MABINGWA watetezi wa Kombe la FA, Yanga wamepangwa kucheza dhidi ya Coastal Union ya Tanga kwenye raundi ya 32 ya michuano hiyo huku wekundu wa Msimbazi, Simba wakipewa TMA Stars ya Championship wakati Azam ikiwa dhidi ya Mbeya City.
Droo ya Kombe la FA, ilichezeshwa jana, Ijumaa makao makuu ya Azam TV, Tabata jijini Dar es Salaam huku ikisimamiwa na Meneja Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto. Kwa mujibu wa matokeo hayo ya droo, michezo ya raundi 32 inatarajiwa kuchezwa kati ya Machi mosi hadi nne.
Yanga na Coastal zina kumbukumbu ya kukutana kwenye michuano hiyo ambapo mara ya mwisho ilikuwa Julai 2022 katika mchezo wa fainali ambao ulishuhudiwa timu hizo zikitoka sare ya mabao 3-3 na waliamuliwa kwa mikwaju ya penalti 4-1. Ulikuwa ushindi wa tabu kwa Wananchi.
Mshindi wa mchezo kati ya Yanga na Coastal Union atakutana na mshindi kati ya Polisi Tanzania na Songea FC katika raundi ya 16 bora.
Baada ya Simba kuing’oa Kilimanjaro Wonders, sasa ni zamu ya kukabiliana na TMA Stars ambayo inafanya vizuri katika Championship msimu huu na mshindi wa mchezo huo atacheza dhidi ya Tanzania Prisons au Big Man.
Katika raundi inayofuata ambayo itakuwa mwanzoni mwa Aprili mshindi kati ya Azam dhidi ya Mbeya City atacheza kati ya Mtibwa Sugar ambayo inaongoza msimamo wa Championship au Towns Stars.
Akiongelea sehemu ambayo fainali ya msimu huu itachezwa, Kizuguto alisema; “Bado tunaendelea kupokea maombi ya mikoa hivyo bado mchakato unaendelea.”
Cosmopolitan FC vs KMC FC
Mbeya Kwanza vs Mambali Academy
Tanzania Prisons vs Big Man
Kagera Sugar vs Namungo
Polisi Tanzania vs Songea United
Kiluvya Utd vs Pamba Jiji FC
Mtibwa Sugar vs Towns Stars
Giraffe Academy vs Green Warriors
JKT Tanzania vs Biashara Utd
Tabora Utd vs Transit Camp
Mashujaa FC vs Geita Gold
Yanga SC vs Coastal Union
Fountain Gate vs Stand Utd