Waziri, Idara ya Uhamiaji waitwa kortini sakata la uraia wachezaji SBS

Kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na Wakili Peter Madeleka akihoji wachezaji nyota watatu wa timu ya Singida Black Star (SBS), kupewa uraia imepangwa kutajwa kwa mara ya kwanza wiki ijayo katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dodoma.

Kwa mujibu wa hati za kuitwa shaurini (samansi) zilizotolewa na ofisi ya Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, wadaiwa wote katika shauri hilo namba 2729/2025 wametakiwa kufika mbele ya Jaji Evaristo Longopa, Februari 14, 2025 saa 3:00 asubuhi.

“Unajulishwa kuwa kesi tajwa imepangwa kutajwa kwa ajili ya amri mbalimbali Februari 14, 2025 mbele ya Jaji Longopa. Unatakiwa kufika mbele ya mahakama bila kukosa na utoe nyaraka zote unazotarajia kuzitumia,” inasema hati ya wito.

Shauri hilo la kikatiba ni dhidi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kama mdaiwa wa kwanza, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji (CGI) mdaiwa wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiunganishwa kama mdaiwa wa tatu.

Wadaiwa wengine ni wachezaji hao watatu, Emmanuel Keyekeh ambaye ni raia wa Ghana, Josephat Bada wa (Ivory Coast) na Muhamed Camara (Guinea). Pia wamo, Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mkurugenzi wa Huduma za Uhamiaji.

Taarifa za raia hao wa kigeni kupewa uraia zilianza kujadiliwa katika mitandao ya kijamii na baadaye kuchapishwa katika vyombo vya habari ndipo Januari 23, 2025 Idara ya Uhamiaji ikajitokeza hadharani na kuthibitisha ukweli wa jambo hilo.

Katika taarifa yake kwa umma iliyotiwa saini na Mrakibu Mwandamizi wa Uhamiaji (SSI), Paul Msele ilisema wachezaji hao waliomba na kupewa uraia chini ya vifungu namba 9 na 23 vya Sheria ya Uraia wa Tanzania, sura ya 357.

Katika kesi hiyo iliyofunguliwa na Madeleka akiwakilishwa na wakili John Seka, anadai kati ya Juni 24 na Januari 23, 2025, wachezaji hao wakiwa raia wa kigeni, waliwasilisha kwa CGI na mkurugenzi huduma za uhamiaji, ombi la kupatia uraia.

Ili kuunga mkono maombi yao, wachezaji hao ambao ni wadaiwa namba 4,5 na 6 waliwasilisha hati zao za kusafiria na vibali vya kufanya kazi nchini kwa ajili ya kupitiwa na kuhakikiwa na CGI na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji.

Baada ya kupitiwa, katika taarifa isiyofahamika, anadai waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ni mdaiwa wa kwanza, CGI na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji waliyakubali maombi ya wachezaji hao na kupewa uraia wa Tanzania kwa Tajnisi.

Wakili Madeleka anadai wadaiwa walipopelekewa nyaraka kwa ajili ya uhakiki, walipaswa wazingatie kuwa wachezaji hao hawakuwa wameishi nchini mfululizo kwa kipindi cha miezi 12 kabla ya siku ya kuwasilisha maombi yao.

Kwamba waziri, CGI na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji hafahamu kuwa wachezaji hao hawakuwa wameishi nchini katika kipindi cha miaka isiyopungua saba lakini pia hawana ufahamu wa kutosha wa lugha ya Kiswahili au Kiingereza.

Madeleka anadai maombi ya wachezaji hao hayakuchapishwa katika gazeti linalosomwa zaidi na taarifa walizoziwasilisha uhamiaji zina maudhui ya uongo au ya kutia shaka.

Anadai licha ya dosari hizo, waziri wa Mambo ya Ndani aliidhinisha wapewe uraia na kwamba, tangazo la Idara ya Uhamiaji lilitaka kuonyesha kuwa waziri ana kinga ya kutoheshimu Katiba na sheria za nchi.

Amedai DPP ana mamlaka ya kikatiba na kisheria ya kuanzisha uchunguzi kubaini viashiria vyovyote vya jinai katika kupata au kushughulikia wachezaji hao kupata uraia wa Tanzania licha ya dosari ambazo anadai zilikuwa za wazi.

Madeleka anadai AG kama mshauri mkuu wa sheria wa Serikali ana mamlaka ya kuishauri Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na hata Rais, kuchunguza kama kulikuwa na njama za kufanikisha suala hilo.

Madeleka anaiomba mahakama itamke kuwa kinga aliyopewa waziri wa Mambo ya Ndani kupitia kifungu cha 23 cha sheria ya uraia, hakiendi mbali na kufikia hatua ya kukiuka Katiba na kifungu cha 9 cha sheria ya uraia.

Anaiomba mahakama itamke kwa kupendekeza wachezaji hao wapewe uraia, CGI na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji, walikiuka Katiba ya nchi na sheria ya uraia.

Oia anaiomba mahakama itamke kwa kuwapa uraia wachezaji hao ambao ni wadaiwa wa 4,5 na 6, waziri wa Mambo ya Ndani alikiuka ibara ya 26(2) ya Katiba ya nchi na kifungu cha 9(1) cha Sheria ya Uraia Tanzania.

Madeleka anaiomba mahakama itamke kuwa wachezaji hao hawana sifa ya kupewa uraia na kwamba, waziri wa Mambo ya Ndani, CGI na wachezaji hao kwa pamoja walishiriki kugushi au kutoa uraia katika mazingira yasiyokubalika.

Anaiomba mahakama itoe amri kwa Waziri wa Mambo ya Ndani na CGI kutaifisha mara moja vyeti vya uraia walivyopewa wachezaji hao na kuwaamuru kusalimisha vyeti hivyo kwa msajili wa mahakama wakati hukumu ikisubiriwa.

Anaiomba mahakama imwamuru AG kama mshauri mkuu wa Serikali, kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha ‘kumulikwa’ kwa waziri wa mambo ya ndani, CGI na mkurugenzi wa uhamiaji na walio chini yao.

Wakili huyo anaiomba mahakama kumwagiza DPP kuanzisha uchunguzi kuhusu vitendo na ushiriki wa waziri wa Mambo ya Ndani, CGI, wachezaji hao na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji kuona kama jinai yoyote ilitendeka na kuchukua hatua.

Madeleka anaiomba mahakama itoe amri kwa waziri, CGI na mkurugenzi wa huduma za uhamiaji kulipa Sh500 milioni kama fidia ya adhabu kwa matendo yao ambayo hayakuzingatia Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977.

Pia anaomba mahakama iwaamuru wachezaji hao kulipa Sh200 milioni kama fidia ya adhabu ya kufanya matendo yanayokiuka Katiba, wadaiwa walipe gharama za kesi na mahakama itoe amri yoyote inayoona inafaa.

Related Posts