Bukoba. Upanuzi wa bandari ya Bukoba uliokuwa umesimama kutokana na kukumbwa na changamoto ya mwamba uliobainika chini ya maji katika ziwa Victoria mkoani Kagera, sasa upo katika hali nzuri kufuatia mwamba huo kupasuliwa.
Julai 16, 2024 mkandarasi wa mradi huo, Mhandisi Mnanka Maginga akitoa taarifa, aliwaeleza wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Uhamasishaji Biashara waliokuwa katika ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo, kuwa kuna mwamba chini ya maji unaoitwa Granite Rocks wenye ukubwa wa mita 300.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Februari 8, Ofisa Mfawidhi wa Shirika la Wakala wa meli Tanzania (TASAC) Mkoa wa Kagera, Muzee Mvihanga amesema mpaka sasa upanuzi huo umefikia asilimia 90.

Ameeleza kuwa, ule mwamba uliokuwa umekwamisha wataalamu kuendelea na ujenzi na upanuzi wa Bandari Bukoba tangu mwaka jana, kwa sasa umepasuliwa.
“Ndiyo maana mlikuwa mkisikia ngurumo sana bandarini tangu Januari, ulikuwa ni upasuaji wa ule mwamba uliotukwamisha tangu mwaka jana, hivyo ujenzi unaendelea vizuri na umefikia asilimia 90,” amesema Muzee.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Kagera, Fatma Mwassa amesema Serikali kwa sasa kwenye sekta ya uvuvi na uchukuzi, inaendelea na ujenzi na upanuzi wa miradi miwili ya bandari ya Bukoba na Kemondo.
Amesema kwa bandari ya Bukoba uliofikia asilimia 90 kinachofanyika ni uboreshaji wa magati matatu na jengo la kupokea abiria 350 kwa gharama ya Sh20 bilioni.
Amesema, awali ulitakiwa kukamilika baada ya miezi 20 lakini kutokana na changamoto za mwamba, ndio maana umesogezwa hadi kufikia Machi 2025 uwe umekamilika.
Kuhusu ujenzi wa gati mpya na chumba cha kusubiria abiria kwenye bandari ya meli za mizigo Kemondo na sehemu ya kuegesha magari, amesema umekamilika kwa silimia 100.
Mwassa amesema miradi yote hiyo inagharimu Sh39 bilioni na ikikamilika mkoa unatarajia usafiri wa majini kuongeza mapato kwa meli kubwa kama ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu” kuanza safari zake.