KAMATI YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII YARIDHISHWA NA UJENZI WA MAKTABA CHUO CHA ARIDHI TABORA

Na Eleuteri Mangi, Tabora

Kamati
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeridhidhwa na ujenzi wa mradi
wa maktaba ya Chuo cha Ardhi Tabora (ARITA) ambao umefikia asilimia 99
na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari 2025.

Akizungumza
wakati wa majumuisho mara baada ya ziara ya kukagua ujenzi wa maktaba
hiyo Februari 8, 2025 mjini Tabora, Mwanyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe.Timotheo Mzava amesema kamati
yake imejionea na kuridhishwa kwa hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa
maktaba hiyo pamoja na maendeleo ya chuo hicho.

“Kwa
ujumla Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii baada kupitia, kukagua,
kupata taarifa na kujionea kwa macho, imeridhishwa na kazi kubwa na
nzuri inayofanywa na uongozi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi pamoja Chuo cha Ardhi Tabora katika kukamilisha jengo hili la
maktaba” amesema Mhe. Mzava.

Aidha,
ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha
Shilingi milioni 500 Septemba 2024 ambayo ilipitishwa na Bunge katika
bajeti ya mwaka 2024/2025 ili kukamilisha ujenzi wa maktaba hiyo na
kuleta tija kwa kuwa utasaidia vijana wanaosoma katika chuo hicho.

Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe.
Geophrey Pinda ameishukuru kamati hiyo ambayo ndiyo yenye dhana ya
kuisimamia, kushauri, kutoa maelekezo mbalimbali na kufuatilia kazi
zinazotekelezwa na wizara hiyo. 

“Wajumbe
wa kamati hii wameridhika na kazi ambayo imefanyika na wanasisitiza
jengo hili lianze kufanyakazi mara moja. Sisi wizara tumeiahidi kamati
kuanzia tarehe 01 Machi, 2025 wanafunzi wataanza kutumia vyumba hivi kwa
ajili ya huduma ya maktaba” amesema Naibu Waziri Pinda.

Akiwakaribisha
wajumbe wa Kamati hiyo mkoani Tabora, Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Paul Chacha
amesema miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa na Serikali katika mkoa
huo na kuihakikishia kamati hiyo kuwa Ofisi yake itahakikisha miradi
yote inakamilika ukiwamo mradi huo wa ujenzi wa maktaba ili kufikia
malengo yaliyokusudiwa.

Akitoa
taarifa kwa kamati hiyo, Mkuu wa Chuo hicho Bw. Jeremiah Minja amesema
maktaba hiyo ilianza kujengwa mwaka 2014 na itakamilika mwezi Februari
2025 ambapo hadi sasa umegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 2.2
za Kitanzania.


 

Related Posts