Trump asitisha misaada Afrika Kusini, mauaji ya Gaza yatajwa

Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kusitishia misaada Afrika Kusini ikiwa ni mwendelezo wa mvutano kati ya utawala wa Washington dhidi ya Pretoria huku sakata la utwaaji wa ardhi inayomilikiwa na wachache ikitajwa kuwa moja ya sababu.

Katika amri ya utendaji aliyoisaini jana Ijumaa Februari 7, 2025, Trump alisema inalenga kuiwajibisha Mamlaka ya Afrika Kusini kuhusu vitendo vyake vya ukiukwaji wa haki za binadamu vinavyotokana na uamuzi wa Serikali kutwaa ardhi kutoka mikononi mwa tabaka la wachache (Afrikaners) bila fidia.

Sheria hiyo (Expropriation Act) ilipitishwa na kusainiwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

Inaelezwa kuwa, inalenga kuondoa matabaka na kuleta uwiano wa umiliki wa ardhi miongoni mwa raia wa Taifa hilo na wageni.

Hata hivyo, Trump amedai kupitishwa kwa sheria hiyo kunachochea ubaguzi na kusababisha walowezi wanaomiliki sehemu kubwa ya ardhi nchini humo kuporwa ardhi yao.

Katika amri hiyo, Trump amesema Afrika Kusini imekuwa mstari wa mbele kukemea baadhi ya matendo yanayofanywa na Marekani na mataifa rafiki ikiwao Israel ambayo imekuwa ikishutumiwa na Afrika Kusini kutekeleza mauaji ya raia wasio na hatia eneo la Gaza nchini Palestina.

Pia, imesema Afrika Kusini ilishiriki ufunguaji wa kesi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) dhidi ya viongozi wa Israel akiwamo Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi wa Israel (zamani), Yoav Gallants.

Mbali na hilo, Trump katika amri yake hiyo, amesema kitendo cha Afrika Kusini kuimarisha uhusiano na Iran kimemsukuma kusitisha misaada kwa Taifa hilo.

“Marekani haitaendelea kuipatia misaada Serikali ya Afrika Kusini kutokana na kuendesha shughuli mbalimbali zinazokiuka haki za binadamu ndani ya nchi na kuminya sera za nje, kufanya hivyo ni kutishia usalama wa wetu (Marekani), marafiki zetu na masilahi yetu,” amesema Trump kupitia amri hiyo.

Amri hiyo pia, imesema uongozi wa Trump utahimiza ulinzi dhidi ya walowezi waliopo Afrika Kusini (Afrikaners) dhidi ya mpango wa Serikali wa kuwanyang’anya ardhi anaouhusisha na ubaguzi.

Trump na Ramaphosa, wamekuwa wakirushiana maneno juu ya sheria hiyo iliyopitishwa katika Bunge na kusainiwa na Rais wa Taifa hilo, sheria ambayo Trump amedai itachochea utwaaji wa ardhi kutoka tabaka la watu fulani nchini humo.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio ametangaza Jumatano hatohudhuria Mkutano wa G20 (mataifa 20 yenye nguvu duniani) kwa kile alichodai ni kupingana na matendo mabaya yanayofanywa Afrika Kusini.

Ramaphosa amekuwa akisisitiza kuwa, sheria hiyo hailengi kutwaa ardhi badala yake ni utekelezaji wa mchakato wa kawaida wa utengenezaji wa sheria katika nchi yoyote ulimwenguni na kwamba, inalenga kuimarisha usimamizi wa ardhi.

Awali, Shirika la Reuters lililiropoti kuwa, Ramaphosa akitoa hotuba yake ya mwaka bungeni jijini Cape Town amesema:

“Sasa hivi tunashuhudia kuibuka kwa harakati za utaifa na ulinzi wa nchi. Hiyo ndiyo dunia tuliomo sasa hivi, kuendeleza uchumi ndicho kipaumbele chetu.

“Ila nisisitize, hatutotetereshwa, wala hatutotolewa kwenye reli. Sisi ni wastahimilivu na hatutoruhusu kupelekeshwa. Tutasimama pamoja kama nchi na tutazungumza kwa kauli moja ya kulinda masilahi ya Taifa letu, uhuru wetu na demokrasia iliyotajwa kwenye katiba yetu.”

Baada ya kutamka hivyo kwenye hotuba yake, ukumbi mzima wa Bunge ulimpigia Rais Ramaphosa makofi ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuridhishwa na kupenda namna anavyoshughulikia msukumo kutoka mataifa ya nje.

‘Expropriation Law’ inasemaje?

Sheria hiyo inasema Serikali ya Afrika Kusini itakuwa na mamlaka ya kutwaa ardhi kutoka kwa raia bila fidia pale ambako ardhi hiyo itahitajika kwa masilahi ya umma hasa ardhi hiyo ikiwa haitumiki ama kuendelezwa.

Ramaphosa na chama chake cha African National Congress (ANC) wanasema sheria hiyo inalenga kuondoa matabaka katika umiliki wa ardhi, matabaka wanayodai yalisababishwa na ukoloni huku watu wachache tabaka la watu weupe, ndiyo waliokuwa wanamilikishwa maeneo makubwa.

Hadi sasa Serikali yaijaanza utekelezaji wa sheria hiyo.

Kwa upande wake, Chama cha Democratic Alliance (DA), ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini humo, kimeikosoa vikali sheria hiyo kwa kile inachodai inaenda kuvunja haki ya umiliki wa ardhi nchini humo.

Chama cha DA, ambacho kina uungwaji mkono mkubwa kutoka wa watu wa tabaka la watu weupe, hususan ni Wahindi na waliochanganya rangi (wazungu) kinakanusha kuwa sheria hiyo inaenda kuimarisha usimamizi wa ardhi nchini humo.

Suala la umiliki wa ardhi Afrika Kusini ni pasua kichwa tangu enzi za ukoloni na uwepo wa Sera ya Ubaguzi (Apartheid Policy) iliyokuwepo nchini humo tangu mwaka 1948 hadi 1994.

Japo tabaka la watu weusi linajumuisha asilimia 80 ya raia wote wa Afrika Kusini, lakini wanamiliki asilimia nne tu ya ardhi yote ya Afrika Kusini, iliyosalia inamilikiwa na wageni na mashirika binafsi kwa mujibu wa Ripoti ya Ukaguzi ya Serikali ya mwaka 2017.

Tabaka la watu weupe nchini humo linaunda asilimia saba pekee ya raia wote nchini humo, tabaka hilo limegawanyika katika jamii ya walowezi kutoka Ujerumani/Uholanzi na Uingereza ambao ndiyo wanamiliki robo tatu ya ardhi yote ya Afrika Kusini.

Kwa mujibu wa takwimu za Washington, Marekani ilitumia Dola 440 milioni kufadhili shughuli mbalimbali nchini Afrika Kusini mwaka 2023.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts