Na Mwaandishi wetu Michuzi Tv
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, amezitaka taasisi za serikali zinazokusanya mapato kupitia utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi ndani ya kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuimarisha uwezo wao wa kifedha na kufanikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato waliyojiwekea.
Taasisi hizo ni Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mamlaka ya Maji Same Mwanga (SAMWASA), Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Halmashauri ya Wilaya ya Same pamoja na kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Akizungumza katika kikao cha mapato ambacho kimewakutanisha Halmashauri ya Wilaya ya Same, wakuu wa taasisi za serikali ndani ya wilaya hiyo katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni amesisitiza umuhimu wa kuboresha vyanzo vya mapato vilivyopo na kuanzisha vipya ili kuhakikisha taasisi zinakusanya mapato kwa asilimia 100 au zaidi kwa mwezi na kwa mwaka.
“Ni lazima tuwe wabunifu katika kubuni vyanzo vipya vya mapato ili tuweze kufanikisha malengo yetu ya ukusanyaji wa mapato. Bila kuboresha vyanzo hivi, taasisi zetu zitashindwa kufikia malengo ya makusanyo ya mapato,” alisema Mhe. Kasilda.
Katika kikao hicho, ilibainika kuwa moja ya changamoto zinazoathiri ukusanyaji wa mapato ni uharibifu wa miundombinu unaofanywa na baadhi ya wananchi wasio waaminifu, hususan katika sekta ya usambazaji maji. Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa Wilaya amesema msimamo wa serikali ni kuwachukulia hatua kali wote watakaobainika kuharibu miundombinu hiyo kwa kuwa vitendo hivyo vinakwamisha maendeleo.
“Serikali haitavumilia vitendo vya uharibifu wa miundombinu vinavyofanywa na watu wachache kwa maslahi yao binafsi. Tutahakikisha wote wanaobainika wanachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria kwa sababu hii miradi ni kwa ajili ya kuwawezesha wananchi wenyewe kupata huduma karibu” amesisitiza Mhe. Kasilda.
Aidha, Mhe. Mgeni amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuhakikisha wakusanyaji wa mapato wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara kuhusu matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki (POS) ili kuepusha mianya ya upotevu wa fedha. Hii itasaidia kuongeza uwazi na ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Lengo la kikao hicho ni Kupitia na kufanya tathmini ya makusanyo ya mapato ya ndani kwa kila taasisi, kubaini changamoto za ukusanyaji wa mapato na kuzitafutia suluhisho pamoja na kupanga mikakati ili kuhakikisha malengo yanatimia kwa asilimia 100 au zaidi.
Hatua hii inalenga kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa mapato, kuhakikisha uwajibikaji, na kusaidia taasisi za serikali kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.