Madiwani Ushetu walalama katikakatika ya umeme

Kahama. Madiwani wa Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga wamembana Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) katika halmashauri hiyo kutokana na kukatika mara kwa mara kwa umeme pasipo taarifa, na kusababisha hasara kwa wananchi.

Wakizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/25 Februai 7, 2025 madiwani hao walisema licha ya umeme kufika kwenye vijiji 112, changamoto ya kukatika mara kwa mara inawaumiza vichwa hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu.

Tanesco imekiri uwepo wa tatizo hilo na kueleza chanzo chake na hatua zinazochukuliwa kutatua tatizo hilo.

Diwani Kata ya Kinamapula, Sharifu Samweli amesema umeme kwenye kata yake umefika, lakini unakatikakatika akimtaka meneja wa shirika hilo kushughulikia changamoto hiyo kwani inawapa hasara wananchi.

“Umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara, ukienda sasa hivi huko mtaani mpaka tunaambiwa Tanesco tumeigeuza kama indiketa za trekta, mpaka inaunguza vifaa vya wananchi.

“Tulitaka tupate majibu kutoka kwa meneja hii hali inasababishwa na nini, hata kama kuna dharura, kwa nini hatupewi taarifa?” amehoji.

Diwani wa Kata ya Ulowa, Gabriella Kimaro amemhoji utaratibu wa wananchi kuunganishiwa umeme, akieleza kwenye kata yake yapo maeneo ambayo nguzo zimepita lakini hakuna umeme.

Diwani wa Kata ya Sabasabini, Emmanuel Makashi ametaka kufahamu utaratibu wa vibarua wanaoajiriwa na mkandarasi anayetekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Amedai amekuwa akiwaajiri lakini wanakopa vitu mbalimbali ikiwemo chakula kwa mamalishe na wanapodaiwa wanasema Serikali haijawalipa, wakiahidi wakilipwa watawalipa lakini hawafanyi hivyo.

Akijibu hoja za madiwani meneja wa shirika hilo Ushetu, George Madaha amesema kukatika kwa umeme mara kwa mara kunatokana na kuzidiwa kwa njia ya umeme inayopeleka nishati eneo hilo kutoka Buzwagi.

Amesema njia hiyo inahudumia maeneo mengi ya nje ya Ushetu, hivyo changamoto inapojitokeza katika maeneo mengine nje ya wilaya inakuwa changamoto kushughulikia kwa wakati.

“Suala la kukatika umeme ni kweli hili lipo lakini tuna changamoto moja kwa halmashauri yetu ya Ushetu, hii ‘line’ yetu ya umeme inayotoka Buzwagi inahudumia Ushetu, baadhi ya maeneo ya Msalala, Kahama Manispaa na baadhi ya maeneo ya Bukombe, kwa hiyo inaweza kutokea changamoto nje ya mipaka yetu ikawa changamoto kulitatua” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ushetu, Gagi Lala amemtaka meneja huyo kufanya utatuzi wa haraka wa hoja za madiwani na yale yote aliyoeleza yatafanyiwa kazi ikiwa ni pamoja na kuongeza kasi ya kupeleka huduma kwa wananchi ili wafaidike.

Hadi Januari, 2025 vijiji 112 vya halmashauri hiyo vimefikiwa na umeme, sawa na asilimia 100 ya utekelezaji wa mradi wa usambazaji wa umeme katika wilaya hiyo.

Related Posts