Kaseke aiua Azam FC jiooni Kirumba

BAO la dakika ya 88 lililofungwa na nyota wa zamani wa Yanga, Deus Kaseke limetosha kuipatia ushindi Pamba Jiji wa 1-0, dhidi ya matajiri wa Jiji la Dar es Salaam Azam FC, katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.

Kaseke aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akiwa mchezaji huru, amepachika bao hilo baada ya kupokea pasi iliyopigwa na mshambuliaji, Abdoulaye Yonta Camara aliyetokea benchi akichukua nafasi ya Habib Kyombo na mfungaji huyo kuzamisha mpira wavuni.

Ushindi huo unakuwa wa pili mfululizo kwa Pamba baada ya mchezo uliopita kuifunga pia bao 1-0, Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, ukiwa ni wa nne katika michezo yake 18, iliyocheza kufuatia kutoa sare sita na kuchapwa minane.

Pamba iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kushuka daraja mwaka 2001, inafikisha pointi zake 18, ikiwa ni wastani wa pointi moja kwa kila mchezo na kuifanya kushika nafasi ya 12 na kuweka matumaini hai ya kubaki.

KAS

Kwa upande wa Azam FC iliyoingia na morali baada ya kushinda michezo mitatu mfululizo ya Ligi Kuu Bara, imepokea kichapo cha tatu msimu huu katika mechi zake 18 ilizocheza hadi sasa, kufuatia kushinda 12, kibindoni na kutoka sare pia mitatu.

Tangu Rachid Taoussi ateuliwe kuiongoza Azam Septemba 7, 2024, akichukua nafasi ya Msenegali Yousouph Dabo aliyetimuliwa Septemba 3, 2024, ameiongoza katika michezo 17 ya Ligi Kuu Bara ambapo ameshinda 12, sare miwili na kupoteza pia mitatu.

Kiujumla Azam imecheza michezo 18, ikishinda 12, sare mitatu na kupoteza mitatu, ikifunga jumla ya mabao 27 na kuruhusu tisa, ikiwa nafasi ya tatu na pointi 39, nyuma ya vinara Yanga inayoongoza na pointi 45, ikifuatiwa na Simba yenye 44.

Related Posts