Wasira awaonya wavuvi Ziwa Victoria

Rorya. Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amewataka wavuvi wa Ziwa Victoria kuchukua tahadhari kwa kutofika kwenye mipaka ya nchi jirani ili kuepusha mitafaruku na kuporwa zana zao za uvuvi.

Wasira ametoa tahadhari hiyo leo Ijumaa Februari 7, 2025 wilayani Rorya baada ya kupata taarifa juu ya uwepo wa matukio 12 ya wavuvi kuporwa na kunyang’anywa zana zao na uvuvi iliyotolewa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Shirati, Musa Chagonje.

Ziwa Victoria linamilikiwa na nchi tatu ambazo ni Tanzania inayolimiliki kwa asilimia 51 ikifuatiwa na Uganda inayomiliki asilimia 43 huku Kenya ikiwa na asilimia sita ya ziwa lote.

Wasira amesema changamoto hiyo ya uvamizi pia inatokana na kutokuwepo kwa uaminifu baina ya wavuvi wenyewe ambao wamekuwa wakigeukana wakati wa utekelezaji wa shughuli zao.

“Acheni kuingia kwenye maeneo mengine kama unaona umekaribia kwenye Taifa jingine jitahidini misiingie huko mtasababisha mitafaruku isiyokuwa na maana yoyote, nchi yetu ina uhusiano mzuri na mataifa mengine,” amesema.

Katika hatua nyingine, Wasira amesema ataiomba Serikali ihakikishe inaharakisha ujenzi wa barabara za Mika – Kirongwe, Tarime – Serengeti pamoja na ya Musoma – Busekela kutokana barabara hizo kuwa na umuhimu mkubwa kwa uchumi wa Mkoa wa Mara.

Amesema Mkoa wa Mara una barabara kuu tatu ambazo zipo katika ilani ya CCM na zinahitaji bajeti kubwa, hivyo atazieleza mamlaka ili ziongeze bajeti, zikamilike.

Awali, Mbunge wa Rorya, Jafari Chege, licha ya kuishukuru Serikali kwa kutekeleza miradi ikiwemo ya afya na elimu, amemuomba Wasira kuangalia namna ya Tarura kuongezewa nguvu ya fedha ili kuwasaidia kutatua changamoto za barabara kwenye maeneo hususani yanayoharibika.

Hata hivyo, Wasira amemtaka kuwasiliana na viongozi wenzake ili kuhakikisha barabara hizo zinapitika wakati wote.

Mbunge huyo amesema mbali na miradi hiyo, pia umekuwepo na ujenzi wa madaraja ambayo yamekuwa msaada mkubwa kwa wananchi kutoka kijiji kimoja hadi kingine.

Amemuomba kusukuma utekelezaji wa mradi wa maji katika miji 28 pamoja na mradi wa maji katika Kata ya Kitembe na Roche unaogharimu Sh400 milioni ili wananchi waondokane na changamoto ya huduma hiyo.

Related Posts