Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ikamilishe sheria ya anwani za makazi ili kuweka utaratibu wa kisheria utakaowalinda wananchi katika kutumia mfumo huu.
Amesema sheria hiyo itasaidia kuweka masharti ya kimsingi kwa matumizi ya anwani za makazi, ikiwa ni pamoja na kupokea huduma na kuhakikisha kuwa matokeo ya mfumo yanapatikana kwa ulinzi wa kisheria.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi, ambapo amewashauri Watanzania kutambua na kutumia anwani za makazi ili kurahisisha utoaji na upokeaji wa huduma. Pia, amezindua mfumo wa kidigitali wa anuani za makazi (NAPA) jijini Dodoma.
Majaliwa amesisitiza kuwa, licha ya Serikali kugharamia miundombinu ya anwani za makazi, bado kuna baadhi ya wananchi wasiokuwa waaminifu wanaoingilia miundombinu hiyo kwa kuondoa mabango ya anwani na kuyauza. Amesema hili haliwezi kukubalika.
“Tunazo taarifa kwamba anuani za makazi zilizobandikwa kwenye nyumba zetu, vibao tulivyoviweka kuonyesha mtaa na barabara, tuna Watanzania wasiokuwa waaminifu wanaang’oa mabango hayo na kwenda kuyauza,” amesema Majaliwa.
Ameongeza, “Ni muhimu kwa kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hii tuliyoiweka, kwa usalama wetu na uhakika wa mahitaji yetu. Hasa sasa tunapoingia kwenye mfumo wa kidigitali.”
Majaliwa amesema mfumo wa anuani za makazi ni daftari la kidigitali linalokusudiwa kutambua masuala mbalimbali, kama vile kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii, na kuimarisha usalama na ulinzi katika nchi kwa kutambua maeneo ya matukio.
Aidha, amesema mfumo huu utachochea uchumi na ukuaji wa biashara mtandao, na kurahisisha uwezo wa kukabiliana na majanga.
Pia, ameagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana na wadau wa kidigitali ili kuhakikisha utendaji kazi wa mfumo huu unafanikiwa hadi ngazi za vijiji na mitaa.
“Mpango huu ni muhimu ili mfumo huu uweze kufika hadi vitongojini, na kuwanufaisha Watanzania katika maeneo haya,” amesema Majaliwa.
Pia, Majaliwa aliiagiza Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kusimamia utendaji wa mfumo wa anuani za makazi, na kuhakikisha mikoa na halmashauri zote zinawateua waratibu wa mfumo huu na kuwapa mafunzo.
Aidha, amewataka wahakikishe vyombo vya usafiri, hasa vya Serikali, vinatumia mfumo wa NAPA ili kurahisisha utambuzi wa maeneo ya huduma za jamii.
Katika uzinduzi mwingine, Waziri Mkuu amezindua mfumo wa barua ya utambulisho wa kidigitali, ambayo itawawezesha wananchi kupata huduma za utambulisho kwa haraka kupitia ofisi za mitaa, badala ya kusubiri kwa muda mrefu.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Slaa, amesema wizara yake imeandaa mpango wa miaka miwili wa kuhakikisha waratibu na watendaji wote wapatao 21,487 wa mikoa na halmashauri za Tanzania Bara na Zanzibar wanapatiwa vishikwambi vya anwani za makazi.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayub Mohamed Mahamudu, ametangaza kuwa asilimia 100 ya Zanzibar imeshaingizwa kwenye mfumo wa anwani za makazi, na nyumba zote zimepatiwa namba, jambo linalorahisisha wageni kujua maeneo wanayokwenda.