UKIMUONA Diarra Djigui akichezea mpira kwa mbwembwe akiwa langoni usishangae kwani alishawahi kuwa mchezaji wa ndani akitumika kama kiungo, lakini unaambiwa Hashim Omary alivishwa jezi ya kipa wa Fountain Gate na kuibania Simba jana mjini Manyara hajawahi kudaka kokote kule kabla ya jana.
Mshambuliaji huyo wa Fountain Gate alilazimika kukaa langoni baada ya kipa John Noble kupewa kadi ya pili ya njano iliyosindikizwa na nyekundu kwa kupoteza muda katika pambano la Ligi Kuu Bara lililopoigwa Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa na timu hizo kutoka sare ya 1-1. Fountain ililazimika kumrudisha Hashim langoni kwa vile ilishamaliza idadi ya wachezaji wa kubadilisha.
Dakika 14 za majeruhi zilizotumika, Hashim aliyetumia jezi ya kipa wa akiba, Fadhil Kisunda alionyesha umahiri ikiwamo kuokoa mchomo mmoja mkali wa chini chini ambao kama sio umakini wake ingeipa Simba ushindi katika mchezo huo.
Hashim ameliambia Mwanaspoti kwamba, katika maisha ya uchezaji hajawahi kukaa langoni kudaka isipokuwa jana na anashukuru kwa kuikoa timu hiyo, huku akikiri mchezaji aliyekuwa akimnyima raha katika mechi ni winga Ellie Mpanzu.
Kipa huyo alisema a baada ya Noble kutolewa kwa kadi nyekundu, benchi la ufundi chini ya kocha Robert Matano na wachezaji wakafanya kikao cha dharura kilichoamua adake kwa muda uliosalia.
“Niliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Salum Kihimbwa. Nilipotakiwa kukaa langoni nikawa nashangaa kwa nini nachaguliwa wakati sijawahi kucheza nafasi hiyo tangu utoto wangu, sikupata presha wakati huo niliamini mabeki watajiongeza zaidi kuhakikisha wananilinda,” alisema Hashim.
“Baada ya kukaa kama dakika moja langoni, ndipo nikakuta presha inapanda na kushuka kutokana na jinsi mastaa wa Simba walivyokuwa wanapigiana pasi, lakini mchezaji hatari zaidi ambaye alikuwa anapiga mipira ya mbali ni Mpanzu.
“Baada ya kuona Mpanzu ana pasi za mwisho za hatari na ameamua kupiga mashuti ya mbali kutokana na mabeki kuweka ukuta nikawa makini naye kila anapokuwa na mpira mguuni. Ndio maana ikawa rahisi kudaka shuti lake lililolenga lango.”
Alisema, huu ni msimu wa pili kucheza Ligi Kuu baada ya kupandishwa uliopita kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, hivyo bado hana uzoefu wa kutosha.
“Nimecheza mechi tatu na Simba ya kwanza katika msimu wangu wa kwanza tulifungwa mabao 3-1 Uwanja Azam Complex. Tulifungwa mabao 4-0 Uwanja wa KMC na hii ambayo tumetoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa, Babati – Manyara. Hivyo najisikia faraja kuona nimefanyika kuwa msaada kwa timu kutofungwa tena na Simba,” alisema Omary anayemkubali Clement Mzize anavyopambana.
Alisema kocha wa timu yao ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Abubakar Ally ndiye aliyemuona akicheza mtaani msimu uliopita akamsajili na hawakumchelewesha kumpandisha.
Hashim alisema baada ya mechi na Simba alipokea simu nyingi na pesa kutoka kwa watu asiyowajua wakimpongeza kwa kazi nzuri.