Ujenzi Bwawa la Kidunda wafikia asilimia 27

Morogoro. Wakati changamoto ya ukosefu wa maji kwenye baadhi ya maeneo katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Pwani ikiendelea kuleta maumivu kwa wananchi, Serikali inaendelea na mradi wa ujenzi wa bwawa la kuhifadhi maji yatakayotumika kiangazi.

Bwawa la Kidunda linajengwa mkoani Morogoro mahususi kwa ajili ya kutunza maji kisha kusambazwa pale yatakapopungua katika mitambo ya uzalishaji ya Ruvu Juu na Chini.

Mpango wa ujenzi wa bwawa hilo umekuwapo tangu mwaka 1961 na sasa utekelezaji wake umefikia zaidi ya asilimia 27.

Moja ya sababu ya mgawo wa maji kama ambao imewahi kushuhudiwa kwa muda mrefu mwaka 2021 na 2022 inatajwa kuwa upungufu wa maji katika Mto Ruvu ambao ndiyo chanzo kikuu cha yanayozalishwa kwenye mitambo hiyo.

Serikali kupitia Wizara ya Maji inajenga bwawa hilo kwa fedha za ndani ikieleza inalenga kumaliza mgawo. Mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa).

Mbali ya Dar es Salaam kukamilika kwa bwawa hilo Juni 2026 kutawezesha kupatikana huduma ya uhakika mkoani Pwani. Ujenzi ulianza Juni 18, 2023.

Akizungumza wakati wa ziara ya siku mbili kwa waandishi wa habari iliyoanza jana Alhamisi Februari 6, 2025, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkama Bwire amesema ujenzi wa mradi huo umefika asilimia takribani 27.

Mpango wa mradi huo ambao umekuwa tangu mwaka 1961 unagharimu Sh336 bilioni zinazotokana na mapato ya ndani kwa asilimia 100. Utekelezaji wake ni wa miaka mitatu.

“Bwawa hili liko katika mkondo wa Mto Ruvu ambao ni chanzo kikuu cha maji katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam ambao kwa zaidi ya asilimia 87 maji yanayozalishwa eneo la huduma yanategemea mto huu.

“Kutokana na changamoto inayojitokeza mara kwa mara ya kupungua kina cha Mto Ruvu kutokana na hali ya hewa imekuwa ikiathiri upatikanaji huduma ya maji, hivyo bwawa hili ni mkombozi,” amesema.

Bwire amesema katika kutatua changamoto na kuhakikisha muda wote kunakuwa na maji ya kutosha katika Mto Ruvu ili kusukuma yaende Dar es Salaam na Pwani, Serikali iliamua kujenga bwawa hilo.

“Makusudi makubwa ya ujenzi wa bwawa hili lenye uwezo wa kutunza lita bilioni 190 za maji ni kuhakikisha hata katika kipindi cha changamoto ya ukame Jiji la Dar es Salaam na Pwani maji yataendelea kupatikana,” amesema.

Akizungumzia sababu ya ukosefu wa maji katika baadhi ya maeneo ya Pwani kama ukanda wa Kibaha na Mlandizi, amesema unatokana na maendeleo ya kasi ya ujenzi wa viwanda.

Amesema Ruvu Juu zinazalishwa lita milioni 196, huku kukiwa na watu wengi zaidi, wakati Ruvu Chini zinazalishwa lita milioni 270 kwa siku lakini kuna maendeleo ya viwanda, hivyo kuwa na ongezeko la matumizi ya maji kuliko uwezo wa mtambo kuzalisha.

Amesema wakati ujenzi wa bwawa ukiendelea, suluhisho la upatikanaji maji kwa sasa linahusisha ufungaji wa pampu mpya.

Licha ya upatikanaji wa maji, amesema Bwawa la Kidunda litazuia mafuriko kutokana na maji kuhifadhiwa.

Amesema maji pia yatatumika katika umwagiliaji kwenye kilimo, uvuaji   samaki, ajira na kuzalisha megawati 20 za umeme zitakazoingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Pia, kutajengwa barabara ya urefu wa kilomita 75 za kiwango cha changarawekutoka Ngerengere hadi eneo ka mradi.

Janeth Kisoma kutoka Bodi ya Maji Bonde la Wami Ruvu, amesema mradi huo pia utasaidia Mkoa wa Morogoro.

“Hadi sasa tumeshatambua vyanzo mbalimbali vya maji vilivyopo kwa kuweka mipaka ili wananchi au mifugo wasiingie sambamba na utoaji elimu katika kutunza vyanzo vya maji,” amesema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema kwa muda mrefu vyombo vya habari vimekuwa vikiandika ukosefu wa maji jijini Dar es Salaam, hivyo ujenzi wa bwawa hilo unaenda kuleta historia mpya ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu viwandani na nyumbani.

Zaidi ya bwawa hilo, Dawasa imesema mradi wa maji Bangulo unaogharimu Sh36.8 bilioni utahudumia wakazi zaidi ya 450,000, ukijumuisha ujenzi wa tangi kubwa la kuhifadhi maji lita milioni tisa na ulazaji wa mtandao wa bomba wenye urefu wa kilomita 108.

Mradi huo utawezesha upatikanaji huduma Kinyerezi, Ukonga, Kitunda, Kibamba na Mwanagati, maeneo ambayo kwa sasa yanakabiliwa na changamoto ya majisafi.

Katika maeneo hayo wananchi wanalazimika kununua maji kwa gharama kubwa, baadhi hununua hadi Sh1,000 kwa dumu la ujazo wa lita 20, huku yakipatikana umbali mrefu.

Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 inaelekeza upatikanaji wa majisafi na salama uwe ndani ya mita 400 kutoka kwenye makazi ya wananchi.

Kwa mujibu wa Dawasa, ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 99 ya utekelezaji.

Mradi huo unaelezwa utachochea shughuli za maendeleo na kuleta ahueni ya gharama za maisha kwa wananchi.

Mradi huo wenye thamani ya Sh36 bilioni unatekelezwa na Dawasa ukilenga kusambaza huduma eneo la Dar es Salaam ya Kusini.

Bwawa la Kidunda linatarajiwa kuhudumia mitambo ya Ruvu Juu na Chini, maeneo yakiwamo Boko, Tegeta, Kunduchi, Salasala, Mbezi Beach, Ununio, Wazo, Bagamoyo mjini, Mapinga, Mikocheni, Kawe, Mbezi Juu, Goba, Kijitonyama na Mabwepande, Mbweni.

Baadhi ya maeneo yanayolishwa na Ruvu Juu ni Tabata, Kulungule, Kibangu, Korogwe, Mwananchi. Tazara, Tabata Matumbi, Bonyokwa, Malamba Mawili, Makongo Kibamba hadi Saranga.

Kero ya ukosefu wa maji imekuwa ikijirudia, huku Wizara ya Maji chini ya Waziri Jumaa Aweso ikifanya jitihada za kuitatua.

Oktoba 28, 2024 Aweso alitembelea mtambo wa kuzalisha na kusambaza maji ya Ruvu Juu na Ruvu Chini mkoani Pwani na kutoa maagizo kwa Dawasa kuhakikisha inapita kila eneo kuona hali ya upatikanaji wa maji.

“Dawasa nachowaambia wakazi wa Dar es Salaam na Pwani hawana mbadala wa maji yanapokosekana na hawana mbadala wa kutegemea wakikosa lazima usikie kelele,” alisema.

Related Posts