Na Mwandishi Wetu,Michuzi TV
Baada ya kuwa na Sheria ya ushindani kwa sasa FCC wanaendelea na mchakato wa kufuata utaratibu ili kuhakikisha Sheria ya Alama za Bidhaa nayo inafanyiwa marekebisho kwa lengo la kuiwezesha kuakisi hali ya sasa ya maendeleo ya biashara duniani na kusisitiza hivyo utaratibu wake unakuja.Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani(FCC)William Erio wakati akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha maofisa wa tume hiyo na Wahariri wa vyombo vya habari nchini ambapo lengo kuu la kikao hicho ni kujengena uwezo kuhusu majukumu yanayotekelezwa na tume.
Akieleza kuhusu wanavyofanya kazi zao kwa mujibu wa sheria amesema kwa sasa wanazo sheria mbili ambako ya kwanza ni Sheria ya Ushindani ambayo imefanyiwa marekebisho hivi karibuni.
“Na katika hili kupitia kwenu naomba kufikisha shukrani kwa Rais DK.Samia Suluhu Hassan kwasababu mchakato huu ulianza miaka 14 iliyopita lakini haukuweza kukamilika lakini ndani ya mwaka mmoja Rais Dk.Samia amewezesha hili kukamilika na sheria sasa imefanyiwa maboresho ili kufanya mazingira ya uwekezaji yanakuwa mazuri.
“Pia naomba kumshukuru Rais Samia kwa kutia saini sheria ile baada ya kupitishwa na Bunge ili sheria hii iweze kutumika na katika kikao hiki tutaeleza kwa kina mjue nini kimebadilishwa katika sheria na nini tukitatarajie katika Sheria ya Ushindani,”amesema Erio.
Aidha amesema pia wanatumia Sheria ya Alama za bidhaa na kwa sasa wameanza mchakato wa awali maana nayo ni ya siku nyingi hivyo inahitaji kufanyiwa marekebisho na iwe inaakisi hali ya sasa ya maendeleo ya biashara duniani.“Hivyo utaratibu wake unakuja na wakati utafika nayo itabadilishwa kupitia taratibu zilizowekwa.”
Ametumia nafasi hiyo pia kueleza umma kupitia kikao hicho kuwa hivi sasa FCC wamepata Cheti cha Ithibati cha utoaji huduma bora kimataita na kwamba sasa huduma zao zitakuwa nzuri zaidi, huduma zinazotabirika, huduma zinazofuata taratibu za Kimataifa.
“FCC ilianza tangu mwaka 2003 ,ni muda mrefu lakini sasa tumepata Cheti cha Ithibiti za Utoaji huduma kwa kuzingatia taratibu za Kimataifa na sisi wateja wetu wengi ni wa Kimataifa,na ndio maana hata shughuli tunazofanya ni za Kimataifa.”
Kuhusu kudhibiti bidhaa bandia amesema wanafanya ukaguzi katika bandari na sehemu nyingine za kuingia nchini kwa kuhakikisha bidhaa bandia haziingii katika nchini na hilo wanalifanya kwa ukaguzi,hapo zamani walikuwa wanakwenda bandarini na kusubiri mzigo utoke wakague.
“Tumezungunza na wenzetu wa TRA ili FCC iingizwe katika mfumo TANOGA ambapo mtu anapotoa taarifa za mzigo wake ukifika bandarini wakati huo huo na FCC tunaona taarifa zote hivyo kama kuna kitu cha kushughulika basi tunachukua hatua mara moja.Mfumo huu tutakuwa tunapata taarifa mapema ili tushughulikie na mzigo uingie sokoni mapema,”amesema Erio.