Kisa Fadlu Davids, Waarabu wabadili gia angani

Siku chache baada ya kocha wa Simba, Fadlu Davids kupiga chini ofa ya kujiunga na FAR Rabat, timu hiyo ya Morocco imemchukua kocha wa zamani wa Petro Luanda ya Angola, Alexandre Santos.

Santos ndiye alikuwa akiinoa CS Sfaxien iliyochapwa na Simba katika mechi mbili za hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

FAR Rabat inayomilikiwa na jeshi la nchi hiyo, imemtambulisha rasmi Santos leo, Februari 10, 2025 akichukua mikoba ya Hubert Velud ambaye alitimuliwa kutokana na mwenendo usioridhisha.

Santos amejiunga na FAR Rabat akiwa huru baada ya mwezi uliopita kuachana na CS Sfaxien ya Tunisia kutokana na timu hiyo kutofanya vizuri katika mashindano mbalimbali.

Timu hiyo ya Tunisia, haikuweza kufuzu robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushika mkia kwenye kundi A lililoongozwa na Simba huku CS Constantine ya Algeria ikishika nafasi ya pili na nafasi ya tatu ikiwepo Onze Bravos ya Angola.

Inaripotiwa kwamba kipaumbele cha FAR Rabat kilikuwa ni Fadlu Davids kutokana na kile alichokifanya ndani ya timu yake msimu huu lakini kocha huyo wa Simba amechagua kubakia ndani ya timu hiyo jambo lililoilazimisha klabu hiyo ya Morocco kumfuata Santos.

Davids ameiongoza Simba kutinga robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika huku timu hiyo ikishika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Simba pia chini ya Fadlu Davids imefanikiwa kutinga hatua ya 32 bora ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

Santos aliyechukuliwa na FAR Rabat ni kocha mwenye uzoefu mkubwa na soka la Afrika na amepata mafanikio makubwa katika baadhi ya klabu alizofundisha.

Akiwa na Petro Luanda, aliiongoza kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Angola, mawili ya Kombe la Chama Cha soka Angola na moja la Super Cup.

Kocha huyo pia aliiongoza Petro Luanda kutinga hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara moja.

Related Posts