Geita. Rais mstaafu Jakaya Kikwete amesema machafuko na vita vinavyoendelea katika mataifa mengine iwe somo kwa Watanzania kuepuka maneno ya uchochezi yanayotolewa na wanasiasa wasiotaka kulinda na kudumisha tunu za Taifa za umoja, upendo, amani na mshikamano.
Akizungumza leo Februari 8, 2025 kwenye mkutano maalumu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bukombe, uliolenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama hicho, amesema tunu za Taifa zimejengwa kwenye msingi wa kutokubaguana kwa vyama vya siasa, dini, rangi wala makabila.
Amesema endapo tunu hizo zitazingatiwa nchi itakuwa salama na Watanzania wataendelea na shughuli zao kwa usalama, akieleza adui hana udogo.
Kuhusu uchaguzi mkuu mwaka huu, amewataka wanachama wa CCM watakaowania nafasi mbalimbali kumaliza mchakato wa uchaguzi bila tuhuma za rushwa.
Amesema tuhuma hizo zinatia dosari sifa na jina la chama hicho mbele ya wanachama na wananchi wanaoitazama CCM kama kimbilio.
“Huu ni mwaka wa uchaguzi watajitokeza watu kuja kutafuta ridhaa ndani ya chama, kwa kuzingatia kanuni za chama wapokeeni, wakaribisheni kwa kuwa ndiyo demokrasia inavyotaka. Wasikilizeni na muwaulize watafanya nini, lakini kama wakija wakidharau kazi zilizofanyika wapuuzeni wekeni mbele masilahi ya chama,” amesema.
Amewahimiza wananchi kutembea na falsafa ya mafiga matatu kama walivyofanya katika uchaguzi wa mwaka 2020, akisema kwa kuwa na watu wa chama kimoja inakuwa rahisi kufanya kazi.
“Kwa uzoefu wangu wa ubunge miaka 15 na urais miaka 10 inakuwa rahisi kufanya kazi unapokuwa na watu wamoja, kazi zilizofanyika ndizo zimefanya wananchi wakiamini chama na kukichagua kwa kishindo katika uchaguzi wa Serikali za mitaa,” amesema.
Amewataka viongozi na wanachama kusemea maendeleo yaliyofanywa na Serikali ili wananchi waendelee kukiamini CCM.
Kikwete akimzungumzia mbunge wa Bukombe, Dk Doto Biteko amesema tangu akiwa mwanafunzi wa chuo, mwalimu, mbunge na sasa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati hajawahi kubadilika kwa tabia wala mwenendo wake.
“Ni mtu wa watu, hana makuu tangu amekuwa Naibu Waziri Mkuu hajabadilika. Wapo wanaopata uwaziri nanga zinapaa lakini Doto alivyo sasa ni kama alivyokuwa waziri wa kawaida, hana ubaguzi wa rangi, wa dini au wa kabila,” amesema.
Amesema Dk Doto ni msikivu, mnyenyekevu kwa wakubwa na wadogo, asiyeangalia mwenye nacho na asiye nacho na muda wote anatabasamu.
“Ni mtu wenye kifua cha kubeba mazingira yote na anajua namna ya kushughulikia changamoto zinazomkabili,” amesema.
Kikwete amesema kwa kazi alizopewa kufanya, amethibitisha kwa umakini na ni mpenda maendeleo mwenye uthubutu, akimtaka asibadilike na ikitokea kubadilika iwe kufanya kazi na kuongeza heshima.
Kwa upande wake, Dk Biteko amesema Serikali imetekeleza miradi ya maendeleo ikiwamo ya elimu, afya, maji umeme na miundombinu ya barabara.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Ushirombo –Katoro ambao utaanza wakati wowote kuanzia sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema kwa kipindi cha miaka minne, shule 150 zimejengwa katika halmashauri sita za mkoa huo.
Katika sekta ya afya amesema zahanati 53, vituo vya afya 15, hospitali nne za wilaya na hospitali ya rufaa moja vimejengwa na huduma kwa wananchi zinatolewa.
Shigella amesema watumishi 2,500 wa sekta ya afya wameajiriwa, huku wakipokea magari 15 ya kubebea wagonjwa.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa NCCR –Mageuzi wilayani Bukombe, Khamis Ngarama amewaomba wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM wilayani humo kumpitisha Dk Biteko bila kupingwa.
Amesema aliyeanza kumuona Dk Biteko ni Kikwete alipokuwa Rais kwa kumchagua kuwa mjumbe wa bunge la Katiba.
Kauli hiyo iliungwa mkono na mwenyekiti mstaafu wa CCM Bukombe, Zackaria Bwire aliyetaka viongozi na wajumbe wa chama hicho kumpitisha Dk Biteko kuwa mgombea bila kupingwa kutokana na kazi kubwa za maendeleo alizofanya.