Banduka atakumbukwa kwa kuanzisha CCM, sakata lake na Mwaibabile

Dar es Salaam. Mmoja wa wajumbe wa Tume ya watu 20 walioandaa kuanzisha Chama cha Mapinduzi (CCM) wakati wa kuunganisha vyama vya Tanganyika African National Union (Tanu) na Afro-Shirazi Party (ASP), Nicodemus Banduka (80), amefariki dunia.

Banduka, aliyekuwa kada wa Tanu na baadaye CCM, amefariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mloganzila.

Mbali na kuwa mjumbe kutoka Tanu aliyeshiriki kuandika katiba ya chama kipya cha CCM, pia aliwahi kuwa mkuu wa mkoa katika mikoa kadhaa ikiwemo Ruvuma, Pwani, na Lindi. Ndani ya CCM, aliwahi kuwa Katibu wa CCM Mkoa wa Kagera.

Kumbukumbu kuu za Banduka ziko katika maeneo mawili—ndani ya chama na serikalini. Akiwa serikalini kama mkuu wa mkoa, hakuwa mtu wa mchezo; alisimamia kile alichoamini.

Banduka alikuwa miongoni mwa wajumbe 10 wa Tanu, ambapo mwenyekiti wao alikuwa Peter Kisumo, na wajumbe 10 kutoka ASP, mwenyekiti wao akiwa Sheikh Thabit Kombo, walioteuliwa kuunganisha vyama hivyo.

Tume hiyo ya watu 20 ilipewa jukumu la kuandaa chama kipya cha CCM, ikiwemo kuandaa katiba, bendera, rangi ya chama (kijani), na nembo ya jembe na nyundo.

CCM ilipotimiza miaka 43 tangu kuzaliwa kwake Februari 5, 1977, Msekwa alizungumza na gazeti hili kuhusu historia ya kuanzishwa kwake, ikiwemo wajumbe wa tume hiyo.

Wajumbe wa ASP walikuwa Thabit Kombo (mwenyekiti), Ali Mzee (katibu), Abdalla Natepe, Seif Bakari, Hamisi Hemed, Rajab Kheri, Asia Amour, Hassan Moyo, Juma Salum, na Hamdan Muhiddin.

Kutoka Tanu walikuwa Peter Kisumo (mwenyekiti), Pius Msekwa (katibu), Daudi Mwakawago, Kingunge Ngombale-Mwiru, Jackson Kaaya, Peter Siyovelwa, Nicodemus Banduka, Lawi Sijaona, Beatrice Mhango, na Basheikh Mikidadi.

Banduka atakumbukwa kwa kushiriki kuanzisha CCM, ambayo sasa imetimiza miaka 48. Ni miongoni mwa wale waliovunja rasmi vyama vya Tanu na ASP ili kuunda CCM.

Kwa mujibu wa Msekwa, tendo la kuvunjwa kwa vyama hivyo lilikuwa la kihistoria kwa lengo la kuendeleza utamaduni wa kuunganisha nguvu katika mapambano. Kwa mfano, ASP kwa upande wa Zanzibar, ilitokana na kuungana kwa African Association (AA) na Shirazi Association (SA), jambo lililounganisha nguvu za wanyonge katika mapambano dhidi ya usultani na utawala wa kikoloni wa Kiingereza.

Kwa upande wa Tanzania Bara, Tanu ilitokana na mabadiliko ya Tanganyika African Association (Taa), kutoka jumuiya ya kutetea maslahi ya kijamii na kuwa chama cha siasa.

Sakata la Banduka na Mwaibabile

Banduka pia atakumbukwa katika tasnia ya habari kwa sakata lake na mwandishi wa habari wa Mkoa wa Ruvuma, Adam Mwaibabile (marehemu).

Mwaibabile, maarufu ‘Mwana’, alikuwa mwandishi wa habari wa kujitegemea kutoka Ruvuma, lakini aliwahi kuhukumiwa kifungo jela baada ya kushtakiwa na Serikali ya mkoa, iliyokuwa ikiongozwa na Banduka, kwa kukutwa na nyaraka za Serikali zenye muhuri wa ‘Siri’.

Mwaibabile, aliyefariki dunia Januari 2007 na kuzikwa katika Makaburi ya Mianzini, Nzovwe, jijini Mbeya, hukumu yake ya kifungo jela iliwaibua wanaharakati wengi waliodai kuwa alifungwa kwa kuonewa.

Hadi Mwaibabile anakutwa na umauti, sakata lake na Banduka liliendelea kubaki katika nyaraka mbalimbali, hasa pale inapozungumziwa masuala ya uhuru wa habari.

Taarifa za familia ya Banduka zinaeleza kuwa alifariki dunia Ijumaa jioni, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mloganzila.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake, Kibaha kwa Matias.

Banduka alikuwa mwanasiasa na kiongozi mashuhuri nchini, ndani ya CCM na serikalini.

Related Posts