Kifo cha Nujoma chafunga ukurasa wa kizazi cha viongozi wapigania uhuru

Dar es Salaam. Kizazi cha viongozi wapigania uhuru wa Afrika kimefungwa rasmi kufuatia kifo mwasisi wa Namibia huru, Sam Nujoma.

Nujoma, Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Namibia, amefariki dunia leo, Februari 9, 2025 nchini Namibia akiwa na umri wa miaka 95, na amefunga hesabu ya kizazi cha viongozi wapigania uhuru waliokuwa bado hai barani Afrika.

Viongozi wengine waliopambana kuzitoa nchi zao kwenye makucha ya wakoloni au utawala wa wazungu wachache, akiwamo Mwalimu Nyerere, wametangulia mbele ya haki.

Wengine waliotangulia mbele ya haki ni Nelson Mandela (Afrika Kusini), Robert Mugabe (Zimbabwe), Kenneth Kaunda (Zambia), Samora Machel (Msumbiji), na sasa Sam Nujoma (Namibia).

Nujoma ndiye aliongoza mapambano na kuiwezesha nchi yake kupata uhuru mwaka 1990 kutoka kwenye utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini.

Alikuwa Rais wa kwanza wa Namibia huru na aliiongoza kwa miaka 15; hadi anaondoka madarakani, aliendelea kuwa Baba wa Taifa hilo.

Nujoma ambaye ni mwanzilishi wa chama cha Swapo kilichoendesha harakati za muda mrefu kudai uhuru, jina lake halisi ni Samuel Daniel Shafiishuna Nujoma. Alikuwa Rais wa kwanza wa Namibia kuanzia mwaka 1990 hadi 2005.

Kiongozi huyo hakumbukwi nchini Namibia pekee kama alama ya ukombozi, bali hata Tanzania jina lake limeacha kumbukumbu.

Barabara inayotoka Mwenge kuanzia kwenye makutano na Barabara ya Bagamoyo hadi Ubungo imepewa jina lake: (Barabara ya Sam Nujoma). Hiyo ni kuenzi harakati zake za kuikomboa Namibia kutoka kwa wakoloni.

Mmoja wa watu wanaoielewa vema historia ya jiji la Dar es Salaam, Sheikh Khamis Mataka, amesema awali barabara hiyo ilikuwa ikiitwa Mlimani kabla ya kubadilishwa kuwa Sam Nujoma.

“Eneo lile kwa kuwa lilikuwa la Chuo Kikuu cha Mlimani (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam), hata ile barabara tulikuwa tukiita barabara Mlimani.

“Miaka ya 1980, ndipo barabara hiyo ilipopewa jina la Sam Nujoma. Lengo la Mwalimu (Baba wa Taifa la Tanzania, hayati Julius Kambarage Nyerere) lilikuwa ni kumheshimu kiongozi huyo mkuu wa chama cha Ukombozi Namibia (Chama cha Swapo),” amesema.

Amesema kabla ya kupewa heshima hiyo, Nujoma alikuja Tanzania wakati huo bado hajawa Rais, akiwa yupo kwenye harakati za kudai uhuru, ndipo Mwalimu Nyerere akampa heshima hiyo.

“Mwalimu alikuwa akiwaenzi wapigania uhuru wa Afrika, akiwamo Nujoma. Wakati ule Tanzania ndiyo ilikuwa mwenyekiti wa nchi tano za kupigania uhuru, ikiwamo nchi za Zambia na Msumbiji.

“Kwa heshima ya Nujoma, ndipo Serikali ya Tanzania ikaipa jina lake hiyo barabara,” amesema Sheikh Mataka.

Nujoma aliwahi kusaidiwa na baadhi ya maofisa wa juu wa Tanu baada ya kushtukia mpango wa kutaka kukamatwa na maofisa wa utawala wa kikoloni wa Uingereza.

Nujoma alitua kwa ndege Mbeya akitokea Ndola, Zambia, na baada ya kushtukia mpango wa kukamatwa alisaidiwa na maofisa wa Tanu na kutoroka hospitali akipita Njombe, Iringa, Dodoma hadi Dar es Salaam.

Kwa msaada wa maofisa wa Tanu, Nujoma alifanikiwa kuonana na Rais wa Tanu wakati huo, Mwalimu Nyerere, aliyemsaidia kupata hati ya kusafiria (pasi) ili iwe rahisi kwake kufanya harakati za ukombozi.

Nyerere alimsaidia Nujoma hasa kwa kumruhusu kuitumia Dar es Salaam kama kituo kikuu cha chama cha Swapo, kilichokuwa kikiendesha harakati za ukombozi nje ya Namibia.

Kabla ya kuingia Ikulu ya Windhoek, Nujoma amepitia shuruba nyingi, huku pia akilazimika kuacha kazi ya kufanya usafi kwenye Shirika la Reli la Afrika Kusini na kujitosa kwenye siasa.

Nujoma aliajiriwa kwenye shirika hilo kama mtu wa kufanya usafi, lakini lengo lake halikuwa tu kufanya usafi, bali pia kupata fursa ya kujifunza lugha ya Kiingereza.

Kazi hiyo aliifanya sambamba na kuhudhuria elimu ya watu wazima, ambayo masomo yake yalikuwa yakitolewa usiku katika Shule ya Mtakatifu Barnabas ya Kanisa la Anglicana.

Kiongozi huyo alizaliwa katika mji wa Etunda, Kijiji cha Ongandjera Mei 12, 1929. Mama yake alijulikana kwa jina la Helvi Mpingana Kondombolo aliyefariki dunia mwaka 2008, na baba yake alijulikana kwa jina la Daniel Uutoni Nujoma.

Sehemu kubwa ya maisha yake ya utotoni ilikuwa kuchunga mifugo ya familia na kushiriki shughuli za kilimo kutokana na wakati huo kutokuwa na fursa ya elimu.

Hata hivyo, alipata bahati ya kusoma shule ya misionari ya Okahao alipokuwa na miaka 10 na kumaliza darasa la sita, ikiwa ni elimu ya juu zaidi kufikiwa na mtoto wa Kiafrika wakati huo.

Related Posts