ANTI BETTY: Mume wangu hataki nijipodoe siku hizi

Anti nimeolewa, tena na mwanamume niliyempenda kwa dhati na niliyembadili kutoka kuvaa kawaida hadi kuwa mtanashati anayevutia.

Pia wakati tunakutana nilikuwa ninajipenda na alikuwa kila mara akiniambia unajipenda mpaka unakera.

Cha ajabu tangu anioe amekuwa na tabia nisiyoielewa kabisa, kwanza alitupa vipodozi vyangu nikajua hapendi ning’ae kwa sababu baadhi vilikuwa vikining’arisha kwa mbali.

Nilishangaa alipotupa wanja na rangi ya mdomo. Sasa ameweka bayana kabisa hataki nijipodoe, nisivae vizuri nikiwa peke yangu, nikitaka afurahi anikute vimevaa kanga au kitenge kutwa nzima. Nikivaa vinginevyo nakuwa adui, anaweza asile wala kulala pamoja nami.

Kabla sijadai talaka maana siyo vitu nilivyozoea, naomba unipe ushauri nifanyeje?

Katika maisha ya ndoa, mara nyingi wanandoa wanakutana na changamoto mbalimbali zinazohusiana na mitazamo na tabia za kila mmoja.

Inaonekana wazi mumeo hataki kukupa uhuru wa kufanya kinachokupa furaha, badala yake anaingilia kila unachokifanya.

Hali hii inaweza kukufanya ujichukie, kwani umeshazoea kujipenda, hivyo ni muhimu kulimaliza suala hilo kwa busara.

Muhimu kwanza kujua kwa nini hataki ujipende, inawezekana ana mtazamo hasi kutokana na kusikia maneno fulani kuhusu wanawake wanaojipodoa.

Pia inaweza kuwa ni tabia yake ya mfumo dume ambayo kwa kawaida inaweza kuwa ndivyo alivyolelewa kuwa mwanamke anapaswa kumtii mume kwa kila kitu, hata namna ya kutunza mwili wake.

Ukijua nini kinamsukuma kuchukua uamuzi huo ilhali alikukuta ukijipenda na kujipodoa itakuwa rahisi kulimaliza suala hilo.

Kudai talaka ili muachane siyo suluhisho, muhimu kutafuta suluhu kwa amani na busara.

Mbali ya hayo niliyoyasema, wivu pia unaweza kuwa sababu ya hayo, kwani anaona ukijipamba utapendwa na wengi na utamuacha.

Sasa kwa sababu ndoa ni pamoja na kujitolea na kuheshimiana, hupaswi kuwa na haraka ya kufanya maamuzi.

Nakushauri ukishajua au kuhisi kinachomsukuma mumeo kukukataza kujiremba utakuwa umepata pa kuanzia. Ukikosa hilo pia si mbaya.

Kabla hujazungumza naye kuhusu kukuruhusu kujipenda na kukuwezesha kufanya hivyo, anza kujipodoa akiwa amerudi, tena ikiwezekana mbele yake kwa kuwa itakuwa ni jioni au usiku ametoka kibaruani, bila shaka mtaishia kulala.

Hapo utakuwa unaweka akiba ya ushahidi siku utakayozungumza naye kuwa kujipenda kwako hakuna uhusiano na kumuonyesha yeyote, bali ni mapenzi yako tu.

Ukipata wasaa wa kuzungumza naye mwonyeshe mumeo kwamba kujipamba hakumaanishi kuwa anataka kuvutia wanaume wengine.

Tena msisitize umuhimu wa kujipodoa kwa maana ya kujipenda na faida zake ikiwamo afya yake ya kiakili na kihisia, kwani huwasaidia wanawake kujiamini na kujiweka katika hali nzuri.

Mweleze kuwa kujipenda kunaweza pia kuwa na faida katika kufanikisha uhusiano mzuri kati yao, kwani mke mwenye furaha na kujiamini anaweza kuwa na mchango mkubwa katika ndoa.

Mazungumzo ya wanandoa ndiyo hulinda ndoa na yanaweza kuleta suluhu ya suala hilo.

Katika mazungumzo yenu usisahau kumkumbusha kuwa alikukuta unajipamba na kujipodoa, hivyo ni tabia yako na hufanyi hivyo kwa kujionyesha au kuvutia watu.

Muhimu kumshawishi akuelewe kwa taratibu na busara, kwani kama amekulia kwenye mfumo dume wa mwanamke kutakiwa kuwa wa kawaida na wa kusikiliza maelekezo tu, itamchukua muda kukuelewa. Ila naamini kwa mazungumzo baina yenu wawili atakuelewa

Related Posts