Unguja. Wasafirishaji wa mifugo ya ng’ombe na mbuzi kisiwani hapa wameeleza changamoto zinazowakumba na kushindwa kusafirisha mifugo yao ikiwemo vibali na wataalamu wa kupima afya za mifugo hiyo.
Wasafirishaji hao wametoa changamoto hizo leo Februari 7, 2025 katika ziara iliyofanywa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kaskazini Unguja ya kukagua utaratibu wa uingizwaji wa mifugo wamesema kuwa hawana vibali vya kusafirishia ng’ombe na mbuzi.
Miongoni mwa wasafirishaji hao, Dhamir Mshenga amesema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa vibali vinavyoonesha idadi ya mifugo waliyoinunua ili kuwa uthibitisho wanapofika sehemu za doria baharini.
Amesema kawaida wanapofika katika Mkoa wa Tanga wanakata vibali kwa ajili ya kufanyia shughuli zao za manunuzi kwa wafugaji ila wanapomaliza kufanya shughuli hizo vinachukuliwa na kubaki bila vielelezo vya usafirishaji wa mifugo.
“Wakati wa kusafirisha mifugo yetu hasa tunapokutana na walinzi wa doria baharini inatuwia vigumu kuwaelesha hadi kufikia hatua ya kuelewana kwasababu hatuna kielelezo chochote kinachothibisha kuwa kweli tumenunua mifugo hiyo,” amesema Mshenga
Changamoto nyingine, amesema wanaporudi kununua mifugo katika mikoa mingine Tanzania Bara, hakuna daktari wa kupima afya zao wala mifugo, jambo ambalo linachangia uingiaji wa maradhi kiholela.
“Tunatembea mikoa mingi kutafuta ng’ombe na mbuzi lakini tunaporudi kununua mifugo hiyo hakuna daktari aliyewekwa kwa ajili ya kuangalia afya zetu, hali hiyo inachagia kuingia kwa maradhi kiholela kisiwani hapa, serikali inapaswa kuzingatia hili,” amesema Mshenga.
Msafirishaji mwingine, Suleiman Abdalla amesema kuna haja kwa serikali kuyafanyia kazi hayo kwasababu ndimo wanapojipatia fedha za kuendeshea familia zao.
Hata hivyo, Suleiman ameiomba Serikali kuwaboreshea huduma mbalimbali ikiwemo kujengewa bandari ya Muwanda kwa ajili ya kushushia mifugo yao.
Pia, amesema ukosefu wa boti aina ya faiba wanapozama au kupotea inakuwa ngumu kutambulika walipo kutokana na usafiri wa wanaotumia wa jahazi kwani hazina vifaa vinavyoonyesha maeneo walipo na upepo katika bandari hiyo ni mkali.
Vilevile, amewataka wafanyabiashara wenzake kuepuka kupitisha biashara kwa njia za magendo kwani kufanya hivyo ni kuikosesha serikali mapato na kuhatarishia biashara zao.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya hiyo, Maryam Said Khamis amewaahidi wafanyabiashara hao kuzitafutia ufumbuzi changamoto na kuwataka kuacha kuvusha mizigo isiyostahiki kushushwa katika bandari hiyo.
“Lengo kuu la bandari hii ni kushusha mifugo pekee na sio mizigo mengine, changamoto ambazo mmeziwasilisha hapa nitazifanyia kazi,” amesema Maryam.
Ofisa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) mkoa huo, Simai Nyange Simai amewataka manahodha kuacha tabia ya kusafirisha abiria kupitia majahazi kwani Serikali haijatoa ruhusa kwa vyombo hivyo kusafirisha abiria na jambo jilo ni hatari kwa jamii.