NYOTA Mtanzania aliyetambulishwa na Wydad Casablanca ya Morocco, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ amesema amefarijika kutimiza ndoto ya kucheza soka la kulipwa na sasa anajipanga ili kufanya vizuri akiwa na kikosi hicho.
Usajili wa mshambuliaji huyo kutoka Singida Black Stars ambaye alikuwa anakipiga kwa mkopo Fountain Gate kwenda Wydad ulifanyika dakika za jioni na kuzua maswali kwa wadau, lakini mwenyewe amesema kuwa haikuwa rahisi kwake pia kuamini kama dili hilo litatimia.
“Mimi pia nilipokea taarifa kwa mshtuko na ilikuwa simu ya kuambiwa kila kitu kimekamilika kinachosubiriwa ni mimi kujiandaa kwa ajili ya kwenda kupambania malengo yangu. Nashukuru Mungu mambo yameenda vizuri hadi natambulishwa huku,” alisema Gomez na kuongeza;
“Mipango iliyopo sasa baada ya ndoto ya kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania kutimia ni kupambania malengo kwa kufanya kile ambacho kinatarajiwa na wengi kuhakikisha napata nafasi ya kucheza.”
Alisema malengo ni kutimiza ndoto zake ambazo siku zote alikuwa anatamani kuzifikia hivyo anapambana kuhakikisha anajitengenenea mazingira mazuri ya kucheza baada ya kutambulishwa na timu hiyo.
Pia alitumia nafasi hiyo kushukuru timu alizopita hadi kufikia ndoto yake ya kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania na sasa anajipanga ili kufanya kazi iliyompeleka Morocco. Hadi anaondoka nchini, Gomez alikuwa ameifungua Fountain Gate mabao sita katika Ligi Kuu Bara.
“Awali ya yote, nipende sana kumshukuru Mungu kwa afya, siha njema na pumzi (alhamdulillah). Nipende kutumia fursa hii kuwashukuru KVZ FC (Zanzibar) kwa kunilea na kunipa nafasi ya kuonekana, lakini pia niwashukuru sana Singida Black Stars FC pamoja na uongozi wake wote kwa kuniona, kuniamini na kunipa mkataba mkubwa wa kucheza ligi kuu ya Tanzania,” alisema na kuongeza:
“Vilevile kipekee naomba niushukuru sana uongozi wa Fountain Gate FC, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzangu.” Suleiman ametua Wydad akiungana na nyota wengine wapya waliosajiliwa katika dirisha la usajili la majira ya baridi kwa Wydad akiwamo kipa Mehdi Benabid; mabeki Fahd Moufi, Mikael Malsa, Hamza Ftiti, Zakaria Fatihti na Mohamed Jaddidi pamoja na Msauzi Thimpenkosi Lorch.