Dorice John ameeleza namna ndoa yake ilivyovunjika kutokana na ugomvi ambao kama mmoja wao angejishusha, ulikuwa unamalizika kwa mazungumzo.
Amesema, yeye ndiye alikosewa, hivyo njia rafiki aliyoamini inafaa kuonyesha hisia zake ni kumnunia mumewe, aliyemtaja kwa jina moja la Michael akiamini kwa kufanya hivyo ataombwa msamaha.
“Tulikaa wiki nzima hatuzungumzi, nikaamua kuondoka kurudi nyumbani kwetu, mume wangu hakunitafuta, nilikaa kwetu miezi mitatu bila kuwasiliana naye.
“Hali ile ilipunguza upendo kati yetu, mwanzoni nilihisi atanibembeleza nirudi nyumbani, hakufanya hivyo, kumbe mwenzangu alikuwa serious, kuja kutahamaki mume wangu anaoa mwanamke mwingine,” anasema Dorice kwa uchungu.
Japo ni miezi 10 imepita tangu ndoa ya Dorice kuvunjika, anasema ni jambo ambalo analijutia hadi sasa.
“Nilikuwa naweza kumaliza ugomvi wetu kwa mazungumzo na tukaendelea kuishi kwa amani na upendo, nilipomnunia nilihisi Michael atanibembeleza kwa jinsi alivyokuwa akinipenda, sikutarajia ndoa yetu ivunjike hivi,” amesema.
Mchungaji Daniel Mgogo amesema kinachotokea kwa wanandoa kutozungumza hadi kuachana kama ilivyotokea kwa Dorice ni kiburi.
Anasema mke anaweza kuishi kwa hisia kwamba mumewe anamfanyia ujeuri kutokana na fedha na mume pia anaweza kuhisi hivyo na kuibuka matokeo ya kiburi.
“Wanasahau kwamba mkishaingia kwenye ndoa, hata kama mwenzako amekuumiza, ushindi mkuu ni kuzungumza na kumaliza tofauti kwa ku-riski furaha yako kwa ajili ya wengine,” amesema.
Mchungaji Mgogo amesema, ndoa ni taasisi inayowahusu watu wanne, akimtaja mtu wa kwanza kuwa ni wanandoa wenyewe, yaani mke na mume.
“Mtu wa pili kwenye taasisi ya ndoa ni watoto, mtu wa tatu ni wazazi na mtu wa nne katika ndoa ni ndugu na jamaa, mnapooana wawili, hiyo si ndoa yenu peke yenu, kuna kundi linawahusu,” anasema.
Katika jamii mambo yako hivi
Ukiachana na Dorice, baadhi ya wanandoa wanasema ugomvi huwa hauepukiki, lakini vitu wanavyoviepuka ni hadi kwenda kulala kila mmoja akiwa amekasirika bila kumaliza tofauti.
“Mimi na baba Rey (mumewe) kugombana ni kitu cha kawaida, tunaweza kugombana tukiwa kazini, tukirudi nyumbani tunazungumza yanakwisha.
“Tangu tumefunga ndoa 2019, hatujawahi kwenda kulala bila kumaliza tofauti kama tumegombana,” amesema Mariam Juma.
Amesema wakiwa wachumba, waligombana na kununia wiki nzima bila kuwasiliana, jambo ambalo liliwaumiza wote.
“Kilikuwa kipindi kigumu, tuligombana Jumapili tukaja kupatana Jumapili iliyofuata, yeye (mumewe) ndiye alianza kunipigia akidai amekuta miss call yangu, wakati sikuwa nimempigia, tukabishanabishana, akajichekesha ugomvi ukaisha, tukakubaliana marufuku kununiana,” anasema.
Elisha Manyama anasema waliwahi kuishi miezi mitatu na mkewe bila kuzungumza baada ya kutofautiana.
“Ilikuwa ni kama hatupo kwenye ndoa, mimi niliweza kulala nje hata siku tatu nikirudi haniulizi, akawa anawatumia watoto wanipigie, kwa kiasi fulani iliwaathiri watoto,” anasema.
Mwalimu Emmanuel Kamenge amegusia migogoro hiyo inavyowaathiri watoto hadi taaluma, akitolea mifano ya baadhi ya wanafunzi kwenye shule ya sekondari ya Dar es Salaam anayofundisha.
“Kuna mwanafunzi alikuwa akifanya vizuri katika masomo, ghafla ufanisi wake ukashuka, nilipomhoji kujua nini changamoto, akanieleza namna wazazi wake wanavyogombana mara kwa mara.
Anasema changamoto hiyo inaweza kumsababishia mtoto msongo wa mawazo, hofu, na wasiwasi ambayo hupelekea kukosa hata utulivu na kupunguza umakini wanapokuwa darasani.
Athari zake kijamii, kisaikolojia
Wanasaikolojia na mtaalamu wa masuala ya malezi, mchungaji Daniel Sendoro, anasema kununa ni tatizo la kisaikolojia, linalosababisha uishi kwenye makasiriko na uchungu.
“Ambacho watu wanapaswa kukifahamu ni kwamba ndoa au mahusiano ni biashara inayowaweka pamoja muda mrefu, hivyo haipaswi kununiana.
“Hamuwezi kuishi kwa amani kila siku katika ndoa, lakini ikitokea mnagombana suluhisho si kununa, bali kutafuta suluhu,” anasema.
Anasema kununa ni gharama na mzigo kwa kuwa kunakukosesha furaha, huwezi kuwasiliana na ikitokea umewasiliana basi utawasiliana vibaya na kuzidi kuchochoa migogoro.
Mchungaji Mgogo anasema lengo la ndoa ni furaha, inapokosekana lile lengo linafeli na hata kuwasababishia watu magonjwa kama presha, vidonda vya tumbo au maumivu ya kichwa.
“Kuna watu tunawasikia wanasema ndoa ni stress, kwani kile walichokitarajia ni tofauti na walichokikuta, hivyo kupoteza furaha ambayo kiuhalisia ni tiba,” anasema Mchungaji huyo na kuongeza:
“Narudia tena hili, ndoa siyo taasisi ya mtu mmoja, mtaoana mke na mume, lakini kuna watu wanaizunguka hiyo ndoa, furaha yao ni furaha, amani na upendo kwenye ndoa yenu, mkigombana amani yako haiwezi kuwepo”.
Anasema kama ndoa hiyo ilijaliwa watoto, basi watakaa katikati ya makwazo ya wazazi wao na mwisho nao watagawanyika na kusababisha familia kusambaratika.
“Athari nyingine kwenye ndoa ni kituo cha matumizi ya fedha, mkiingia huko mtatakiwa kuwa na vyanzo vya pesa, mkigombana na kutofikia muafaka hata uchumi wa familia mtauharibu.
“Mkiwa na gari mtaliuza, nyumba hata mali nyingine, uchumi ukiyumba wale watu waliokuwa wanafaidika kupitia ninyi nao watapoteza mwelekeo,” anasema.
Katika athari ya familia kupoteza mwelekeo, Seleman Mutabazi anatolea mfano baadhi ya kina baba wanapogombana na wake zao hata matumizi ya watoto hatoi.
“Wapo ambao amegombana na mkewe, anaondoka bila kuacha pesa ya chakula, akikasirika anakasirika na kila kitu, jambo ambalo si sahihi,” anasema.
Anasema katika migogoro ya wanandoa, waathirika wakubwa ni watoto, akitolea mfano wa rafiki yake aliyegombana na mkewe.
“Hadi leo hatujui alipo, aliacha watoto ambao baba hawezi kuwalea peke yake, akawapeleka kwa bibi yao ambaye naye mgonjwa hawezi kufuatilia kama mtoto kaenda shule au la, mwisho wa siku tunatengeneza kizazi cha aina gani?” amehoji.
Anasema, kununiana kwa wenza kuna athari nyingi, kubwa ni kusababisha kutengana, akiamini katika kununiana ndipo usaliti huanzia.
“Mapenzi ni faraja, kama anaikosa kwa uliyemtarajia hapo ndipo baadhi wanalazimika kutafuta faraja mbadala na kuchochea usaliti.
“Kwenye ndoa huwa inaumiza mwenzako kukununia, inaumiza zaidi kwa anayependa zaidi, kama mnapendana itawaumiza wote na wapo hali hiyo inawasababishia maradhi na wengine hadi kifo,” anasema.
Mutabazi anafafanua kwamba msingi wa ndoa zote ni kuishi kwa uvumilivu, upendo na unyenyekevu, vitu hivyo vinapokosekana ndipo inazaliwa migogoro, akisisitiza mke kuishi kwa utii na mumewe na mume kuishi kwa akili na mkewe.
Daktari wa binadamu, Daud Gambo anasema si kwa wanandoa tu, mtu yeyote anapoishi kwa makasiriko inamsababishia msongo wa mawazo.
“Akiishi muda mrefu akiwa na msongo wa mawazo, kiafya itamsababishia Sonona na kupitia katika katika hofu na wasiwasi.
Dk Gambo, ambaye ni meneja mradi wa afya ya mama na mtoto na mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la Word Vision, anasema mtu mwenye msongo wa mawazo anaweza kuongezeka uzito kupitiliza au kupungua uzito kupitiliza.
“Wapo ambao akifikia hatua hiyo ndicho kipindi anapata sana hamu ya kula, hivyo anakula kupitiliza, akiona chakula ndicho kinampa faraja hivyo kuongezeka uzito kupitiliza.
“Mwingine anapoteza hamu ya kula, kwa hiyo inapelekea mtu kupungua uzito na kupata changamoto nyingine za kiafya,” anasema.
Mchungaji Mgogo anasema hakuna ndoa ambayo haina migogoro, lakini wanapopitia vikwazo wasiweke kiburi.
“Wanapopitia vikwazo ni vema wanandoa hao kuwa wepesi kusuluhisha kwa faida ya kizazi chao,” anasema.
Mchungaji Sendoro anasema: “Kununiana kwenye mahusiano hakujawahi kuwa na matokeo mazuri, na kisaikolojia hali hii inamuacha mtu na majeraha.
“Ni hatari kwa afya na unaweza kumdhuru aliyenuna, hivyo ni vema aliyenuniwa atafute suluhu kwa kuuliza ili wazungumze yaishe, njia ya pili ni kumpa nafasi akimaliza kununa aongee.
Mwalimu Kamenge anasema wazazi wanapogombana, jambo kubwa ni kuhakikisha hawawahusishi watoto kwenye migogoro yao.
“Njia salama ni kutafuta mbinu bora zaidi ya kutatua migogoro ili kuhakikisha watoto wanakua katika mazingira salama, yenye amani, na yanayowajenga kuwa watu wenye furaha.
“Kinyume na hapo, huyo mtoto naye atakua katika mazingira hayo na atakapokuwa mkubwa ataona ni kawaida kufanya hivyo kwa mke au mumewe,” anasema.
Kadhi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Ramadhan Kitogo anasema mambo hayo katika nyumba yanatokea, lakini suluhisho ni aliyesababisha mgogoro kujishusha na siyo kuruhusu kununiana.
“Kama mwenzako amenuna, unapaswa kujua sababu na kumaliza tofauti, sisi katika misingi na taratibu za Kiislamu katika ndoa mume ndiye anabebeshwa majukumu makubwa na ndiye anatakiwa ailee ndoa.
“Ikitokea ndani hamzungumzi, anapaswa aangalie suluhisho na mke hatakiwi kupaniki, kinachotakiwa ni mmoja kujishusha na kufikia muafaka, hakuna ndoa ya mke au mume akipanda na mwingine anapanda,” anasema.