NYOTA wa Tanzania, Madina Iddi na Vicky Elias wameambulia patupu kwenye mashindano ya gofu ya mashimo 36 ya R&A yaliyofanyika Afrika Kusini, mmoja akimaliza nafasi ya 14 huku mwingine akijitoa.
Michuano hii ya siku tatu iliyojumuisha mashimo 54, ilimalizika mwishoni mwa juma katika viwanja vya Leopard Creek, mjini Mpumalanga, Afrika ya kusini na kushirikisha nyota 21 wa Afrika.
Madina alisema kilichomwangusha kwenye michuano hiyo ni matokeo ya siku ya pili na yalimtoa kwenye mchezo.
Aliianza na mashindano 18 ya kwanza kwa kurudisha mikwaju 79 na kushika nafsi ya saba, kabla ya kuwangushwa na alama za siku mbili zilizofuata na alipiga mikwaju 86 katika mashimo 18 ya pili kabla ya kurudisha mikwaju 83 katika mashimo 18 ya mwisho na hivyo kumaliza mashindano na jumla ya mikwaju 248.
“Nimeangushwa sana matokeo dhaifu ya siku ya pili ya mikwaju 86 kwani yalinitoa kabisa mchezoni hadi kupiga mikwaju 83 siku ya mwisho. Lakini ndiyo gofu ilivyo,” alisema Madina ambaye anatokea klabu ya Gymkhana Arusha.
Madina alimaliza katika nafasi ya 14 akifungana na Mganda Peace Kabasweka ambaye pia alipiga mikwaju 248.
Lakini mambo yalikuwa mabaya zaidi kwa Vicky Elias, Mtanzania mwingine aliyeshiriki mashindano hayo akitokea Dar es Salaam.
Kwa upande wa Vicky ambaye alimaliza nafasi ya 18 siku ya kwanza baada ya kupiga mikwaju 86, alilazimika kujitoa katika mashimo 18 ya siku ya pili, sawa na Mganda Martha Babirye.
Wenyeji Afrika Kusini ndio waliotawala orodha ya wachezaji 10 bora ikiingiza majina saba, huku Kenya na Zimbabwe zikichukua nafasi tatu zilizobaki.
Mshindi wa kwanza, Gia Raad alipiga jumla ya mikwaju 212, huku wa pili Bobbi Briown alirudisha mikwaju 214 na wa tatu Lina Coetzer aliyepiga 219 na ni raia wa Afrika Kusini.
Mshindi wa nne, Chanelle Mwangi aliyepiga mikwaju 228 ni Mkenya na ndiye pekee aliyewachachafya magwiji hao wa Bondeni baada ya kuongoza kwa muda mrefu katika mashimo 18 ya siku ya kwanza.
Nafasi za ya tano hadi ya nane pia zilienda kwa Waafrika Kusini, Kesha Louw, Oliva Wood, Izabella Ferreira na Zane Kleyhans huku Wazimbabwe Danielle Bekker na Miriam Masiya wakimaliza nafasi mbili za mwisho tisa na 10.