Mauzo ya mafuta yaongezeka Januari Zanzibar

Unguja. Imeelezwa kuwa, sherehe za miaka 61 ya Mapinduzi, Zanzibar Januari 2025, zimeongeza mauzo ya mafuta visiwani humo kwa kuingiza lita milioni 28 kutokana na uhitaji.

Ofisa mwandamizi wa mafuta na gesi kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (Zura), Ali Abdalla Ali ametoa kauli hiyo leo, Februari 8, 2025, akisema uingizaji wa mafuta kwa Januari umepaa na kufikia lita milioni 28 kiwango ambacho hakijawahi kuingizwa kwa kipindi cha karibuni, huku kukiwa na matumizi ya lita milioni 20.5 kwa mwezi.

Hivi karibuni, Mamlaka ya mapato Zanzibar (ZRA) ilitangaza kuvuka lengo la makusanyo yake kufikia Sh81.512 bilioni kati ya lengo la kukusanya Sh80.984 bilioni, miongoni mwa sababu zilizotajwa kuchochea ufanisi huo ni kutokana na matumizi ya nishati kwa vyombo vya moto kwa kipindi hicho.

 “Ni kweli mafuta yameingia kwa wingi, lita milioni 28 zimeingizwa, kwa kipindi cha karibuni haikuwahi kutokea, mara ya mwisho nakumbuka kwenye Novemba ndio ilifika lita milioni 25 za mafuta,” amesema Ali alipoulizwa swali kuhusu kiasi cha mafuta kilichoingizwa wakati wa kutangaza bei za mafuta katika ofisi za Zura.

Katika kiwango hicho cha mafuta kiliongozwa na mafuta ya ndege yaliyokuwa lita milioni tisa.

Hata hivyo, amesema kwa wastani wa matumizi ya mafuta yote kwa jumla kwa kawaida ni kati ya lita milioni 20 na 21 kwa maana ya petroli ni lita milioni tisa, dizeli lita milioni saba na mafuta ya ndege yanategemeana lakini wastani wa lita milioni nne kwa mwezi kulingana na msimu.

Amesema mafuta ya taa ambayo yanatajwa kutokuwa na matumizi makubwa, zinatumika lita 50,000 kwa mwezi.

Akitangaza bei za nishati hiyo kwa mwezi huu, zitakazoanza kutumika Februari 9, 2025, Kaimu Meneja Kitengo cha Uhusiano Zura, Shara Chande Omar amesema bei za nishati kwa Februari zimeongezeka ikilinganishwa na Januari kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ongezeko la gharama za mafuta katika soko la dunia.

Amesema lita moja ya petroli itauzwa Sh2,819 ikilinganishwa na Sh2,775 ya Januari sawa na ongezeko la asilimia 1.58 huku bei ya dizeli itauzwa Sh2,945 ikilinganishwa na Sh2,892 za Januari sawa na ongezeko la asilimia 1.83.

“Kwa upande wa mafuta ya ndege lita moja itauzwa Sh2,423 ikilinganishwa na Sh2,414 ya mwezi uliopita, sawa na ongezeko la asilimia 0.39 huku mafuta ya taa yataendelea kuuzwa kwa bei ileile Sh3,200,” amesema Shara.

Ametaja sababu nyingine za kuongezeka kwa bei hizo ni pamoja na kuongezeka kwa gharama za uingizaji wa nishati hiyo na kuongezeka kwa wastani wa thamani ya Dola ya Marekani ikilinganishwa na Shilingi ya Tanzania.

Kwa kawaida bei za mafuta hupangwa kuzingatia wastani wa mwenendo wa mabadiliko ya bei za mafuta duniani, gharama za uingizaji katika Bandari ya Tanga, mabadiliko ya fedha za kigeni, usafiri, kodi na tozo za Serikali pamoja na kiwango cha faida kwa wauzaji wa jumla na rejareja.

Related Posts