kwa mrengo wa kibiashara.

Hivi karibuni Bw. Mchechu alisema serikali inafuatilia kwa ukaribu taasisi za umma kabla ya kuzipa uhuru zaidi wa kiutendaji ambao utatoa nafasi ya ubunifu na hivyo kupelekea ufanisi zaidi.

“Ili kuongeza tija, na kuhakikisha kuwa uhuru huo unatumika kama inavyokusudiwa, kutakuwa na vigezo vitakavyotumika katika kuzitambua taasisi na kupima matokeo ya utendaji wao,” alisema Bw. Mchechu.

Miongoni mwa vigezo hivyo ni maslahi na malengo ya kimkakati ya nchi, uwezo wa kujiendesha kwa mapato ya ndani ya taasisi bila kutegemea ruzuku ya serikali, na uchangiaji wa mapato yasiyo ya kodi katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali kwa kiwango kilichowekwa na Msajili wa Hazina.

Vigezo vingine ni uwezo wa kujiendesha kibiashara na kukabiliana na ushindani wa ndani na nje ya nchi, unyeti wa huduma zinazotolewa na kuchangia katika kuimarisha usalama na ustawi wa nchi, utoaji wa huduma ambazo hazina mtoa huduma mbadala, na utoaji wa huduma ambazo zinagusa sekta nyingi za uchumi.

Sanjari na vigezo hivyo, ni mchango wa taasisi kwenye masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama na uchangiaji katika pato la Taifa na mchango wa ajira kwa wananchi.

Msajili wa Hazina alisema: “Tunataka taasisi za umma ambazo tunazisimamia ziweze kufanya kazi kwa ufanisi ili kupunguza utegemezi wao kwa serikali kuu na kuongeza michango yao katika mfuko mkuu wa serikali.”

Lakini Bw. Mchechu alitoa angalizo kuwa uhuru zaidi wa kiutenaji, hauji bila usimamizi.

“Serikali haitaishia kutoa uhuru wa kiutendaji—tutaendelea kutathmini utendaji kwa karibu ili kuhakikisha kuwa taasisi hizi zinabaki katika njia sahihi na zinafuata malengo ya kitaifa,” alisisitiza.

Hili ni jambo muhimu kwa sababu linamaanisha kuwa uhuru na uwajibikaji lazima viwe katika uwiano mzuri.

“Taasisi zinazofanya vizuri tutazipatia uhuru zaidi, huku zile zinazoonesha utendaji duni zikipatiwa msaada wa kuboresha,” alitimisha Bw. Mchechu.

Related Posts