Laizer atangaza vita mpya TMA

BAADA ya kupata pointi nne katika michezo miwili akiwa na TMA FC ya jijini Arusha, kocha wa kikosi hicho, Mohamed Ismail ‘Laizer’, amesema maendeleo hadi sasa sio mabaya kwake, licha ya kukiri ana kazi kubwa ya kufanya ili kufikia malengo.

Kocha huyo amejiunga na timu hiyo na kuiongoza katika michezo miwili akishinda mmoja kwa mabao 2-1, dhidi ya Geita Gold na sare ya 1-1, mbele ya Polisi Tanzania, akichukua nafasi ya Maka Mwalwisi, aliyeanza nayo msimu na kuiongoza mechi 15.

“Maendeleo sio mabaya kwa sababu nimeanza na timu raundi hii ya pili, wachezaji wote wanaonyesha wako tayari kwa ajili ya kukipambania kikosi ili kifanye vizuri na kufikia malengo yetu ya kumaliza mwishoni mwa msimu huu tukiwa nne bora.”

Kabla ya mchezo wa jana ugenini dhidi ya Biashara United, kikosi hicho kimecheza michezo 17, ambapo kati yake kimeshinda tisa, sare minne na kupoteza minne, kikifunga mabao 27 na kuruhusu mara 17, kikishika nafasi ya tano na pointi zake 31.

‘Laizer’ amejiunga na kikosi hicho ambapo alikuwa kocha msaidizi wa Fountain Gate chini ya Mohamed Muya aliyejiunga na Geita Gold ambao walitimuliwa pamoja Desemba 29, mwaka jana baada ya timu hiyo kucharazwa kwa mabao 5-0, dhidi ya Yanga.

Related Posts