Watoto waliotekwa Mwanza wapatikana | Mwananchi

Mwanza. Wamepatikana. Ndilo neno lenye uzito wa kuelezea taarifa ya Polisi Mkoa wa Mwanza kuhusu kupatikana watoto wawili waliotekwa wakiwa kwenye basi la shule jijini hapa.

Magreth Juma (8) anayesoma darasa la tatu na Fortunata Mwakalebela (5) wa darasa la pili katika Shule ya Blessing Modern iliyopo Nyasaka wilayani Ilemela walitekwa Februari 5, 2025, saa 12:30 asubuhi.

Washukiwa wa utekaji walitekeleza tukio hilo baada ya mmoja wao kuomba lifti kwenye basi la wanafunzi hao kutokea Capri Point jijini Mwanza kuelekea katikati ya jiji kisha kumgeuka dereva na kumwekea kisu shingoni akimtaka asimamishe basi hilo.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi mtekaji aliwabeba watoto hao kimabavu kisha kuteremka nao, huku watuhumiwa wawili waliokuwa na pikipiki (kila mmoja) akitokea mbele ya gari hiyo kisha kuwabeba watoto na kutokomea nao.

Baada ya siku nne za msako, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa leo Februari 8, amesema wamebaini watekaji waliwaficha watoto hao ndani ya nyumba namba nane iliyopo Mtaa wa Nyaburogoya, Kata ya Nyegezi, jijini Mwanza.

“Kwa sababu kila mtaa mkoani Mwanza ulikuwa unafanyiwa doria, askari wetu walifika kwenye nyumba namba 8, Mtaa wa Nyaburogoya leo (Februari 8) saa 6:30 mchana wakapata ushirikiano mzuri wakazingira na kuivamia nyumba.

“Baada ya kugonga milango ya nyumba ambayo tulikuwa na taarifa za kutosha za kikachero kwamba watoto wamo humo ndani, wakatokea watu wawili wenye jinsia ya kiume ambao mikononi walikuwa na mapanga, nondo na jambia,” amesema.

Amesema baada ya kubaini waliogonga mlango ni polisi, watuhumiwa walianza kukabiliana nao wakiwatishia kwa silaha hizo jambo lililowalazimu Polisi kuwarushia risasi za moto na kuwajeruhi.

Amesema walifariki dunia baada ya kujeruhiwa.

“Askari wetu kwa sababu wamefunzwa namna ya kulinda usalama na maisha yao kwanza na wananchi wengine walilazimika kutumia risasi za moto,” amesema.

Amesema Jeshi hilo limechoka kuendelea kusikia vitendo vya uvunjifu wa sheria, ikiwamo utekaji akiwataka wananchi kufika mochwari ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou Toure kutambua miili ya watu hao.

Kamanda Mutafungwa katika taarifa kwa umma siku ya tukio alisema watuhumiwa baada ya kutokomea na watoto hao kusikojulikana walianza kumshurutisha Mkurugenzi wa shule hiyo, Ezekiel Mollel awatumie fedha ili kuwaachia.

Katika uchunguzi wa tukio hilo, Polisi ilimtia mbaroni dereva wa gari hilo na mwalimu mlezi (matroni) wa shule kwa mahojiano na uchunguzi zaidi wa tukio hilo.

Alisema maofisa na makachero wa Jeshi huilo wamesambazwa maeneo yote ya mkoa kwenye vituo vya ukaguzi vinavyopakana na mikoa jirani ili kufanikisha kupatikana kwa watoto huo.

Mkazi wa Nyaburogoya walikofichwa watoto hao, Nina Juma amesema tukio hilo linashtua, akiwataka wazazi kuongeza maombi kwa watoto wao wanapoondoka nyumbani kwenda shuleni.

“Hili tukio ukiliangalia unabaini hawa watu hawakuwa na nia nzuri na watoto hao. Kwa sababu mtu anayejitambua na mwenye nia njema huwezi kumteka mtoto mdogo na kumficha sehemu kama hii,” amesema.

Akizungumza tukio hilo, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke ameitaka jamii kutenda kila jambo kwa hofu ya Mungu, akieleza mtu mwenye hofu ya Mungu ndani yake hawezi kuthubutu kumteka binadamu mwenzake na kumtendea uovu.

Amewashauri viongozi wa dini kuwafundisha waumini masuala yanayoendana na matukio yanayotokea katika jamii ya sasa ikiwemo uhalifu na matukio ya utekaji.

“Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu ni hatua kubwa iliyofanywa na Jeshi la Polisi. Naitaka jamii kuishi kwa kumhofia Mungu na kuamini kwamba ipo siku utaondoka duniani,” amesema.

Askofu wa Kanisa la International Evengelical Tanzania, David Mabushi amesema tukio hilo ni ishara ya namna roho ya uasi isivyo na huruma, akiwataka wananchi kufanya kazi halali ili kujipatia kipato.

“Kwenye Biblia Yusuph aliuzwa na ndugu zake, kwa hiyo matukio kama haya yanaashiria roho ya uasi ambayo haina huruma kwa sababu kama watu waliweza kumuuza ndugu yao kwa sababu inaonekana walilenga kupata fedha. Watu tumrudie Mungu na kutafuta kipato halali,” amesema.

Related Posts