WAKATI Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah akichekelea kuanza kwa kishindo kibarua, winga machachari wa timu hiyo, Beno Ngassa, amesema mechi dhidi ya Simba itakuwa ngumu lakini wanajua pakupenya kupata ushindi.
Josiah aliiongoza Prisons kwa mara ya kwanza akiwa kocha mkuu wa timu ya Ligi Kuu ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa na sasa atakutana na Simba, Februari 11, Dar es Salaa.
Kocha Josiah alisema licha ya kuanza vyema kibarua chake lakini bado inahitajika nguvu ya ziada kujitoa ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kukwepa kushuka daraja.
Alisema anachofanyia kazi ni morali na hamasa kwa wachezaji kuhakikisha kila mechi wanapata pointi tatu ambazo zitawaweka katika mazingira mazuri ya kubaki kwenye ligi.
“Tuna mechi nyingi zimebaki tunakutana na kila aina ya timu, vita yetu ni kila mchezo tupate pointi tatu bila kujali tunacheza na nani au wapi, huu ni wakati wa mashabiki na timu kushikamana,” alisema Josiah.
Kwa upande wake, Ngassa ambaye amekuwa tegemeo kikosini alisema wanafahamu mchezo dhidi ya Simba kuwa mgumu, lakini wameona panapovuja kuweza kupenya kupata pointi tatu.
Alisema wachezaji watatimiza wajibu uwanjani wakisubiri dakika 90 kuamua, akiwatoa hofu mashabiki wao kuwa watarajie mwendelezo mzuri wa timu hiyo. “Mechi itakuwa ngumu kwakuwa wapinzani wametoka kudondosha pointi mbili, sisi tutatimiza wajibu wetu na kusubiri dakiki 90, japokuwa matarajio yetu ni kushinda,” alisema.