Wawili kortini wakidaiwa kusafirisha kilo 58 za heroini

Dar es Salaam. Mkazi wa Salasala, Goodnees Remy(32) na raia wa Nigeria, Emmanuel Chigbo (42) maarufu kama Chasi, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye jumla ya kilo 58.62.

Washtakiwa hao ambao wote ni wafanyabiashara wamefikishwa mahakamani hapo, leo Ijumaa, Februari 7, 2025 na kusomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali Mwandamizi, Phoibe Magili, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga.

Kabla ya kusomewa mashtaka hao, hakimu Ruboroga amesema washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mashtaka yanayowakabili, mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Pia kiasi cha dawa walichoshtakiwa nacho hakina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Mshtakiwa Goodness Remy (aliyejifunika uso) akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa kesi yenye mashtaka ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine zenye uzito wa kili 58.62. Picha na Hadija Jumanne

Akiwasomea shtaka mashtaka yao, Magili amedai washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 3346/2025.

Akisoma mashtaka hayo, amedai katika shtaka la kwanza washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 19, 2023 eneo la Salasala, mtaa wa Upendo uliopo wilaya ya Kinondoni, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha kilo 29.71 za heroini kinyume cha sheria.

Shtaka la pili, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 14, 2023 eneo la Salasala, ambapo washtakiwa walikutwa wakisafirisha kilo 22.91 za heroini.

Shtaka la tatu, siku na eneo hilo, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha kilo sita za heroini, kinyume cha sheria.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yao, upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kwenda Mahakama Kuu kusajili nyaraka za kesi hiyo.

Hakimu Ruboroga ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 21, 2025 kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Related Posts