Dar es Salaam. Mwili wa binadamu una viungo vingi vikiwemo vya ndani na nje.
Kila kiungo kinahitaji kutunzwa ili kifanye kazi yake kwa ufasaha, baadhi utunzaji wake hutokana na aina ya maisha unayoishi kuanzia asubuhi mpaka wakati wa kulala.
Baadhi ya viungo ambavyo ni muhimu kwa afya zetu ni pamoja na figo. Kazi yake kubwa ni kutoa sumu, maji ya ziada mwilini, kudhibiti shinikizo la damu na kusaidia katika michakato mingine ndani ya mwili.
Hata hivyo, mara nyingi tunasahau kutoa kipaumbele kwa figo zetu katika maisha ya kila siku, kutokana na mambo tunayoyafanya asubuhi ambayo huleta athari kwa wakati ujao.
Utafiti wa American Journal of Kidney Diseases wa mwaka 2016, ulionyesha umuhimu wa kunywa maji mara tu unapoamka,.
Watafiti waligundua kuwa unywaji wa glasi moja ya maji kunazuia usagaji wa sumu mwilini na kuipunguzia mzigo figo.
Daktari wa binadamu, Lilian Mwakyosi anasema unywaji wa maji hasa asubuhi unapoamka ni muhimu kwa kuilinda figo.
“Unywaji maji kwa wingi hasa asubuhi ni tiba kwa namna nyingi mojawapo kuna namna inaboresha mmeng’enyo wa chakula. Si asubuhi pekee tunashauri kila dakika 30 unywe maji, unapokula chakula unapumzika dakika 30 unakunywa tena maji, upe mwili nguvu na huboresha ufanisi wa mwili,” anasema Dk Mwakyosi.
Kauli yake inaungwa mkono na Daktari bingwa mshauri wa magonjwa ya figo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) iliyopo Dodoma, Kessy Shija anayesema; “Ukinywa maji mengi utasaidia kuzuia kupata mawe kwenye figo.”
Kula kifungua kinywa kilichojaa virutubisho asubuhi ni bora zaidi kuliko vitu vyenye sukari nyingi.
Utafiti mwingine kutoka Journal of Nephrology wa mwaka 2018, ulionyesha umuhimu wa kula kifungua kinywa kilicho na virutubisho muhimu, kwa afya ya figo ambavyo ni matunda, mboga na vyakula vyenye potasiam.
Utafiti huo ulionyesha kuwa kifungua kinywa chenye madini hayo ambayo hupatikana kwenye ndizi, parachichi na mboga za majani kunalinda figo kutokana na madini hayo kusaidia kudhibiti shinikizo la damu, ambalo mara nyingi husababisha magonjwa ya figo.
Vyakula vyenye nyuzi nyingi na molekuli zinazolinda mwili, husaidia pia kupunguza uharibifu wa seli katika figo na kuongeza ufanisi wa kazi za figo.
Utafiti uliofanywa na International Journal of Environmental Research and Public Health wa mwaka 2020, ulizungumzia umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili kama vile matembezi na mazoezi mengine, husaidia kupunguza hatari ya ugonjwa wa figo kwa kuboresha mzunguko wa damu na kudhibiti uzito.
Walithibitisha kuwa mazoezi huboresha kiwango cha sukari kwenye damu jambo ambalo huboresha figo na madhara ya sukari.
”Msukumo wa damu na namna mwili unavyofanya kazi na mazoezi, inasaidia kupunguza figo kujeruhiwa, hivyo ni muhimu kujitahidi kubaki na uzito unaotakiwa kiafya,” anasema Mwakyosi.
Ulaji wa vyakula vya asili
Aidha walithibitisha kuwa vyakula vya asili kama vile mboga za majani, matunda na nafaka kamili, vinasaidia kupunguza viwango vya sodiamu mwilini ambayo inaweza kuongeza shinikizo la damu na kuathiri figo.
Utafiti ulionyesha kuwa vyakula vyenye chumvi nyingi kama vile vyakula vilivyopikwa viwandani vinaongeza kiwango cha sodiamu na hatimaye kuharibu figo.
Unapoamka asubuhi epuka vinywaji vya kafeini kama kahawa. Kinywaji hiki mara tu unapoamka kinatajwa kuongeza shinikizo la damu na kuharibu kazi ya figo, hivyo unashauriwa kutumia chai asili.
Epuka msongo. Hali hii huongeza shinikizo la damu na kuathiri afya ya figo. Kwa mujibu wa maandiko mbalimbali na tafiti, unapaswa kufanya mazoezi ya kupumua ili kupunguza msongo wa mawazo na kuboresha afya ya akili ili kuongeza ufanisi wa figo.
Dk Kessy anasema ili kuepuka kufeli kwa figo ni muhimu kuzingatia mtindo bora wa maisha.
“Ukiugua utaenda kwa mtaalamu utachunguzwa na kutibiwa, usiende kununua dawa pharmacy. Tunashauriwa tule chakula ambacho ni kamili chenye makundi yote ambayo ni sahihi, usile wanga kupita kiasi au chakula chenye mafuta, unatakiwa ule chakula kizuri.”
“Wengi wanakula sana hawafanyi kazi na mazoezi kwa maana utatumia kile chakula ulichokula utakua vizuri, chakula cha wastani kitatumika mwilini, kile chakula kilichozidi kuhifadhiwa kwake ni kwa mafuta, hivyo utanenepa.
“Unapoushughulisha mwili inasaidia kupambana, tutumie chumvi kiasi kwa sababu kuna uhusiano mkubwa sana wa chumvi nyingi na shinikizo la juu la damu,’’ anasema.
Akitoa ushuhuda, mgonjwa wa figo Ruben Mchakuru (63) anasema kutokana na ugonjwa huo, amekuwa akifanya usafishaji wa damu kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa muda wa miaka mitano sasa.
“Naomba niwashauri Watanzania watunze figo zao.” Anasema ugonjwa huo unatokana na changamoto za vyakula, utumiaji holela wa dawa na utumiaji wa vileo ndiyo sababu kuu ya ugonjwa wa figo,” anaeleza.