Halmashauri Mafinga yajipanga kukabili athari za Trump kufuta misaada

Mufindi. Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji Mafinga, wilayani Mufindi Mkoa wa Iringa limetenga Sh15.6 milioni kwa ajili ya malipo ya watumishi waliokuwa wakilipwa na taasisi za Benjamin William Mkapa Foundation na Mpango wa USAID Afya Yangu.

Uamuzi huo uliofikiwa wakati halmashauri ikisubiri maelekezo ya Serikali, unatokana na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kutangaza kusitisha utoaji fedha mpya na usambazaji wa fedha chini ya makubaliano ya malengo ya Maendeleo (DOAG) hadi uhakiki kwa programu za msaada wa nchi zinazofadhiliwa na USAID utakapokamilika ndani ya siku 90 kuanzia Januari 24, 2025.

Mchakato wa uhakiki unalenga kuhakikisha msaada wa nje unalingana na ajenda ya sera ya nje ya Rais Donald Trump.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Regnant Kivenge amesema hayo leo Februari 8, 2025 wakati wa kikao cha kawaida cha baraza la madiwani kupitia bajeti za robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025 kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Madiwani wa halmashauri ya Mji Mafinga wakiwa katika kikao Cha Baraza hilo. Mary Sanyiwa

Amesema wakati wakisubiri tamko la Serikali, halmashauri imejipanga na kuchukua hatua madhubuti kutenga kiasi hcho cha fedha kuhakikisha wanawatoa hofu wanufaika waliokuwa wanahudumiwa na taasisi hizo.

“Halmashauri yetu ilikuwa na wafanyakazi wapatao 73 kwenye taasisi hizi, tulimuomba mganga mkuu aangalie maeneo muhimu ambayo wakipunguza haitaweza kuathiri, hivyo kuleta idadi ya watumishi 26 ambao tutaendelea kuwatumia na kuwalipa kiasi hicho cha fedha ambacho halmashauri imemua kukitenga,” amesema.

Amesema watumishi hao walikuwa wanatoa huduma za ushauri kwenye vituo vya afya vya halmashauri hiyo, ikiwamo kwenye afua za Ukimwi, Kifua Kikuu (TB), uzazi wa mpongo, saratani ya shingo ya kizazi na huduma ya mama na mtoto.

Mwenyekiti huyo amesema maeneo mbalimbali yalikuwa yamefadhiliwa na mashirika hayo, hivyo watumishi 26 wataendelea katika afua hizo.

Amesema licha ya madaktari wa halmashauri hiyo kuwa vizuri, lakini wafanyakazi hao walikuwa wanasadia kutoa huduma ya mama na mtoto ili kuhakikisha wanapunguza mzigo kwa watumishi  wa afya, ndiyo maana waliajiriwa kwenye mashirika hayo.

“Ajira hizi zitakwenda kwa miezi mitatu kama ambavyo agizo linasema kwa sababu, Rais wa Marekani Trump ametoa siku 90 anaweza kufikiria vinginevyo kisha atatoa majibu katika miezi hiyo, wakati anajifikiria cha kufanya halmashauri ikaona  iweze kusaidia katika maeneo hayo ili wananchi wasiweze kuathiriwa,” amesema.

Amesema dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi za ARV zipo za kutosha kwa mujibu wa mganga mkuu wa halmashauri hiyo, hivyo wananchi wataendelea kuhudumiwa kama kawaida.

“Dawa hizi zipo kwa muda huo, lakini baada ya hapo upo utaratibu wa masuala ya kununua dawa na kuagiza kama ilivyokuwa siku zote, kwa sababu huwa zinachukuliwa Bohari ya Dawa (MSD),” amesema.

Awali, akichangia hoja baada ya kuwasilishwa taarifa ya Kamati ya Ukimwi, Diwani wa Wambi, Menja Kalinga aliipongeza halmashauri na wataalamu kwa hatua waliyochukua ya kutenga fedha hizo.

“Niwasihi wananchi kama wamesikia taarifa zozote kuhusu agizo la Rais wa Marekani, lakini niwatoe hofu dawa zitakuwepo na huduma hizo zitaendelea kutolewa kama kawaida kwa sababu halmashauri imejipanga vizuri,” amesema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu swali la papo kwa hapo bungeni Februari 6, 2025 alisema Serikali inajiimarisha kukuza uchumi kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kumudu utekelezaji katika maeneo yote muhimu yakiwamo ya sekta ya afya, elimu na maji.

Majaliwa alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, George Mwanisongole aliyehoji Serikali inajipangaje kukabiliana na mabadiliko ya sera za nje za Marekani zinazokwenda kuathiri utekelezaji wa sera za Tanzania kwenye maeneo kadhaa yakiwamo ya elimu na afya.

Alisema Tanzania inaheshimu sera za mambo ya nje na inatekeleza mikataba ya sera hizo kama ambavyo wamekubaliana na nchi husika kwenye maeneo mbalimbali.

“Tumeanza kuona nchi zenye uwezo mkubwa ikiwamo Marekani na mabadiliko haya yanaathiri baadhi ya nchi na hata yetu inaweza kupata baadhi ya athari, lakini kwetu ni muhimu kuzingatia sera za nje kama ambavyo tumekubaliana,” alisema Majaliwa.

 “Uwezo tunao, tunazo maliasili, tunazo rasilimali, kazi ambayo tunayo ni Watanzania kushirikiana kuhakikisha tunatumia maliasili na rasilimali tulizonazo kujenga uchumi wa ndani kuwezesha mipango na bajeti iweze kutekeleza haya.”

Bunge Februari 4, 2025 liliazimia Serikali itekeleze mpango wa kupata rasilimali za ndani kupambana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi bila kutegemea msaada wa wafadhili.

Azimio la Bunge lilifikiwa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu kuwasilisha taarifa ya kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa shughuli zake kati ya Februari 2024 hadi Februari 2025.

Kingu alisema kiwango kikubwa cha utekelezaji wa afua za VVU na Ukimwi nchini hutegemea fedha za wafadhili kutoka nje ya nchi.

Related Posts