Kikwete ajenga ukumbi wa mikutano Bukombe

Geita. Rais mstaafu, Jakaya Kikwete amejenga ukumbi wa mkutano wa kisasa katika Shule ya Sekondari Bulangwa, wilayani Bukombe Mkoa wa Geita, kwa ufadhili wa Kampuni ya MM Steel.

Ukumbi huo una uwezo wa kubeba watu kati ya 3,500 na 4,000.

Akiweka jiwe la msingi la ukumbi huo leo Februari 8, 2025, Kikwete amesema kujengwa kwa ukumbi huo kumetokana na tamanio la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko baada ya kukuta ukumbi kama huo katika Jimbo la Chalinze.

Jengo la ukumbi wa mkutano lililojengwa na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete kwa ufadhili wa kampuni ya MM Steel

Amesema Serikali imefanya kazi kubwa katika kuinua sekta ya elimu.

Amempongeza mbunge wa Bukombe, Dk Biteko kwa kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo anayoifanya.

Awali, Dk Biteko alisema mwaka jana alihudhuria mkutano kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM Chalinze, inayoongozwa na Ridhiwani Kikwete, akavutiwa na ukumbi.

Dk Biteko amesema alipotaka kujua siri, ndipo alipopewa taarifa kuwa umejengwa na Rais mstaafu Kikwete.

“Nilimuuliza mdogo wangu Ridhiwani amewezaje kujenga ukumbi, akaniambia si yeye ni mzee. Wakati huo mzee amekaa pembeni yangu nikamuuliza akaniabia unautaka, nikamwambia ndiyo siku ya siku napigiwa simu naambiwa tumepewa kazi ya kujenga ukumbi kwako,” amesema Dk Biteko.

“Kwa kweli ukumbi huu wapo wanaosema umejengwa na Biteko mimi niwaambie leo, ukumbi huu ni wa mzee Kikwete na nimemuomba aje auweke jiwe la msingi,” amesema.

Dk Biteko amesema ukumbi huo kwa sasa ujenzi umefikia asilimia 85 na unatarajiwa kukamilika Mei mwaka huu.

Akisoma taarifa ya ujenzi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Bulangwa, Sane Elizabeth Machembe amesema shule hiyo iliyoanza mwaka jana ina wanafunzi 388.

Rais Jakaya Kikwete akizungumza na wananchi wa Kata ya Bulangwa wilayani Bukombe mkoani Geita

Amesema kujengwa kwa ukumbi huo kutasaidia wanafunzi kuwa na sehemu nzuri na salama ya kukusanyika kwa pamoja.

Pia, utasaidia kuongeza mapato pale utakapokodishwa kwa watu wanaotaka kufanya sherehe au mikutano.

Mwalimu huyo amesema utawawezesha kupunguza gharama za uendeshaji mikutano kwa kukodi ukumbi.

Kikwete yupo wilayani Bukombe kwa ziara ya siku moja, pamoja na mambo mengine ni mgeni rasmi kwenye mkutano maalumu wa CCM wilayani humo wenye lengo la kutoa taarifa ya miaka mitano ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa kipindi cha mwaka 2020/5.

Related Posts