Dodoma. Wakili Tenzi Nyundulwa aliyekuwa akiomba kibali cha mahakama ili afungue kesi kupinga hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kumruhusu makamu wake, Dk Philip Mpango kuendelea na majukumu yake amekwaa kisiki mahakamani.
Nyandulwa alikuwa akiomba kibali afungue maombi ya mapitio ya mahakama akidai kitendo cha Rais kumruhusu Dk Mpango kuendelea kuhudumu baada ya kupokea barua yake ya kujiuzulu ni kinyume cha Katiba.
Katika uamuzi alioutoa Februari 7, 2025, Jaji Angelo Rumisha wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma amesema mwombaji ameshindwa kutoa taarifa za kutosha kuiwezesha mahakama kujua mzozo unaobishaniwa.
Katika maombi namba 1948 ya 2025, Nyandulwa alikuwa anaiomba mahakama impe kibali kufungua maombi hayo, akidai ofisi ya Makamu wa Rais ilikuwa wazi kulingana na Ibara ya 50(2)(c) ya Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.
Ibara hiyo inasema Makamu wa Rais, atashika kiti hicho kwa miaka mitano tangu alipochaguliwa kuwa Makamu wa Rais hadi atakapojiuzulu wadhifa huo, hivyo kitendo cha Dk Mpango kuwasilisha barua ya kujiuzulu, kunafanya nafasi iwe wazi.
Pia, katika maombi hayo, ameeleza angeiomba mahakama imuamuru Rais Samia kumteua mtu mwingine kushika wadhifa huo kulingana na ibara ya 50(4) na 48(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 pamoja na marekebisho mbalimbali.
Pia angeiomba mahakama itoe amri kumzuia Dk Mpango kuendelea kuhudumu kama Makamu wa Rais na kuendelea kushikilia nafasi ya hiyo mara tu alipowasilisha barua ya kujiuzulu wadhifa kwa Rais.
Katika mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) uliofanyika Dodoma, wakati wa kuchagua mgombea mwenza, Rais Samia alisema Makamu wa Rais alikuwa amekwenda kumuona na kumuomba ampumzishe, hivyo ni lazima wateua mrithi wake.
“(Mpango) ana sababu kadhaa lakini siyo za mahusiano ya kazi. Ana miaka 68 na angependa kuishi zaidi ikiwezekana agonge 90 huko. Aliniambia mama yake aliyemzaa alifika 88 na angependa ampite mama yake kidogo asogee mbele.
“Sasa (akamwambia) hizi pilika mnazoniingiza sitafika huko. Naomba nipumzisheni. Nikambishia-bishia, wiki iliyopita hapa akanikabidhi barua yangu hii. Kama hunijibu kwa mdomo barua yangu hii na barua pia sikumjibu,” alisema.
“Tulipokwenda kuzungumza na kamati kuu nikaieleza hiyo hali na wajumbe wote tukakubaliana tumpumzishe. Lakini nataka niwaambie, mambo makubwa na mafanikio tuliyoyaona ni kwa sababu ya msaada mkubwa wa mbobezi wa uchumi.
“Tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa sana. Nimemtuma sana na wala halalamiki. Kwenye kamati kuu tumekubaliana tumshukuru sana sana kwa kazi anayotufanyia na atakayoendelea kutufanyia mwaka mzima unaokuja lakini bado ana 68 ninaweza kumtumia,” alieleza Rais Samia katika mkutano huo uliofanyika Januari 19, 2025 na ambao ulimchagua Rais Samia kuwa mgombea urais uchaguzi mkuu 2025 na Balozi Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza.
Katika kiapo chake, Nyundulwa amedai Januari 19, 2025 wakati akiangalia matangazo ya moja kwa moja kupitia TBC1, alimsikia Rais Samia akitangaza amepokea barua ya Dk Mpango kuomba kujiuzulu wadhifa wake.
Amedai katika matangazo hayo ya mkutano mkuu maalumu wa CCM, Rais alimtaja Dk Mpango kuwa amemfuata na kumweleza nia yake ya kujiuzulu na alienda mbali na kumkabidhi barua ya kujiuzulu ambayo hata hivyo hajaijibu.
Amedai kitendo cha Rais kukubali kupokea barua ya kujiuzulu kwa Dk Mpango lakini akashindwa kutangaza rasmi kuwa nafasi hiyo iko wazi, imesababisha ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.
Amedai kushindwa huko kuheshimu Katiba ya nchi, kumefanya ofisi ya makamu wa rais kukaliwa na watu ambao uhalali wao wa kisheria una utata.
Amedai kama Mtanzania na wakili, aliona kuwa hilo limemuathiri na anaona anao wajibu wa kiraia na kisheria kuhakikisha kuwa vitendo vyovyote vile vinafuata Katiba na utawala wa sheria ndiyo maana amewasilisha maombi hayo.
Amedai ombi lake lina mashiko kuhusu kujiuzulu kwa makamu wa rais na hiyo hufanyika mara tu Rais anapopokea barua kinyume cha hoja za wadaiwa ambao ni Dk Mpango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Anadai makamu wa rais hakushika ofisi hiyo kwa furaha ya Rais na ana haki ya kujiuzulu wakati wowote, hivyo kuendelea kubakia ofisini ilikuwa kinyume cha Katiba hali inayohitaji mahakama kuingilia kati suala hilo.
Wakili huyo alidai mapitio ya mahakama ndiyo ilikuwa njia pekee ya kusahihisha kosa hilo kwa vile shauri hilo linahusisha kupinga maamuzi ya kiutawala, akisisitiza hakuna kiapo kinzani kimewasilishwa na wajibu maombi.
Katika uamuzi wake, Jaji amesema kupewa kibali siyo jambo la moja kwa moja kwani mahakama itatoa kibali hicho pale tu itakapojiridhisha kuwa imekidhi vigezo vinavyotakiwa na maombi yenye sifa ndiyo huruhusiwa.
“Utaratibu huu unalinda na kuhakikisha kuwa ni shauri tu linalokidhi vigezo ndilo huendelea hatua inayofuata ya mapitio ya mahakama, hii ni ili kuzuia madai ya kipuuzi au yasiyo na uthibitisho kuielemea mahakama,” amesema.
Jaji amesema utaratibu wa mtu kuomba kwanza kibali cha mahakama ili kufungua maombi ya mapitio hufanyika ili kutimiza malengo kadhaa muhimu, nayo ni kuhakikisha maombi yasiyo na mashiko yanachujwa katika hatua za mwanzo.
Katika kesi hiyo, jaji amesema mwombaji amewasilisha hoja kuwa maombi hayo yanajadilika kwa sababu baada ya kujiuzulu, mdaiwa wa kwanza (Dk Mpango), bado ameendelea kuwapo ofisini kinyume cha Katiba.
“Hata hivyo, mwombaji alieleza hajawahi kuiona barua ya Dk Mpango ya kujiuzulu, hivyo hafahamu kama ilianza kutumika (barua) katika tarehe ya baadaye au tayari imeanza kutumika,” amesema jaji akichambua hoja za mwombaji.
“Kwa kweli, hakuna hiyo barua inayodaiwa ya kujiuzulu ambayo iliambatanishwa na maombi haya. Inawezekana ikawa kweli Dk Mpango amejiuzulu. Lakini inawezekana pia tu kwamba ana kusudio la kujiuzulu siku za usoni.
“Kukosekana kwa barua hiyo, itakuwa ni uvumi tu unaoweza kuchukua nafasi. Siku zote kuna hatari ya kucheza kamari. Mchezaji anatazamia kupata zaidi na ushindi ukawa upande wake. Bahati mbaya mahakama haiwezi kucheza kamari. Itakuwa ni majanga na ni hatari kuchukua njia hiyo,” amesema.
“Madhara yake ni makubwa. Bila kuwepo kwa barua ya kujiuzulu au uthibitisho wa wazi, ninaogopa nitashindwa kuamua kama kuna shauri la msingi hapa.
“Kuamua kama shauri hili linajadilika na lina msingi, maombi ni lazima yawe na taarifa za kutosha ili mtu yeyote mwenye busara, hasa ukizingatia asili, malengo na dhamira ya shauri lenyewe na ibainishwe hoja inayobishaniwa,” amesema.
Jaji amesema: “Ni lazima kuwepo nyaraka zenye taarifa mbele ya mahakama ili kuiwezesha kuamua kwa haki. Uvumi hata kama unashawishi namna gani, hauwezi kufikia vigezo vya kesi inayojadilika mbele ya uso wa sheria.”
Kutokana na hoja hizo, jaji ameyatupa maombi hayo akisema ili kuyaruhusu ni lazima kuwepo sababu za msingi na kutokuwepo kwa sababu hizo na mahakama ikayasikiliza na kuamua, ni matumizi mabaya ya mamlaka.