Unguja. Kamisheni ya Zanzibar, Naibu Kamishna wa Polisi, Simon Chillery amewataka maofisa wa madawati ya jinsia na watoto (PGDs) kuongeza nguvu na uadilifu katika kushughulikia kesi za udhalilishaji na ukatili dhidi ya watoto ili kuhakikisha kesi hizo zinafika haraka mahakamani.
Amesema ingawa matukio ya unyanyasaji yanaonekana kupungua kwa asilimia 12.8, bado inahitajika juhudi kubwa za makusudi kuzuia ukiukwaji wa haki dhidi ya watoto na wanawake.
Kwa mujibu wa Naibu Kamishna Chillery, kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, jumla ya kesi 1,116 ziliripotiwa katika vituo vya polisi, ambapo kati ya hizo, 829 zilikuwa za ubakaji.
Kesi hizo zimepungua ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo kesi 1,280 ziliripotiwa, lakini bado kuna changamoto za kushughulikia ukatili huo kwa haraka.
Akiwahutubia maofisa wa polisi wa madawati ya jinsia na watoto katika semina ya siku mbili iliyofunguliwa leo Jumapili, Februari 9, 2025, Chillery amesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuwa na mazingira yanayowaruhusu waathirika kuripoti kesi bila hofu, huku wakipatiwa msaada wa kisaikolojia na huduma sahihi za kisheria.
“Tunaendelea kushuhudia kesi za ubakaji, sodomy (ulawiti), unyanyasaji wa mwili, ndoa za watoto, ujauzito wa vijana na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia,” amesema Chillery.
Ameongeza kuwa kumaliza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ni jukumu la kila mmoja katika jamii, na kwamba maofisa lazima washirikiane kuhakikisha haki za waathirika zinatambuliwa na kulindwa.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Polisi, Maria Nzuki, ambaye ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto kutoka Makao Makuu ya Polisi, Dodoma, amesema ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto bado ni changamoto kubwa katika jamii.
Amesisitiza kwamba kila mmoja anahitaji kuchukua hatua madhubuti ili kupambana na ukatili huu.
“Waathirika wengi wa GBV ni wanawake na watoto, na ni jukumu letu kuzuia ukiukwaji huu.
“Mafunzo haya yatasaidia maofisa kuboresha usimamizi wa kesi kwa kuhakikisha haki inatolewa kwa waathirika kwa njia bora na ya kisheria,” amesema Nzuki.
Amesema kwamba hatua kali zitachukuliwa dhidi ya maofisa watakaoshindwa kutekeleza haki za waathirika, na kwamba utendaji wao utahusisha utoaji wa huduma bora na ufanisi zaidi katika madawati ya jinsia na watoto.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Programu wa UN Women juu ya kumaliza ukatili dhidi ya wanawake, Lucy Tesha, amethibitisha kujitolea kwa shirika hilo katika kushirikiana na Jeshi la Polisi la Tanzania ili kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
“UN Women imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na Jeshi la Polisi, na tutaendelea kutekeleza juhudi zetu za pamoja katika kupambana na vurugu za kijinsia kote nchini,” amesema Tesha.
Amesema semina kama hiyo hufanyika kila mwaka, si tu kuboresha uwezo wa maofisa, bali pia kutoa fursa ya kutafakari na kupanga mikakati ya jinsi bora ya kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia kulingana na takwimu zinazopatikana.