Boli limo halafu  komedi freshi!

SOKA lina burudani yake, lakini ndani ya wanaocheza pia wana burudani zao mbalimbali ambapo timu nyingi zikiwa kambini baadhi ya wachezaji hugeuka na kuwa burudani kwa wenzao.

Azam FC iliwahi kumwajiri Mbwiga wa Mbwiguke kuwa sehemu ya kikosi ili kuwaburudisha wachezaji wanapokuwa safarini kwenye mechi mbalimbali za ligi na hata kambini wanapocheza nyumbani.

Hebu tuwaone wachezaji sita ambao wako kwenye timu mbalimbali ambao ni maarufu kwa kuwachekesha wenzao kwa vituko mbalimbali na wakikosekana, ni lazima wauliziwe walipo.

Huyu ni mchezaji mpya wa KenGold ya Mbeya, lakini amewahi kufanya kazi na Yanga na Simba. Mahali alipo Morrison ni lazima atajulikana kutokana na vituko vyake kwani atawatania wenzake na watu wengine bila kujali nafasi zao.

Hata kwenye mitandao ya kijamii pia utakubali uchekeshaji wake kwa vituko mbalimbali. Angalia majuzi alivyowageukia Yanga akiwaambia timu yake mpya, KenGold wataibadili jina wakati wanakwenda kukutana na mabingwa hao kwa lengo la kutafuta ushindi na wataita MC KenGold akiidhihaki na ile MC Alger ambayo iliinyima Yanga nafasi ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu.

Kiungo mkongwe wa Namungo FC ya Lindi, lakini amewahi kufanya kazi Azam FC na Simba. Nyoni anahesabika kuwa mchezaji mcheshi zaidi kwa kuwaigiza wachezaji wenzake na hata kambini. Ikitokea kuna mchezaji kataniwa na wenzake wanacheka, basi wa kwanza kuhisiwa anakuwa mkongwe huyo.

Ucheshi wake umemfanya kuwa kipenzi cha wachezaji wengi kwenye timu anayoichezea na akikosekana tu lazima atauliziwa alipo kwa kuwa wenzake wanaona kuna kitu kinakosekana.

Winga huyu wa Yanga akipata nafasi ya kucheza hafanyi ajizi, lakini nje ya uwanja ni mchezaji mwenye vituko vingi kwa wenzake na hugeuka kivutio anapokuwa kambini na timu.

Nkane ucheshi wake hauishii kambini pekee kwani hata mitandaoni hutembeza vipande vya video akiwatania wenzake na kuleta mvuto mkubwa kwa mashabiki wa soka. Kuna wakati aliwahi kutoa swali eti yeye na mwenzake Kibwana Shomari nani mrefu. Hebu fikiria hapo nani zaidi?

Kiungo wa Simba aliyetolewa kwa mkopo kwenda Namungo, kwani ukifika katika kambi ya Wekundu wa Msimbazi mchezaji ambaye anahesabika kuwa ‘komediani’ mkubwa alikuwa kijana huyu kutoka Tanga aliyesajiliwa na klabu hiyo akitokea Zanzibar.

Karabaka anachekesha kila baada ya kauli yake. Anaweza kukuchekesha hata wakati anakusalimia tu, kwani hata alipotangazwa anakwenda kwa mkopo Namungo wachezaji wenzake waliumizwa na taarifa hiyo kutokana na namna alivyokuwa kipenzi chao katika ucheshi.

Unamuona Feisal Salum ‘Fei Toto’ anavyoubonda akiwa uwanjani? Basi elewa kwamba jamaa pia ni mtu mwenye vituko akiwa kambini kwani anapenda kufurahi wakati wote na hata kuwafurahisha wenzake.

Fei Toto hata mitandaoni kuna video nyingi anazopoti kuwachekesha mashabiki na hivi majuzi aliwavunja mbavu aliposhindwa kutaja idadi ya rangi zilizopo kwenye bendera ya Tanzania, akidai zipo sita huku akishindwa kabisa kuzitaja ilhali akicheka. Lakini pia ni mjuzi wa kutania wachezaji wenzake kupitia ‘status’.

Huyu jamaa ni beki wa Yanga ambaye akikutana na Nkane lazima ujiandae kucheka vibaya. Hawa watu wana vita ya kutaniana. Hebu kumbuka wakati beki mwenzake, Yao Akouassi, akionyesha kiwango bora akaenda kuandika mitandaoni kwamba kazini kwake kuna kazi. Msemo huo uliwaacha wengi wakicheka.

Kibwana anapenda kuchekesha sana wenzake na hivi karibuni alivyorudi uwanjani tu akiona wachezaji wengi waliokuwa  hawafanyi vizuri wanaonyesha makali, kisha wakiweka picha kwamba walikwenda kuombewa na wachungaji mbalimbali, basi yeye akaja na yake aliporudi kwa kishindo akasema “unaweza sema na mimi nilienda kwenye maombi.”

Ukiingia kwenye akaunti ya Instagram ya Kibwana utacheka zaidi. Alipoupiga mwingi dhidi ya TP Mazembe kwenye mechi ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika aliandika “jana simu iliisha chaji nikashindwa kuposti” akaupiga tena mpira mwingi Yanga ikishinda 5-0 dhidi ya Fountain Gate kisha akaandika, “jana kumbe tulishinda tano.” Mambo hayo, uwanjani wamo na utani pia wanaweza, basi raaaaaha mstarehe!

Related Posts