Hamdi amtisha Fadlu, awapa neno mastaa Yanga mtihani uko hapa!

KITENDO cha Kocha Miloud Hamdi kukabidhiwa kikosi cha Yanga huku zikipita takribani siku nne pekee, mwenyewe ametoa kauli inayoweza kuwa ni kama tishio kwa watani zao, Simba wanaonolewa na Msauzi, Fadlu Davids.

Kocha huyo mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, ametua Yanga Februari 4, 2025 ikiwa ni muda mfupi baada ya klabu hiyo kuachana na Sead Ramovic aliyetimkia CR Belouizdad ya Algeria.

Miongoni mwa mambo ambayo kocha huyo anataka kuona yakitokea katika kikosi hicho ni kufikia malengo yaliyobaki ikiwa ni kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara na Kombe la FA.

Hamdi (53), amewahi kufundisha soka Ufaransa, Italia, Saudi Arabia, Algeria na Morocco, huku pia kwa mara ya kwanza akitua Tanzania kuifundisha Singida Black Stars iliyomtambulisha Desemba 30, 2024 kabla ya kuibukia Yanga.

Kocha huyo alifichua ameridhishwa na wachezaji aliowakuta anaoamini watamrahisishia kazi yake kwani wanaendana na falsafa yake ya kucheza soka la kushambulia kwa kasi.

Akizungumzia mikakati yake ndani ya Yanga, Hamdi alisema anataka kuhakikisha anaendelea kuwapa furaha Wanayanga kwa kubeba mataji ya ndani ambayo si mageni kwao.

Kitendo cha kusema anataka kutembelea kwenye malengo ya klabu kubeba makombe ya ndani wakati Simba ikiyapigia hesabu pia, inaashiria kocha huyo kuiendeleza vita aliyoiacha Ramovic.

Mbali na mataji ya ndani, kocha huyo alisema anataka kuweka rekodi yake kimataifa kwa kufanya vizuri zaidi kwani ndiyo malengo ya klabu hiyo kwa sasa.

“Naifahamu Yanga kwa sababu imeshiriki mara nyingi michuano ya kimataifa ni nadra kusikia kocha anasema haifahamu hii timu ambayo tayari imevaa medali ya CAF, imetwaa mataji mengi ya ndani makocha wengi wameandika rekodi hivyo kwangu presha kubwa ni kuipambania ifikie malengo kimataifa.

“Naheshimu makocha wote waliopita na walichokifanya, hivyo nitafanya muendelezo huku nikisaka rekodi yangu pia kwa kufanya kilicho bora zaidi, kikubwa ninachojivunia ni kuona wachezaji wengi wanacheza aina ya mfumo ninaoupenda,” alisema.

Aliongeza, juzi alikaa na wachezaji kabla ya kuanza mazoezi na kuweka mikakati ya pamoja kuhakikisha hawaachi nafasi kwa wapinzani kufanya vizuri zaidi yao sambamba na kuwaambia makosa wanayopaswa kuyafanyia kazi kutokana na kile alichokishuhudia walipocheza dhidi ya KenGold.

Ikumbukwe, katika mchezo huo, kipa wa Yanga, Djigui Diarra alifungwa bao la mbali kutokea katikati ya uwanja na Seleman Bwenzi likiwa ni la pekee kwa KenGold huku kocha huyo akiwa jukwaani akishuhudia kila kitu.

“Nilikuwa na kikao na wachezaji wangu juzi kabla ya mazoezi, nimezungumza nao nini nataka na nimewaambia wapi walikuwa na mapungufu, tumeelewana, kilichobaki ni kufanya kazi vizuri.

“Kwa sasa hakuna muda wa kupoteza kwani ukiangalia ratiba kwa mwezi Februari imebabana sana, tuna mechi mfululizo tunazopaswa kucheza.

“Wachezaji wangu wapo timamu hivyo kazi yangu haitakuwa ngumu sana, napambana kuhakikisha nawajenga kiushindani ili kufikia malengo waliyojiwekea mwanzo wa msimu kutetea mataji,” alibainisha kocha huyo.

Alisema anafurahi kuifundisha timu ambayo ipo kwenye ubora mkubwa na aina ya wachezaji waliopo ndani ya timu kwa upande wake anaamini ni muda sahihi kuipata nafasi aliyopewa atapambana kuhakikisha anaendelea kuipaisha timu hiyo kuendelea kuwa bora kwa kushinda mataji kimataifa.

“Hakuna kinachoshindikana, Yanga ina wachezaji wengi bora na wenye uzoefu mkubwa, mbinu imara itakuwa chachu ya wao kuisaidia timu kufikia malengo, naamini uwekezaji mkubwa uliopo na ushirikiano mzuri na viongozi hakuna kitakachoshindikana,” alimaliza kocha huyo.

Kwa sasa Yanga wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha pointi 45, moja zaidi ya Simba iliyopo nafasi ya pili huku zote zikicheza mechi 17.

Pia timu hiyo ipo hatua ya 32 bora katika Kombe la FA wakiwa ni mabingwa watetezi.

Kwa sasa Yanga ipo kwenye maandalizi chini ya Hamdi ikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya JKT Tanzania utakaopigwa kesho Jumatatu kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar.

Ili kufanikisha hayo yote ya kutetea ubingwa na kuendelea kuwapa furaha Wanayanga, kwanza Kocha Hamdi ana kazi kubwa ya kufanya katika mechi 10 zijazo kuhakikisha haangushi pointi yoyote.

Hiyo itamsaidia katika hesabu zake za ubingwa katika mechi 13 zilizobaki zenye jumla ya pointi 39.

Ukiangalia mechi kumi zijazo kati ya hizo 13 zilizobaki kabla ya kumaliza msimu huu, Yanga itakutana na Simba na Azam.

Simba na Azam ndiyo wapinzani wakubwa wa Yanga katika kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwani ndani ya kipindi cha kuanzia mwaka 2001 hadi 2024, timu hizo zimebadilishana taji huku msimamo wa sasa ukionyesha Yanga imeiacha Azam iliyo nafasi ya tatu kwa pointi sita. Pia imeiacha Simba pointi moja ikiwa nafasi ya pili.

Katika kipindi hicho cha miaka 24, Azam imechukua ubingwa mara moja msimu wa 2013-2014 wakati Simba ikibeba mara 10 na Yanga 13.

Pia itacheza dhidi ya Singida Black Stars, timu inayopambana kumaliza nafasi nne za juu kwenye msimamo.

Mechi kumi zijazo za Yanga ni dhidi ya JKT Tanzania (Februari 10, Dar), KMC (Februari 14, Dar), Singida Black Stars (Februari 17, Dar), Mashujaa (Februari 23, Kigoma), Pamba Jiji (Februari 28, Mwanza), Simba (Machi 8, Dar), Tabora United (Aprili 1, Tabora), Coastal Union (Aprili 7, Dar), Azam (Aprili 10, Dar) na Fountain Gate (Aprili 20, Manyara). Baada ya hapo, itacheza dhidi ya Namungo (Mei 13, Dar), Tanzania Prisons (Mei 21, Mbeya) na Dodoma Jiji (Mei 25, Dar).

Related Posts