Leo Jumapili Februari 9, 2025 Namibia, Afrika na dunia kwa ujumla imeamka na taarifa mbaya ya kifo cha mwanamema na mwanamajumui mashuhuli wa Afrika, Sam Nujoma.
Nujoma alipigania uhuru wa Namibia na kufanikiwa kumuondoa mkoloni madarani na kuwa Rais wa kwanza na baba wa Taifa wa Taifa hilo mwaka 1990 hadi 2005.
Jina lake kamili ni Samuel Daniel Shafiishuna Nujoma, mwanzilishi wa Chama cha Swapo kilichoendesha harakati za muda mrefu kudai uhuru, hakumbukwi nchini Namibia pekee kama alama ya ukombozi, bali hata Tanzania jina lake limeacha kumbumbuku.

Barabara inayotoka Mwenge kuanzia kwenye makutano na Barabara ya Bagamoyo hadi Ubungo imepewa jina lake; (Barabara ya Sam Nujoma). Hiyo ni kuenzi harakati zake za kuikomboa Namibia kutoka kwa wakoloni.
Kana kwamba haitoshi, Nujoma aliokolewa na baadhi ya maofisa wa juu wa Chama cha Tanganyika African National Union (Tanu) baada ya kushtukia mpango wa kutaka kukamatwa na maofisa wa utawala wa kikoloni wa Uingereza.
Nujoma alitua kwa ndege Mbeya akitokea Ndola, Zambia na baada ya kushtukia mpango wa kukamatwa alisaidiwa na maofisa wa Tanu kutoroka hospitali akipita Njombe, Iringa, Dodoma hadi Dar es Salaam.
Kwa msaada wa maofisa wa Tanu, Nujoma alifanikiwa kuonana na Mwenyekiti wa Tanu wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere aliyemsaidia kupata hati ya kusafiria (pasi) ili iwe rahisi kwake kufanya harakati za ukombozi.
Nyerere alikuwa msaada mkubwa kwa Nujoma hasa baada ya kumruhusu kuifanya Dar es Salaam kama kituo kikuu cha jeshi la Swapo, nje ya Namibia kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kijeshi.
Nujoma pia aliitumia Tanzania kupitishia silaha kutoka Algeria kwa ajili ya jeshi lake. Silaha hizo kabla ya kupelekwa Omugulugwombashe katika mji wa Ovamboland, Namibia ilipokuwa ngome kuu ya jeshi la Swapo, ziliingia Tanzania zilitoka Algeria kupitia Misri, Sudan kabla ya kupelekwa Zambia zilikochukuliwa hadi Namibia.
Miongoni mwa askari wa Swapo walipatia mafunzo hayo Dar es Salaam ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba, Mzee Kaukungwa na Mose Tjitendero. Mwaka 1965, Umoja wa Nchi Huru za Afrika Afrika (OAU sasa AU) uliitambua rasmi Swapo.
Kabla ya kuingia Ikulu ya Windhoek, Nujoma amepitia shuruba nyingi, huku pia akilazimika kuacha kazi ya kufanya usafi kwenye Shirika la Reli la Afrika Kusini kujitosa kwenye siasa.
Nujoma aliajiriwa kwenye shirika hilo kama mtu wa kufanya usafi, lakini lengo lake halikuwa tu kufanya usafi, bali pia kupata fursa ya kujifunza lugha ya kiingereza.
Kazi hiyo aliifanya sambamba na kuhudhuria elimu ya watu wazima, ambayo masomo yake yalikuwa yakitolewa usiku katika Shule ya Mtakatifu Barnabas ya Kanisa la Anglicana.

Nujoma alizaliwa katika mji wa Etunda, Kijiji cha Ongandjera Mei 12, 1929. Mama yake alijulikana kwa jina la Helvi Mpingana Kondombolo aliyefariki dunia mwaka 2008 akiwa na miaka 110 na baba yake alijulikana kwa jina la Daniel Uutoni Nujoma. Sehemu kubwa ya maisha yake ya utotoni ilikuwa kuchunga mifugo ya familia na kushiriki shughuli za kilimo kutokana na wakati huo kutokuwa na fursa ya elimu. Hata hivyo, alipata bahati ya kusoma shule ya misionari ya Okahao alipokuwa na miaka 10 na kumaliza darasa la sita ikiwa ni elimu ya juu zaidi kufikia na mtoto wa Kiafrika wakati huo. Mwaka 1946, akiwa na miaka 17, alikwenda kuishi na shangazi yake katika mji wa Walvis Bay, ambako alipata kazi aliyofanya kwa miaka mitatu na kisha kurudi Windhoek alikoajiriwa kama mfagizi kwenye Shirika la Reli la Afrika Kusini(SAR).

Nujoma alijitumbukiza kwenye siasa mwanzoni mwa miaka ya 50 kupitia vyama vya wafanyakazi. Uwezo wake kwenye mambo ya siasa ulikuzwa zaidi na uzoefu alioupata kazini ikiwa ni pamoja na uelewa mkubwa wa mikataba ya kazi uliochochewa na harakati za ukombozi.