Maadhimisho ya Kilele cha Wiki ya Anwani za Makazi Dodoma

MAADHIMISHO ya kilele cha wiki ya Anwani za Makazi yamefanyika leo jijini Dodoma, yakiongozwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ambapo ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana tangu kuzinduliwa kwa operesheni ya mfumo wa anwani za makazi na Rais, Samia Suluhu Hassan.

Waziri Mkuu amesema, operesheni hiyo iliyofanyika kwa muda wa miezi minne imewezesha kukusanya taarifa milioni 12.3 za anwani za makazi, ambazo sasa zimehifadhiwa katika mfumo wa kidijitali wa NaPA na kuongeza kuwa mafanikio hayo yameifanya Tanzania kuwa kinara katika utekelezaji wa mfumo huo, huku nchi jirani kama Uganda, Comoro na Eswatini zikileta wataalamu wake nchini kuja kujifunza.

“Mfumo huu ni muhimu kwa wananchi kupata huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na barua za utambulisho ambazo sasa zitapatikana bila kufika kwenye ofisi za Serikali za Mitaa.” amesema Majaliwa .

Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa mfumo huu ni endelevu na unahitaji ushirikiano wa Serikali na wananchi ili kuhakikisha ufanisi wake.

Katika hotuba yake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, ameeleza kuwa kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni “Tambua na Tumia Anwani yako ya Makazi Kurahisisha Utoaji na Upokeaji wa Huduma”. Amesema kuwa lengo la wiki hii ni kuhamasisha wananchi na taasisi kutumia mfumo wa anwani za makazi katika shughuli za kijamii na kiuchumi. Pia, ameeleza kuwa Wizara imeandaa mpango wa miaka miwili wa kuhakikisha waratibu na watendaji wa Mikoa na Halmashauri wanapatiwa vifaa vya kidijitali kama vishikwambi ili kurahisisha kazi zao.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, amesema kuwa mpango wa anwani za makazi umeleta mafanikio makubwa, ikiwemo kuweka vibao vya mitaa na barabara, hivyo kurahisisha usafiri na utoaji wa huduma.

Amesema, Serikali itaendelea kufanya uhakiki wa taarifa na kutoa mafunzo kwa watendaji wa Serikali za Mitaa ili kuimarisha mfumo huu.

Naye, Naibu Waziri wa Ulinzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Nadir Abdulatiff Alwady, amebainisha kuwa Zanzibar imekamilisha uhakiki wa anwani za makazi kwa asilimia 100 katika halmashauri zote 11.

“Mfumo huu utasaidia utoaji wa huduma mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usalama wa wananchi na ulinzi wa miundombinu.” Amesema Alwady

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ameeleza kuwa Mkoa wake umepata minara 36 ya mawasiliano ili kusaidia upatikanaji wa mtandao kwa mfumo wa anwani za makazi na kwamba mkoa umetenga bajeti ya shilingi milioni 300 za kufunga kamera za CCTV kwa ajili ya usalama.

Kwa upande wa Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud, ameshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi.

Amesema kuwa mitaa yote ya Zanzibar sasa ina postikodi na majaribio ya utoaji wa barua za utambulisho kidijitali yameanza katika shehia nne.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, ameeeleza kuwa Bunge litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mfumo wa anwani za makazi unaimarishwa.

Alieleza kuwa Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, hivyo kuwezesha utekelezaji wa mradi huu kwa ufanisi zaidi.

Kwa ujumla, maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi yameonyesha mafanikio makubwa katika kutambua na kusajili anwani za makazi nchini. Serikali imejipanga kuhakikisha mfumo huu unakuwa endelevu kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya taifa.
 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisikiliza maelezo kutoka kwa Postamasta Mkuu Bw. Macrice Mbodo namna Mfumo wa Anwani za Makazi unavyorahisisha huduma za usafirishaji kwa Shirika la Posta Tanzania, wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi, jijini Dodoma.

Aidha, Postamasta mkuu ameelezea namna ambavyo vifaa saidizi vya kidijitali vijulikanavyo kwa jina la (Personal Digital Assistant-PDA) vinavyosaidia utendaji wa Shirika la Posta Tanzania kwa kupokea, kusafirisha na kufikisha taarifa za bidhaa kwa wateja.

Shirika la Posta Tanzania linashiriki Maonesho ya siku tatu ya Wiki ya Anwani za Makazi yaliyoanza Februari 6, 2025 hadi Februari 8, 2025 katika Viwanja vya Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Related Posts