Na: Mwandishi Malaalumu – Dar es Salaam
Wataalamu 50 wanaotoa huduma za matibabu ya dharura, na matibabu kwa wagonjwa mahututi kutoka hospitali mbalimbali nchini wameshiriki katika mafunzo ya kuongeza ujuzi katika fani ya huduma za dharura na mahututi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Tatizo Waane alisema mafunzo hayo ya siku mbili yameandaliwa na Kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA) na kufanyika JKCI.
Dkt. Waane alisema katika mafunzo hayo pia wamepata wataalamu wanaotoa huduma za dharura kutoka nchi za New Zealand, Australia ambao wataongeza ujuzi zaidi kwa wataalamu wa hapa nchini.
“Serikali yetu imejenga vyumba vya wagonjwa mahututi na kutoa vifaa tiba kwaajili ya matibabu hayo katika hospitali mbalimbali nchini, hivyo kupitia mafunzo haya tutaweza kuwajengea uwezo wataalamu wa afya na kuongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa wanaotutegemea”, alisema Dkt. Waane
Kwa upande wake Daktari bingwa wa mifupa ambaye pia ni Mkufunzi kutoka Kituo cha mafunzo cha tiba na huduma za dharura (Emergency Medicine Services Academy – EMSA) Sylvester Faya alisema mwitikio wa wataalamu kushiriki katika mafunzo hayo hapo awali ulikuwa mdogo tofauti na ambavyo sasa watu wanashiriki kwa wingi.
Dkt. Faya alisema kupitia mafunzo hayo wanategemea huduma za matibabu ya dharura na kwa wagonjwa mahututi yaongezeke ili wagonjwa waweze kutibiwa kwa ujuzi wa hali ya juu.
“Kupitia mafunzo haya tumeanza kupokea wataalamu kutoka nje ya nchi kushiriki mafunzo kwani hadi sasa tumeshatoa mafunzo kwa wataalamu kutoka Sudan, na sasa tuna maombi ya ushiriki kutoka Kenya, na Zambia”, alisema Dkt. Faya.
Naye mshiriki wa mafunzo hayo kutoka Hospitali ya Mwananyamala Dkt. Mwanahawa Hamidu alisema hii ni mara yake ya pili kushiriki mafunzo hayo yanayomuwezesha kutoa huduma bora na kufanya maamuzi kwa wagonjwa wa dharura na mahututi.
Dkt. Mwanahawa alisema mafunzo aliyoyapata mwanzo yamekuwa chachu kwake kumfanya ashiriki kwa mara ya pili ili aweze kujifunza zaidi na kwenda kurahisisha matibabu huku akiokoa maisha ya wagonjwa anaowahudumia.
“Fursa hizi zinapotokea kwetu madaktari zinatusaidia kuongeza ujuzi, kwani kama una vitu viwili ndani yako hapa utatoka na vya ziada vitatu au vinne hivyo kuboresha huduma zaidi”, alisema Dkt. Mwanahawa
Wataalamu hao wametoka katika Hospitali ya Benjamini Mkapa (BMH), Shree Hindu Mandal, Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na MloganzilaB (MNH), Bugando Medical Center, Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Hospitali ya Mananyamala, wataalamu kutoka Zanzibar pamoja na Chuo Kikuu cha Aga Khan, na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS).