Kilichomkuta Bocco Arachuga | Mwanaspoti

KOCHA wa JKT Tanzania, Ahmad Ally amesema sababu kubwa za mshambuliaji nyota wa timu hiyo, John Bocco kushindwa kucheza mchezo wa juzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Coastal Union ni kutokana na kuishiwa nguvu, hali iliyosababisha kukosekana.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha na JKT kuchapwa mabao 2-1, Bocco alikuwa sehemu ya nyota 11 wanaoanza, ingawa muda mfupi tu mechi kuanza alifanyiwa mabadiliko na nafasi yake kuchukuliwa na Edward Songo.

“Baada ya mazoezi ya kupasha mwili ‘Warm Up’, Bocco alisema kifua kinamsumbua na anaishiwa nguvu kwa sababu ya hali ya hewa, ndipo tukashirikiana na madaktari na kuamua kumuondoa katika mipango yetu ya mchezo huo husika,” alisema Ahmad.

Ahmad alisema kitendo cha Bocco kushindwa kucheza kilichangia kwa kiasi kikubwa kupoteza mchezo huo, kwa sababu moja ya mipango aliyoingia nayo ni kutumia sana mipira mingi ya krosi, kwani wapinzani wao walikuwa na udhaifu mkubwa eneo hilo.

“Bocco alikuwa mtu sahihi kwa sababu ya kimo chake ndio maana tulitaka sana kutumia mipira ya krosi kwa sababu Coastal Union tulishawaona ni dhaifu sana kwenye eneo hilo, licha ya yote hayo ila nikiri pia wazi hatukucheza vizuri,” alisema.

Katika mchezo huo, mabao ya Coastal Union yalifungwa na Bakari Selemani dakika ya 26 na Maabad Maulid dakika ya 68, huku lile la kufutia machozi kwa upande wa JKT Tanzania likiwekwa kimiani na beki wa kati, Lameck Lawi aliyejifunga mwenyewe.

Bocco aliyejiunga na kikosi hicho msimu huu akitokea Simba aliyoitumikia kwa misimu saba tangu 2017-2018, amefunga mabao mawili ya Ligi Kuu Bara na timu hiyo, huku nyota huyo akishikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara.

Mshambuliaji huyo amefunga jumla ya mabao 156, ya Ligi Kuu Bara ambapo alianza kuifungia Azam FC aliyoitumia kwa misimu tisa kuanzia 2008 hadi 2017, mabao 84, huku Simba akiifungia 70, wakati kikosi hicho cha Maafande amekifungia mawili tu.
Bocco ni miongoni mwa wachezaji watakaobaki katika historia ya Azam FC kwani alichangia timu hiyo kupanda rasmi Ligi Kuu Bara mwaka 2008, baada ya kuifunga Majimaji ya Songea kwa mabao 2-0 kwenye Ligi ya Taifa 2007, Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Timu hiyo ilianza kwa kutoka suluhu na Mbagala Market, ikaifumua Kijiweni mabao 3-0, kisha ikakutana na Majimaji katika mechi iliyopigwa Julai 27, 2007 huku mabao yote mawili yakiwekwa kimiani na mshambuliaji huyo tishio kikosini humo msimu huo.

Bocco kabla ya kujiunga na Azam, alikuwa akiichezea Cosmopolitan katika Ligi ya Mkoa wa Dar es Salaam na kiwango bora alichokuwa nacho msimu huo kiliwavutia mabosi wa matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam waliomsajili kuwaongezea nguvu.

Katika misimu tisa ya nyota huyo, moja kati ya jambo ambalo ni la kukumbukwa ndani ya kikosi cha Azam ni kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya kwanza msimu wa 2013-2014 ikiwa ndio mara ya kwanza kwao na hadi leo wamekuwa wakiuota tu.
Mbali na ubingwa huo na mingineyo ambayo amechukua, ila amewahi pia kuibuka mfungaji bora akiwa na timu hiyo wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011-2012, alipofunga jumla ya mabao 19, ikiwa ni rekodi iliyodumu misimu 12 hadi kufikiwa msimu uliopita.

Mabao 19 ya nyota huyo yalidumu kwa muda mrefu bila kufikiwa au kuvunjwa na mchezaji yoyote ndani ya kikosi hicho hadi ilipotokea msimu uliopita baada ya kufikiwa na kiungo mshambuliaji, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga idadi kama hiyo.
Kiwango bora alichokionyesha ndicho kilichowavutia mabosi wa Simba kumsajili msimu wa 2017-2018 akiwa sambamba na nyota wengine wakiwemo kipa, Aishi Manula na beki wa kulia, Shomari Kapombe na kiungo kiraka, Erasto Nyoni aliyepo Namungo kwa sasa.

Katika misimu saba Bocco akiwa na kikosi cha Msimbazi, amenyakua mataji manne ya Ligi Kuu Bara mfululizo baada ya kusota miaka mitano, Kombe la FA mara mbili, Ngao ya Jamii mara nne, Kombe la Mapinduzi na Kombe la Muungano mara moja moja.

Mbali na hilo, ila ameibuka pia mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021 akiwa na kikosi hicho akifunga jumla ya mabao 16, akimpiku dakika za mwishoni aliyekuwa mshambuliaji mwenzake wa timu hiyo, Chris Mugalu aliyemaliza na 15.

Bocco ndiye aliyevunja rekodi ya kutupia mabao mengi iliyokuwa inashikiliwa na Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyetamba na timu za Bandari Mtwara, Yanga, Simba, Mmbanga na Twiga Sports katika Ligi Kuu kwani alikuwa amefunga jumla ya mabao 153.

Related Posts