M23 wana ushawishi halisi au bandia Goma?

Dar es Salaam. Wakati juhudi za kutafuta suluhu ya vita kati ya Muungano wa makundi ya wapiganaji (Alliance Fleuve Congo-AFC/M23) dhidi ya Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zikiendelea, makundi hayo yameonekana kuwa na ushawishi mkubwa Mashariki ya nchi hiyo.

Kundi la M23 lililoanzishwa Machi 2009 baada ya kuvunjika kwa mazungumzo kati ya makundi ya waasi na Serikali ya DRC, limekuwa kama moto usiozimika kaskazini mwa nchi hiyo.

Kundi hilo limeibuka upya mwaka huu na kuanzisha mapigano na hatimaye kuteka miji Mashariki ya DRC.

Baada ya kuteka mji wa Goma ambao ndio mkubwa eneo hilo, kundi hilo likajitapa kwamba sasa linajipanga kwenda hadi Kinshasa, yaani kupindua Serikali.

Katika maeneo hayo, waasi hao wamefanya mikutano mikubwa hadi kusimika uongozi wao.

Kwa upande mwingine, jeshi la Serikali ya DRC, FARDC linapigana pamoja na washirika yakiwamo majeshi ya Sadc kutoka nchi za Afrika Kusini, Tanzania and Malawi, huku pia kukiwa na madai ya mamluki na wananchi wazalendo.

Februari 6, 2025, muungano wa makundi hayo ulifanya mkutano mkubwa wa hadhara, kwenye Uwanja wa Unity.

Maelfu ya wananchi walijitokeza uwanajani hapo kuonyesha kuwa makundi hayo yanaungwa mkono na watu wengi.

Mwandishi wa habari aliyeko Bukavu nchini DRC ambaye ameomba asitajwe jina lake, ameeleza kuwa ushawishi huo na sura mbili; kwanza ni mshangao wa wananchi wakitaka kujua baada ya kutekwa kwa miji nini kitafuata, pili, wengi wana hofu kutokana na vitisho vya askari wa M23.

“Sio kwamba wanafurahia sana M23, bali wamekuwa na mshtuko wa vita sasa wanataka kuona niki kitaendelea baada ya hapo.

“Hapo awali, wanajeshi wa M23 walipita nyumba kwa nyumba kutangaza huo mkutano na wakasema mtu ambaye hatafika watamfuatilia, hivyo wengi wamehofia kufuatiliwa,” amesema.

Katika mkutano huo, M23 walimtangaza Bahati Musanga Joseph kuwa gavana wa Jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC.

Mwandishi huyo pia ameeleza sababu za jeshi la Serikali, FARDC na washirika wake, kushindwa kufua dafu kwa M23 na wenzake.

“Kwanza kuna madai kuwa M23 wanaungwa mkono na Rwanda, kwa hiyo wao wanapelekwa tu mbele, lakini kazi kubwa inafanywa na majeshi mengine nyuma yake.

“Pili, M23 wanatumia vifaa vya kisasa zikiwamo drones (ndege zisizo na rubani) kufanya upelelezi kabla ya kuanza kushambulia, hivyo wanaweza kufanya mashambulizi ya kumshtukiza adui,” amesema.

Mwanahabari huyo pia anataja muundo wa jeshi la FARDC lililogawanyika kuwa ni sababu moja wapi ya kushindwa vita.

“Wakati M23 wakiwa pamoja, wenzao wamegawanyika katika vikosi vingi, kiasi kwamba inakuwa vigumu kutoa amri ikapokelewa kwa umoja.

“Kuna kuzidiana pia mbinu za vita, mfano M23 walitangaza kusitisha vita juzi, lakini kesho yake asubuhi tu wakaenda kuteka mji (mji wa Nyabibwe).”

Sababu nyingine zinahusishwa na mataifa makubwa hasa ya Ulaya na Marekani, ambapo mchambuzi wa masuala ya kimataifa, Dennis Konga amesema mataifa hayo yakiamua vita vinakwisha.

“Kwanza tujiulize, nani anafadhili majeshi ya nchi hizo yanayopigana DRC? Kwa kiasi kikubwa nchihiyo zinafadhiliwa na mataifa yanayoendelea na huenda hayatoi ufadhili wa kutosha kwenye majeshi yanayoisaidia DRC.

“Pili, sheria za Umoja wa Mataifa zinazuia majeshi yaliyo chini ya Mpango wa kulinda raia na amani nchini DRC (Monusco) kutumia silaha za kivita, ndio maana majeshi hayo yanashindwa kirahisi na M23,” amesema.

Vita vya ukabila, uchumi?

Wakati awali ilielezwa kuwa M23 wanapigana kutetea haki za Watusi na Banyamulenge walioko Mashariki ya DRC, sura imebadilika na inaonekana vita hiyo inachukua sura ya kiuchumi.

Hata kiongozi wa AFC/M23, Corneille Nangaa si Mtutsi wala Mnyamulenge, bali ni mzaliwa wa jimbo la Orientale linalotambulika kama Haut-Uele Kaskazini ya DRC.

Nangaa aliyezaliwa Julai 9, 1970 alipata elimu ya Chuo Kikuu cha Kinshasa, ambapo alipata shahada ya uchumi na kutumikia mashirika mbalimbali likiwamo Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mwaka 2015 aliteuliwa na Rais mstaafu wa nchi hiyo, Joseph Kabila kuwa rais wa Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) na aliitumikia mpaka mwaka 2021.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2018, yeye ndiye aliyemtangaza Rais Felix Tshisekedi wa UDPS kuwa mshindi wa kiti cha urais, baada ya kupata upinzani mkali kutoka kwa Martin Fayulu wa Muungano wa Lamuka katika Awamu ya kwanza.

Hata hivyo, Tshisekedi aliungana na Emannuel Shadary wa FCC ndipo akapata ushindi.

Katika hali isiyoeleweka, Nangaa aliyemaliza muda wake CENI mwaka 2021, aliibua madai kuwa matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2018 yalikuwa ni ya kupika kutokana na kuwapo kwa makubaliano kati ya Rais Tsishekedi na mtangulizi wake Joseph Kabila, madai ambayo Tsishekedi anayapinga.

Agosti 2023, Nangaa akipanga kushiriki uchaguzi katika ngazo zote, alizundua muungano wa CRA uliohusisha vyama 17 vya sias,a yakiwamo makundi mawili ya waasi.

Hata hivyo, alikumbana na mashtaka ya umma, akituhumiwa kucheza mchezo mchafu wa kura kwenye Uchaguzi Mkuu 2018, hivyo akakimbia nchi kwa madai ya hofu ya usalama wake.

Akichambua sababu za Nangaa kuibukia AFC/M23, mwanahabari huyo anasema ni mbinu inayotumiwa na mataifa yanayopora rasilimali DRC kwa kuwatumia wenyeji.

“Hii ni vita ya kiuchumi na inapiganwa na mataifa mbalimbali, sasa wanataka kutumia mtu ambaye ataficha sura zao, mtu wa kabila la wenyeji.

“Wakati M23 wakihusishwa na Rwanda, wenyewe wanatumia mtu anayeonekana kuwa mwenyeji ili kuficha sura yake,” amesema.

Anasema si tu waasi, bali hata FARDC wamekuwa wakiwatumia makamanda wenye asili ya Watutsi na Banyamulenge.

Anamtaja Kanali Alexis Rugabisha, aliyekuwa Kamanda wa Brigedi ya 12 ya FARDC, ambaye asili yake ni Mnyamulenge.

Kanali Rugabisha ameuawa mwaka huu akiwa mstari wa mbele akipambana na M23.

Mwingine ni Jenerali Pacifique Masunzu aliyeteuliwa kuwa kamanda wa jeshi wa Ukanda wa tatu wa ulinzi, Mashariki ya Congo.

Licha ya nguvu na mbinu walizonazo M23 katika vita hivyo, mwanahabari huyo haoni mpango wao wa kuendeleza vita kwenda Kinshasa.

“Hawana mpango wa kwenda Kinshasa, kama ungekuwepo tungeona dalili. Mwaka 1997 walipompindia Rais Mobutu Seseseko, wananchi wengi walikuwa wamechoka uongozi wake,” amesema.

Related Posts