Viongozi wa EAC, SADC wazungumzia kutatua mgogoro DRC

Dar es Salaam. Viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) wamezitaka pande zote zinazohusika katika mgogoro unaoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kukubali kushiriki  majadiliano ili kuleta amani ya kudumu nchini humo.

Viongozi hao wamebainisha hayo leo Februari 8, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Pamoja wa Wakuu wa Nchi wa Wanawacha wa EAC na SADC.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali chini ya uenyekiti wa Rais wa Kenya, William Ruto ambaye pia ni mwenyekiti wa EAC na Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa ambaye ni mwenyekiti wa SADC.

Mkutano huo unahudhuriwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame wakati Rais wa DRC, Felix Tshisekedi akishiriki kwa njia ya mtandao, huku akiwakilishwa Waziri Mkuu wake, Judith Tuluka.

Akizungumza wakati akiwakaribisha wageni kwenye mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan amesema DRC bado inakabiliwa na mwendelezo wa migogoro ambayo athari zake zinavuka mipaka yake na kusababisha madhara kwa nchi jirani.

Amesema wiki chache zilizopita, yameshuhudiwa mapigano makali ambayo yamesababisha madhara makubwa kwa maisha ya binadamu, watu kuyakimbia makazi yao na kukosekana kwa usalama, jambo ambalo limeathiri shughuli za kiuchumi na biashara zinazovuka mipaka.

“Kama viongozi wa kanda, historia itatuhukumu kama tutakaa tukitazama hali ikizidi kuwa mbaya kila siku. Nchi zetu zina wajibu wa pamoja kuhakikisha tunatatua changamoto ya usalama iliyopo ambayo imeathiri ustawi wa raia wasio na hatia,” amesema Rais Samia.

Ameongeza kuwa, Tanzania inaguswa na kukosekana kwa usalama mashariki mwa DRC.

Rais Samia amesema mgogoro unaoendelea si tu unaiathiri DRC, lakini pia, unahatarisha juhudi za mara kwa mara za kuleta utengamano wa kikanda.

“Nchi yangu inaunga mkono kwa dhati jitihada za kidiplomasia zinazoendelea kumaliza migogoro mashariki mwa DRC. Kwa hiyo, tunayataka makundi yote yanayohusika katika mgogoro mashariki mwa DRC, kushiriki katika majadiliano ili kuleta ustawi wa watu wake na kuleta amani,” amesema Rais Samia.

Amewataka wakuu wa nchi za EAC na SADC kutafakari nini kinatakiwa kufanyika ili kuja na suluhisho la mzozo DRC.

“Tunatakiwa kuamini kwamba, mkutano huu utakuja na mapendekezo na hatua za kutatua mzozo unaoendelea DRC ili kulinda haki za binadamu,” amesema Rais Samia kwenye mkutano huo wa dharura unaolenga kutatua mzozo mashariki mwa DRC.

Kwa upande wa Rais Ruto, amesema eneo la mashariki mwa DRC limekuwa katika vita kwa miongo miwili sasa na janga hilo limegharimu maisha ya maelfu ya watu na wengine wasio na idadi wakiyakimbia makazi yao, kupoteza mali, jambo lililorudisha nyuma kasi ya maendeleo.

Amesema wamekutana pamoja kutoa kauli kwa pande zinazohusika katika mgogoro huo, kusitisha mara moja uhasama baina yao na kuchukua hatua chanya kuruhusu majadiliano yanayolenga kurejesha amani na usalama.

“Tunasimama pamoja kuzitaka pande zote kusitisha mapigano mara moja hususani M23 kuacha kusonga mbele na vikosi vya DRC kusitisha operesheni zao za kijeshi dhidi ya M23.

“Kusitisha mapigano mara moja ndiyo njia pekee tunaweza kutengeneza masharti muhimu ya majadiliano ya kujenga na utekelezaji wa makubaliano ya amani,” amesema Ruto wakati wa hotuba yake ya ufunguzi.

Amesema kama wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na Umoja wa Mataifa (UN), wanafungwa na kanuni ya uhuru wa nchi na kanuni ya ujirani mwema. Kanuni hizi mbili ni za uhakika wa usalama na amani.

Rais Ruto amesema maisha ya mamilioni ya watu, yanategemea uwezo wao wa kuvuka katika kipindi hiki kigumu kwa busara, akili safi na huruma.

Amesema ni wazi kwamba mapigano DRC yanahusisha makundi mengi ambayo kila moja linapigania masilahi yake.

Rais Ruto amesema ni muhimu kukubali majadiliano katika kutafuta suluhisho la kudumu.

“Mtakubaliana na mimi kwamba, majadiliano siyo dalili ya udhaifu ni ushuhuda wa busara na nguvu yetu ya pamoja, sisi viongozi na jamii kwa jumla. Inaonyesha uwezo wetu wa kutatua matatizo kwa utulivu na kusikilizana, kushauriana hadi tufikie mwafaka bora.

“Hivyo, tunazitaka pande zote kuweka tofauti zao pembeni na kukubali majadiliano ya kujenga yanayolenga kupata suluhisho la kudumu katika mgogoro huo,” amebainisha Rais Ruto.

Kwa upande wake, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amesema mkutano huo wa kanda mbili ni ushuhuda wa dhamira yao  ya kuanzishwa kwa AU, hivyo wanatakiwa kutoka na azimio litakalotatua mzozo wa DRC.

Amesema kuongezeka kwa uhasama na kukosekana kwa usalama Mashariki mwa DRC kuna athari za muda mrefu, siyo tu kwa watu wa DRC bali pia kwa kanda zetu na Bara la Afrika kwa jumla.

“Umoja, mshikamano na uimara wa watu wa Afrika, unatakiwa kuvuka majaribu katika nyakati kama hizi tunazopitia. Tunatakiwa kushikamana kama tulivyokuwa wakati wa harakati za ukombozi wa Afrika kutoka kwa Wakoloni.

“Tuna wajibu wa pamoja kuhakikisha tunatatua changamoto zinazokwamisha kupatikana kwa amani na usalama kwa watu wa Mashariki ya DRC,” amesema Rais Mnangagwa.

Amewataka wakuu hao wa nchi za EAC na SADC kujadili hoja iliyopo mezani kwa uwazi, ukweli na dhamira ya kutafuta suluhisho la kudumu la amani Afrika. Rais Mnangagwa amesisitiza kwamba, masilahi ya watu wa DRC yanatakiwa kuwa kipaumbele katika mjadala huo.

Related Posts