RAUNDI ya 18 ya Ligi Kuu Bara itaanza kesho kwa michezo miwili kupigwa kwenye viwanja viwili, mchezo wa mapema saa 10:00 jioni utapigwa CCM Kirumba mjini Mwanza kati ya Pamba Jiji dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC.
Timu hizo zitakutana zikiwa na morali baada ya kushinda michezo ya mwisho baada ya Pamba kushinda ugenini bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji, huku Azam FC ikiifunga KMC kwa mabao 2-0 ikiwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Pamba iliyorejea Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kusota kwa zaidi ya miaka 23 tangu iliposhuka daraja 2001, itahitaji ushindi ili kuweka matumaini hai ya kubaki katika ligi kufuatia kushinda michezo mitatu, sare sita na kupoteza minane kati ya 17.
Katika michezo 17 iliyocheza timu hiyo iko nafasi ya 14 na pointi 15 ikiwa na wastani wa pointi moja kwa kila mchezo, ambapo ushindi utaisogeza hadi nafasi ya 12 na kuzishusha Tanzania Prisons na Namungo zilizokuwa juu yake.
Changamoto pekee ya kikosi hicho ni kutokuwa na uwiano mzuri kwenye eneo la ulizi na ushambuliaji, kwa sababu hadi sasa imefunga mabao manane ikiwa ndio timu inayoongoza kwa kufunga machache ikifuatiwa na Tanzania Prisons iliyofunga tisa.
Mbali na idadi hiyo ndogo, lakini imeruhusu pia mabao 16 sawa na Mashujaa, huku ikimtegemea nyota mpya raia wa Kenya, Mathew Tegisi Momanyi aliyetokea Shabana FC ambaye mchezo uliopita ndiye aliyeifungia bao la ushindi.
Kwa upande wa Azam FC chini ya Kocha Rachid Taoussi itahitaji kuendeleza wimbi la ushindi, ingawa itaendelea kusalia nafasi ya tatu kwani hata ikishinda itafikisha pointi 42 nyuma ya vinara Yanga wenye 45 na Simba 44.
Ubora wa Azam FC ni eneo la ushambuliaji kwani hadi sasa inashika nafasi ya tatu kwa kufunga idadi kubwa ya mabao (27) ikizidiwa na washindani wake waliopo juu Yanga wanaoongoza na 42, huku Simba ikifuatia kwa kutupia kambani mara 35.
Timu hizo zinakutana huku kukiwa hakuna mbabe kwani mchezo wa raundi ya kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex uliisha kwa suluhu (0-0) Septemba 14, mwaka jana, hivyo kuongeza msisimko baina ya miamba hiyo zitakapokutana kesho.
Akizungumzia mchezoa huo, Kocha Msaidizi wa Pamba, Mathias Wandiba alisema ushindi dhidi ya Dodoma Jiji umewaongezea morali, ilhali Kocha wa Azam FC, Taoussi akisema wachezaji wake wako tayari kwa ajili ya mchezo huo.
NAMUNGO VS DODOMA JIJI
Huu ni mchezo mwingine utakaopigwa kesho kuanzia saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Majaliwa, Lindi na Namungo baada ya kuchapwa mechi ya mwisho kwa mabao 2-1 na Tabora United itajiuliza mbele ya Dodoma Jiji iliyochapwa 1-0 na Pamba FC.
Mchezo huo ni wa kisasi zaidi kwa Namungo ambayo mechi ya raundi ya kwanza zilipokutana kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Septemba 12, mwaka jana ilichapwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na Paul Peter katika dakika ya kwanza.
Ushindi kwa Namungo utakuwa na maana kubwa kwani itasogea kutoka nafasi ya 12 iliyopo sasa na pointi 17 hadi ile ya nane, huku Dodoma Jiji ikiwa itashinda itatoka nafasi ya 10 iliyopo na pointi 19 hadi ya sita.
Matumaini kwa Namungo yanabaki kwa nyota mpya, Ibrahim Joshua aliyejiunga katika dirisha dogo akitokea KenGold aliyoifungia mabao manne katika Ligi Kuu Bara sawa na Peter wa Dodoma Jiji aliyefunga pia manne.
Kocha wa Namungo FC, Juma Mgunda alisema changamoto kubwa anayoendelea kupambana nayo ni eneo la ulinzi, huku upande wa Mecky Maxime wa Dodoma Jiji akiwataka nyota wa kikosi hicho kuongeza umakini hasa katika matumizi ya nafasi.